Wadau waeleza ushirikiano unavyoleta maendeleo thabiti

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa, ushirikiano baina ya sekta binafsi na umma ni nguzo muhimu ya kuhakikisha Tanzania inafanikisha Dira ya Maendeleo ya 2050, inayolenga kujenga Taifa jumuishi kidijitali, lenye uchumi thabiti, jamii yenye ustawi na utunzaji wa mazingira.

Hayo yameelezwa leo Jumanne, Agosti 26, 2025 na wadau waliohudhuria uzinduzi wa Ripoti ya Ujumuishi wa Mazingira, Kijamii na Utawala (ESG) ya Vodacom Tanzania iliyokwenda sambamba na mjadala kuhusu masuala muhimu na namna yanavyopaswa kushughulikiwa.


Mjadala huo ulioandaliwa kwa kushirikiana na Mwananchi Communications Limited (MCL) ulikuwa na kauli mbiu isemayo ujumuishi kwa ajili ya watu bora, sayari na uwezekano.

Viongozi wa Serikali, asasi za kiraia, wadau wa mazingira na wabia wa maendeleo walihudhuria.

Katika hafla hiyo Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo aliyekuwa mgeni rasmi amesema katika kuhakikisha ulimwengu wa kidijitali unashika kasi kwa kila Mtanzania lazima watu wawezeshwe kidijitali bila kusahau ushirikiano wa sekta binafsi sambamba miundombinu na sera madhubuti.

Amesema suala lililopo watu wanafuata huduma za Serikali kwa kwenda ofisini bali dunia ya sasa ilipo na lengo la Serikali hata katika Dira ya 2050 ni Serikali si tu kuwa karibu zaidi na watu bali iwafuate watu walipo na hilo linawezekana kupitia uboreshwaji wa kidijitali.

Amesema watu hawapaswi kuachwa katika ulimwengu huo bali inabidi wawezeshwe kuhakikisha wanashiriki hatua inayosaidia hata katika majukumu ya Serikali kuhudumia wananchi wake na hilo linawezekana kupitia upatikanaji.


“Tunachotazamia katika miaka ijayo si tu Serikali kuwa karibu na watu bali inayowafuata watu mahali walipo na hilo linawezekana, hapa ndipo ushirikiano kama wa Vodacom unapohitajika,” amesema.

Katika kufanikisha hilo,  Profesa Kitila amesema Serikali haitaki tena kuonekana kama mkusanyaji kodi pekee, bali kama msimamizi wa mazingira wezeshi yatakayosaidia sekta binafsi kustawi, huku ikiwafuata wananchi walipo kidijitali.

“Ulimwengu wa leo na tunakoelekea katika miaka ijayo si Serikali kuwa karibu tu na watu, bali Serikali inayowafuata wananchi walipo. Hilo linawezekana kupitia mageuzi ya kidijitali,” amesema Profesa Kitila.

Amesema  Serikali inaendelea kuwekeza kwenye sera thabiti na miundombinu ya kisasa ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kidijitali unakuwa wa uhakika.

Amesema ushirikiano na kampuni binafsi kama Vodacom ni muhimu ili huduma hizo zipatikane kwa bei nafuu na kwa upana zaidi.

Profesa Kitila amesema mtazamo mpya wa Serikali ni kuona sekta binafsi kama mshirika wa maendeleo, na si mchangiaji kodi pekee.

 “Tunapaswa kushirikiana si kwa masharti ya kodi pekee, bali katika kuibua suluhu za kijamii na kiuchumi zinazogusa maisha ya watu,” alisema Profesa Kitila.

Akizungumzia mafanikio yaliyowasilishwa katika ripoti iliyozinduliwa na mikakati ya kampuni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire amesema safari ESG ni ya kila mmoja; na kila mtu anapaswa kushiriki kulingana na nafasi yake.

“Kwa miaka 25 tumekuwa daraja la muunganisho (connectivity) kwa Watanzania, kwa sababu tunaamini huduma na bidhaa jumuishi hujengwa juu ya msingi wa upatikanaji. Ujumuishi unamaanisha kila mmoja kushiriki Watanzania wa kawaida waweze kupata, kutumia na kushirikiana ipasavyo katika ulimwengu wa kidijitali,” amesema Besiimire.


Kwa upande wa sekta binafsi Besiimire amesisitiza umuhimu wa kuunganisha dhana ya uendelevu katika shughuli za biashara ili kuchochea athari chanya za kijamii na kiuchumi kwa muda mrefu.

“Uendelevu unapaswa kuunganishwa moja kwa moja katika namna tunavyofanya biashara. Huwezi kuuchukulia kama jambo la pembeni,” amesema Besiimire na kufafanua kuwa kujenga uendelevu hakumaanishi tu kuwa na sera au matamko.

“Kunahitajika kujenga uwezo sahihi, kuendeleza vitendo vinavyowajibika, na kuhakikisha kila uamuzi unachangia thamani ya kudumu kwa wateja wetu, jamii na mazingira,” amesema bosi huyo wa kampuni ya simu.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Vodacom Tanzania, Zuweina Farah amesema kuwa mikakati ya ESG ya kampuni hiyo inalenga watu kwanza.

“Tunajitokeza wakati wa majanga, tunatoa msaada wa dharura, tunalinda sayari kupitia miradi ya mazingira na tunadumisha uaminifu kwa kulinda wateja dhidi ya ulaghai na usalama wa data,” amesema.

Pia, amesema msingi wa ushirikiano wowote ni kuendana kwa mikakati ya pande zote, akisema kampuni yao inalenga kusaidia jamii mbalimbali kwa kujumuisha na kujiandaa na majanga, kutoa msaada wa dharura na kujitokeza pale jamii zinapohitaji msaada.

“Kulinda sayari, suala hili linafanikishwa kupitia mipango inayojali mazingira. Pamoja na kudumisha uaminifu kwa kuhakikisha wateja wanapata ulinzi wa data na usalama mtandaoni,” amesema Farah.

Pia, amesema Vodacom inatambua kuwa uunganishaji wa kidijitali (connectivity) ni muhimu ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata ulimwengu wa kidijitali.

Amesema zaidi ya hayo, kampuni inalinda wateja wake kupitia kampeni za uhamasishaji kuhusu ulaghai, ulinzi wa data na usalama wa mitandao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia, amesema vyombo vya habari ni kiungo muhimu katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya 2050 kupitia elimu ya umma, ushawishi wa sera na uwajibishaji wa viongozi.


“Hii hafla ni sehemu ya safari ya kuelekea Dira ya Taifa ya 2050, inayohitaji uongozi shupavu, ushirikiano jumuishi na uwajibikaji. Vyombo vya habari havipaswi kuishia kuripoti matukio pekee, bali vina wajibu wa kufahamisha, kuhamasisha mjadala wa kitaifa na kukuza utamaduni wa uwazi na ubunifu,” amesema.

Pia, amesema nguzo za ESG za Vodacom kuwawezesha watu, kuilinda sayari na kudumisha uaminifuzinaendana moja kwa moja na malengo ya Dira ya Taifa ya 2050 lakini pia kauli mbiu ya Mwananchi ya kuliwezesha Taifa.