MABINGWA wa kihistoria wa Fainali za Ubingwa kwa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024, Morocco wamefuzu fainali ya michuano hiyo kwa kuivua ubingwa Senegal.
Katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa leo Agosti 26, 2025 kwenye Uwanja wa Mandela uliopo Kampala nchini Uganda, mikwaju ya penalti 5-3 imetosha kuifanya Morocco kuwa mbabe mbele ya Senegal, timu iliyokuwa inatetea ubingwa wake iliouchukua michuano iliyopita iliyofanyika nchini Algeria.
Hatua hiyo ya mikwaju ya penalti imekuja kufuatia dakika 120 matokeo kuwa sare ya bao 1-1.
Beki Joseph Layousse Samb alianza kuifungia Senegal dakika ya 16, bao hilo lilidumu kwa takribani dakika saba kabla ya kiungo wa Morocco, Sabir Bougrine kusawazisha.
Kipindi cha kwanza cha mchezo huo kilikuwa cha vuta nikuvute, lakini hadi mwamuzi Jelly Alfred Chavani kutoka Afrika Kusini anapuliza filimbi kuashiria kuashiria kutamatika kwa dakika 45, matokeo yalikuwa sare.
Kipindi cha pili, kwa msaada wa VAR, Morocco ilibaki na wachezaji wake wote 11 hadi mwisho wa mchezo baada ya dakika ya 56 adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa beki Marouane Louadni kubadilishwa na kuwa ya njano.
Katika mikwaju ya penalti, Morocco ilianza kupiga kupitia nahodha Mohamed Rabie Hrimat, akafunga, kabla ya Senegal kukosa, mkwaju uliopigwa na Seyni Mbaye Ndiaye.
Baada ya hapo, wachezaji wote waliopiga walifunga ambapo upande wa Morocco walikuwa Oussama Lamlioui, Ayoub Khairi, Anas Bach na Youssef Mehri.
Senegal waliofunga ni Vieux Cissé, Baye Assane Ciss na Daouda Ba.
Kwa ushindi huo, Morocco inakwenda kucheza fainali ya CHAN 2024 dhidi ya Madagascar, itakayofanyika Agosti 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Moi uliopo Nairobi, Kenya.
Siku moja kabla kwa maana ya Agosti 29, 2025, kwenye Uwanja wa Mandela uliopo Kampala nchini Uganda, Sudan itakabiliana na Senegal katika mechi ya kusaka nafasi ya tatu.
Ikumbukwe kuwa, Morocco ndiyo timu yenye rekodi mbili za kipekee katika historia ya CHAN baada ya kushinda ubingwa mwaka 2018 ikiwa timu mwenyeji, kisha 2020 ikatetea taji lake, hakuna iliyowahi kufanya hivyo.
Morocco inasaka taji la tatu la CHAN baada ya kushinda 2018 na 2020 ikitaka kuandika rekodi ya timu iliyotwaa ubingwa huo mara nyingi zaidi, huku Madagascar ikisaka ubingwa wa kwanza kufuatia michuano iliyopita kushika nafasi ya tatu.