Mambo matatu ya kitasa kipya Yanga

Kuna mambo yataanza kuonekana msimu ujao pale Jangwani, ambapo mastaa kibao wamesajili na kuna dalili kwamba vita ya namba, lakini namna shoo za uwanjani zitakavyokuwa.

Lakini, unaposoka hapa elewa kwamba ndani ya kikosi cha Yanga kuna nyota wawili wanaounda ule ukuta wa chuma ambao msimu waliruhusu mabao 10 tu kuvuka na kutinga ndani ya nyavu zao kwenye mashindano ya Ligi Kuu Bara, jambo ambalo liliifanya kuwa timu iliyoruhusu mabao machache zaidi.

Hata hivyo, msimu huu kile kitasa kipya cha Yanga, Frank Assinki, kinaendelea kujichafua huko mazoezini, huku usajili wake ndani ya klabu hiyo ukidaiwa kuwa na faida tatu Jangwani.

Ukiweka kando hilo, kuna kocha mmoja Mfaransa amekizungumzia kwamba, jamaa ni kama toleo la Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, hivyo Yanga “imepata mtu wa maana.”

Kocha huyo si mwingine, bali ni yule aliyewahi kuinoa Yanga, Miloud Hamdi ambaye alipoondoka mwisho wa msimu uliopita ndipo akatua Romain Folnz.

Hamdi ambaye pia ana uraia wa Algeria alisema anamfahamu Assinki kwa muda mfupi aliofanya naye kazi ndani ya Singida Black Stars akidai kwamba kitendo cha Yanga kumshusha beki huyo ni sawa na kuingiza Bacca mpya kikosini.

Miloud ambaye baada ya kuipa Yanga makombe matatu ambayo ni Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA alitimkia Ismailia ya Misri, alisema alikutana na Assinki alipotua Singida Black Stars na kwa muda mfupi tu aliukubali ubora wake.

Mfaransa huyo akimuelezea Assinki, alisema ni beki wa kazi anayejua sehemu ya kutumia nguvu na akili kama ambavyo anafanya Bacca.

“Nilipokuwa Singida nilimkuta Assinki japo sikukaa naye sana, lakini siku ambazo alifanya mazoezi nilimpenda, hata ningebaki pale ningemsajili,” alisema Miloud na kuongeza:

“Assinki ni beki anayejua wapi atumie akili na wapi atumie nguvu, sio beki rahisi kukubali matokeo, kama amekwenda Yanga wamepata beki mzuri ambaye ni kama wamepata Bacca mwingine.”

Hamdi aliongeza kuwa Assinki ataipa utulivu Yanga hata kama siku akikosekana Bacca au nahodha msaidizi, Dickson Job kwenye eneo la beki wa kati, huku akitoa angalizo kwa mabeki hao kwani presha ya namba itaongezeka. “Nakumbuka tangu nikiwa Yanga, kulikuwa na hesabu za kusajili beki wa kati, kuna wakati Bacca alipokuwa akikosekana kulikuwa na presha itakuwaje, kwahiyo najua walikuwa wanatafuta beki mwenye ubora kama wa hao wawili.

“Kuja kwa Assinki kutaongeza presha ya ushindani kwa Job na Bacca lakini ni faida kubwa kwao, ikitokea Bacca au hata Job, mmoja hayupo, kutakuwa na Asinki, hapo hakuna tena shida.

“Vitu vingine vizuri kwa Assinki ni kwamba anaweza kukaba kwa chini au hata juu kutokana na urefu wake, ukiamua kuongeza ugumu kwa wapinzani unaweza kuwabakisha Bacca na Job uwanjani na kisha ukamuongeza Asinki, inategemea kocha wao ataamua kuwatumia kwa namna gani,” alisema Hamdi ambaye Desemba 2024 alitambulishwa kuwa kocha wa Singida Black Stars, kabla ya Februari 4, 2025 kuibukia Yanga akienda kuchukua nafasi ya Sead Ramovic.

Assinki ambaye alianza kuitumikia Singida Black Stars kipindi cha dirisha dogo msimu uliopita, alicheza michezo 12 kati ya 15 ya Ligi Kuu Bara huku mitatu pekee akianzia benchi na mingine akiwa kikosi cha kwanza.

Nyota huyo raia wa Ghana ambaye kiasili ni beki wa kati, faida ya kwanza anayokwenda kuipa Yanga ni eneo hilo ambalo kwa muda mrefu Job na Baaca wamekuwa wachezaji muhimu, huku nahodha Bakari Mwamnyeto akiwa mbadala wao. Hali hiyo ikalilazimu benchi la ufundi kumtoa kiungo mkabaji, Aziz Andabwile kucheza beki wa kati.

Faida ya pili, Assinki ana uwezo wa kucheza beki wa kulia, eneo ambalo kuna Israel Mwenda na Shomari Kibwana, hiyo ni baada ya Kouassi Attohoula Yao kuwa na majeraha ya muda mrefu, hivyo amewekwa kando.

Mwisho kabisa, Assinki anaweza kucheza beki wa kushoto, eneo alilokuwa anacheza Nickson Kibabage kabla ya hivi karibuni kupelekwa Singida Black Stars kwa mkopo na kumuacha Chadrack Boka, kisha ukafanyika usajili wa nahodha wa zamani wa Simba, Mohamed Hussein.

Endapo maeneo hayo ya kulia na kushoto ikitokea kuna upungufu, Assinki anaweza kuziba mapengo hayo na kuiweka salama Yanga. Lakini pia kocha akitaka kutumia mfumo wa mabeki watatu, bila shaka Job, Baaca na Assinki, watakuwa wachezaji muhimu zaidi kuilinda ngome ya timu hiyo.

Ikumbukwe kuwa, usajili wa Assinki umemuondoa kwenye mfumo aliyekuwa beki wa kulia wa timu hiyo, Kouassi Attohoula Yao siyo kwa sababu ya uwezo bali majeraha ya mara kwa mara, huku akiondolewa kwa lengo la kutimiza kigezo cha wachezaji 12 wa kigeni.

Uwepo wa beki huyo unaifanya Yanga sasa kuwa na wachezaji 12 wa kimataifa wanaotakiwa ambao ni Djigui Diarra, Duke Abuya, Mohammed Douambia, Celestine Ecua, Andy Boyell, Prince Dube, Maxi Nzegeli, Lassane Kouma, Moussa Balla Conte, Chadrack Bocca na Pacome Zouzoua.

Usajili huu unaifanya Yanga kuwa imesajiliwa wachezaji 11, kati ya hao sita wa kigeni ambao ni Mohammed Douambia, Celestine Ecua, Andy Boyeli, Lassane Kouma, Moussa Balla Conte na Frank Assinki.

Wazawa wapya ni Offen Chikola, Abdulnassir Mohamed Abdallah ‘Casemiro’, Abubakar Nizar Othuman ‘Ninju’, Mohamed Hussein na Edmund John.