Israeli yaua wanajeshi sita wa Syria

Maofisa sita wa Jeshi la Syria wameuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Israel kusini mwa Damascus, kituo cha televisheni ya Serikali ya Syria, El Ekhbariyaimeripoti.

Mashambulizi hayo yamefanyika ikiwa ni siku moja baada ya Syria kulaani kile ilichokiita “uvamizi wa kijeshi” mpya wa Israel, nje ya mji mkuu Damascus.

Ndege zisizo na rubani za Israel zililenga ngome za jeshi la Syria katika maeneo ya vijijini karibu na mji wa al-Kiswah, kituo hicho cha televisheni kimeripoti leo Jumatano Agosti 27, 2025, kama ilivyoelezwa na kituo cha Aljazeera.

Baada ya kuanguka utawala wa Bashar al-Assad, Desemba mwaka jana, Israel imeanzisha mashambulizi ikilenga maeneo ya kijeshi na mali ndani ya Syria.
Israel pia imekuwa ikipanua eneo lake la utawala katika milima ya Golan upande waSyriakwa kutwaa eneo la mpaka lililopaswa kubaki bila jeshi, hatua iliyokiuka makubaliano ya kujiondoa kijeshi ya mwaka 1974.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria ilisema Jumatatu Agosti 25, kwamba Israel ilituma wanajeshi 60 kudhibiti eneo lililo ndani ya mpaka wa Syria.

Eneo hilo lipo karibu na Mlima Hermon, jirani na kilima cha kimkakati kinachoangalia Beit Jinn, karibu na mpaka wa Lebanon kusini mwa Syria. Israel haikutoa maoni mara moja kuhusu shutuma hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Asaad al-Shaibani, aliishutumu Israel kwa kujenga vituo vya kijasusi na ngome za kijeshi katika maeneo yaliyopaswa kubaki bila jeshi, ili kusukuma mbele “mipango yake ya upanuzi na mgawanyo.”

Mapema mwezi huu, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu aliweka hadharani maono yake ya “Israeli kubwa” dhana inayoungwa mkono na Waisraeli wenye misimamo mikali ya utaifa, ambayo inadai umiliki wa Ukingo wa Magharibi, Gaza na sehemu za Lebanon, Syria, Misri na Jordan.

Muungano wa nchi 31 za Kiarabu na Kiislamu pamoja na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, ulisema msimamo huo ni uvunjaji wa wazi na hatari wa kanuni na sheria za kimataifa na misingi ya mahusiano ya kimataifa yenye uthabiti.