Gamondi kuitumia Kagame kunoa makali CAF

KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi amesema mashindano ya Kagame yatamsaidia kuandaa timu shindani kuelekea mechi za ligi na kimataifa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema anafurahishwa na mwenendo wa maandalizi huku akidai kuwa wachezaji wake wapo kwenye hali nzuri ya ushindani matarajio yao ni makubwa.

“Timu inaendelea vizuri licha ya kwamba sio wachezaji wote wapo kikosini wanaendelea kuungana nasi kidodo kidogo lakini matarajio ni makubwa na wachezaji wengi wapo tayari kwa ushindani,” alisema na kuongeza:

“Nahitaji kuwa na kikosi chote kambini ili kuwa na machaguo sahihi. Nafikiri siku zinavyozidi kwenda wachezaji wengi wanawasili na nafikiri mashindano haya ambayo tumepata nafasi ya kushiriki yatatoa mwanga mzuri kwetu.”

Gamondi alisema ni nafasi sahihi kwao kushiriki michuano hiyo baada ya kufanya mazoezi kwa muda na kukosa mechi za kirafiki zilizo na hadhi ya ushindani, hivyo wanaamini michuano hiyo itawapa nafasi ya kufanya kitu sahihi na kutambua ubora na udhaifu.

“Ni michuano mizuri inakutanisha timu nyingi, hivyo tutapata mechi nyingi ambazo zitaongeza utimamu kwa wachezaji ukiondoa mazoezi ya kuchezea mipira uwanjani tunahitaji mechi nyepesi na ngumu ili kujua upungufu na ubora wetu,” alisema.

Gamondi alisema wamejiandaa na mikakati ni kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye michuano hiyo ili kuwapa mwanga mzuri wapi wanaanzia kimataifa na ligi ya ndani.

“Tuna timu nzuri ambayo imesheheni vipaji vikubwa na uzoefu… nafikiri hili litathibitishwa kwenye uwanja wa mashindano na naamini tutapata maandalizi mazuri kupitia mashindano hayo ambayo yanatarajia kuanza mapema mwezi ujao.”

Gamondi amejiunga na Singida Black Stars baada ya kuiongoza Yanga kwa misimu miwili akiipa mataji ya ndani na kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.