Msuva adai CHAN 2024 ina darasa kali

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva ambaye anacheza soka la kulipwa nchini Iraq katika kikosi cha Al-Talaba SC, ameeleza kuwa mashindano ya CHAN 2024 yataacha somo kubwa kwa soka la Tanzania, ambalo linaweza kuwa msingi wa mafanikio katika mashindano yajayo.

Msuva ambaye kabla ya mchezo wa ufunguzi kati ya Taifa Stars dhidi ya Burkina Faso aliahirisha safari yake binafsi na kwenda kambini kuwapa moyo wachezaji wa Stars, alisema hisia hizo zilikuwa muhimu kwa kujenga morali ya kikosi.

“Nilihisi ni wajibu wangu kuwapunguzia wachezaji hofu kabla ya kuingia uwanjani. Soka la Tanzania linakua kwa kasi, na mashindano haya yameonyesha kwamba tuna uwezo wa kushindana na timu bora barani Afrika,” alisema Msuva.

Mshambuliaji huyo aliendelea kwa kubainisha kuwa kuishia hatua ya robo fainali hakupaswi kuangaliwa kama kushindwa, bali ni mafanikio makubwa kwa Taifa Stars.

“Robo fainali ni rekodi kwa Taifa Stars. Hatujawahi kufika hatua hiyo nyuma, na hili ni somo kubwa kwa wachezaji wetu wa ndani na timu nzima,” alisema.

Msuva ambaye alizichezea Difaa El Jadida na Wydad Casablanca za Morocco kabla ya kwenda Saudia na sasa Iraq, alisema uzoefu uliopatikana CHAN utasaidia wachezaji wa Tanzania kuwa na nidhamu na mbinu bora zaidi katika mashindano yajayo.

“Tunatakiwa kutumia uzoefu huu kujenga timu yetu. Hii ni changamoto na fursa kwa wachezaji wote, kutoka wachezaji wa ndani hadi wale wa kimataifa,” aliongeza.

Alionyesha pia umuhimu wa mashabiki kushirikiana na timu ili kuendeleza soka la Tanzania.  “Mashabiki wapo kwa ajili ya timu. Tupo hapa kwa ajili ya Taifa na kwa mashabiki wetu, na lazima tushirikiane kuona soka la Tanzania likikua zaidi,” alisema.

Msuva alimpongeza kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, kwa juhudi za kuhakikisha wachezaji wa ndani wanapata nafasi ya kuonyesha vipaji.

“Kocha Morocco amefanya kazi nzuri. Kuleta wachezaji wa ndani na kuwakilisisha kikosi kikubwa ni hatua nzuri. Hii inatupa somo kubwa la jinsi ya kuendeleza wachezaji,” alisema Msuva.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga alisema mashindano ya CHAN yameonyesha kwamba Tanzania ina wachezaji wenye uwezo wa kushindana na sio kushiriki kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Taifa Stars iliishia robo fainali katika mashindano hayo wikiendi iliyopita baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Morocco.

Mashindano hayo yanayofanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, yalianza Agosti 2 na yanatarajiwa kufikia tamati Agosti 30 mwaka huu ambapo jana zilichezwa mechi za nusu fainali.