KATI ya masharti matatu iliyopewa Simba kukamilisha usajili wa kipa wa JKT Tanzania, Yakoub Suleiman, imeyatimiza mawili, lililobaki lipo hatua za mwisho ili kumtangaza mchezaji huyo kuwa mali ya klabu hiyo.
Ipo hivi; Simba iliambiwa ili Yakoub awe mali yake pesa ya usajili iingizwe kwenye akaunti ya JKU, mchezaji mwenyewe na JKT Tanzania aliyokuwa akiitumikia kwa mkataba wa makubaliano kati ya pande hizo tatu hadi 2027.
Lakini, jambo la tatu ni lile la JKT kupata mgawo wake na pia ipewe wachezaji watatu kwa mkopo kutoka Simba.
Mwanaspoti limenasa taarifa za ndani zinazodai tayari Simba imeweka pesa katika akaunti ya timu ya JKU, Yakoub na juzi Jumatatu kikao na JKT Tanzania kilikuwa hatua za mwisho kukamilisha hilo.
“JKT Tanzania ilikuwa inahitaji sana kuendelea na huduma ya Yakoub aliyemaliza msimu uliyopita akiwa na ‘cleansheet’ 10, lakini Jumatatu walikaa kikao kilichoenda vizuri, hivyo ndani ya siku mbili hizi kila kitu kitakuwa sawa,” kilisema chanzo na kuongeza:
“Japokuwa viongozi wa Simba walikuwa wanapambana ili mchezaji akaungane na wenzake Misri, nadhani kwa muda uliosalia Simba kurejea nchini anaweza akaungana nao Dar es Salaam, ila kwa sasa mchezaji yupo mapumziko baada ya kutoka katika majukumu ya timu ya Taifa ya Tanzania iliyokuwa inashiriki CHAN.”
Alipotafutwa katibu wa JKU, Khatib Shadhil alisema: “Sisi na Simba mambo yameenda sawa kuhusiana na Yakoub ambaye ni askari wa JKU, hivyo anaposajiliwa na timu nyingine lazima timu ipate fungu lake, ila nikujibu kwa kifupi sana, sisi na Simba tupo sawa.”
Mbali na Yakoub, Simba ilihitaji huduma ya beki Wilson Nangu ambaye msimu uliopita alifunga mabao mawili na asisti mbili pia ishu yake imefikia pazuri anaweza akaruhusiwa kujiunga na Wanamsimbazi.
“Nangu mkataba wake na JKT Tanzania ulikuwa unamalizika mwaka 2028, lakini ishu yake ipo hatua nzuri maana JKT Tanzania licha ya kutaka pesa pia iliwaomba wachezaji watatu kwa mkopo ambao ni Awesu Awesu, David Kameta, Valentino Mashaka,” kilisema chanzo hicho.
Beki wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Amir Maftah alisema endapo Simba itafanikisha usajili wa Nangu itafaidika naye kwa miaka ya mbele, kutokana na ari yake ya kujituma na kupambana uwanjani.
“Ni beki anayejitolea sana uwanjani, hata kama hatapata namba kwa uharaka ila naamini akijengwa kwa manufaa ya baadaye atafanya mambo makubwa na atakuwa tunu kwa Simba na Taifa Stars,” alisema.