Malalamiko ni silika ya kawaida kwa mwanadamu yeyote. Pale anapoguswa na hali isiyompendeza, mtu hataacha kulalamika hata iwe kwenye mambo madogo kiasi gani.
Mmoja atalalamikia uhuru na haki zake, lakini mwingine atalalamika hata aking’atwa na mbu. Wataalamu wanasema malalamiko ni dawa ya kuepusha msongo, ni mbaya sana kuishi na vijiba rohoni.
Malalamiko yanataka kufanana kidogo na maswali, lakini tofauti ni kwamba maswali hutangulia na malalamiko huja baadaye. Kwenye jambo lolote lisiloeleweka, watu huwa na maswali.
Dawa ya maswali ni majibu, na kutokuwapo kwa malalamiko hutegemea majibu ya maswali hayo. Iwapo muulizaji hatojibiwa au kutoridhishwa na majibu atakayopewa, hapo sasa ataanza kulalamika.
Kulalamika ni haki ya kila mtu.
Si mara zote watu wanajibiwa kwa jinsi wanavyotegemea, hivyo ni lazima kuwa na malalamiko. Wapo wenye ujasiri wa kulalamika hadharani, lakini wengine huogopa kutokana na aina ya malalamiko yao.
Hivyo hulalamikia mtimani hadi pale muujiza wa “sauti ya bubu” unapotokea. Hii ni hatari kwani sauti hiyo inajulikana uzito wake hata kama haisikiki.
Wakati huu tunaoelekea uchaguzi mkuu, ni wakati wa shughuli nzito (tena ya lawama) kwenye jamii yetu. Kulingana na tofauti za itikadi za wananchi, tunategemea maswali mengi sana. Si rahisi kuyajibu yote, na hata yakijibiwa si rahisi kumridhisha kila muulizaji.
Wengine huwa na majibu yao, au namna maswali yao wanavyotaka yajibiwe. Lakini pamoja na hao, wapo wenye maswali ya msingi yanayohitaji majibu ya msingi.
Hivi karibuni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imekanusha uvumi unaoenea mitandaoni ukidai kuwa mfumo wa uchaguzi umeunganishwa na mifumo mingine kinyemela.
Inadaiwa kuwa mfumo huo umeunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na chama fulani cha siasa. Kubwa zaidi, kuna madai kwamba zoezi la kupiga kura tayari limekamilika, kilichobaki ni kutangazwa kwa matokeo tu.
Sanjari na hilo, Tume pia inaumiza kichwa kwa mjadala ulioanza baada ya kutangaza idadi ya wapigakura katika daftari la kudumu. Hesabu inaonesha waliojiandikishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 imefikia zaidi ya milioni 37.5. Tume imebainisha kuwa kati ya wapigakura hao, Milioni Saba na Nusu ni wapya, sawa na ongezeko la asilimia 26.55 kutoka idadi ya waliokuwamo kwenye daftari mwaka 2020. Haya tunaweza kuyaita vyovyote tupendavyo, lakini hayana budi kutolewa fafanuzi. Si ajabu pia yakawa ni maswali au hata malalamiko.
Wapo watu wanaouliza na kulalamika kwa njia mbadala kama namna ya kutumia tafsida. Inafikirisha sana ukutanapo na mtu anayekuuliza “hivi hilo shati umelifua lini?” Au “tangu lini hujaenda kwa kinyozi?” Ni lazima nawe utajiuliza kama shati lako linanuka au ndevu zako zimekosa ushirikiano.
Swali ni je, inawezekana nusu ya Watanzania ni wapigakura? Ni vema Tume ikajiridhisha iwapo takwimu zao zipo sahihi. Inawezekana kwa jambo hilo kuwapo iwapo tu litathibitishwa rasmi na Tume.
Hapo ndipo tutakapotazama ni kwa nini Watanzania wa leo wamekuwa na mizuka ya kushiriki uchaguzi huu. Labda ni ishara nzuri kwa chama fulani na mbaya kwa chama kingine kinachogombea uongozi katika msimu huu.
Lakini izingatiwe kuwa sio rahisi kuyajua yote yanayoendelea huku mtaani. Kila wakati jambo jipya huibuka, lakini yanayojitokeza au kujulikana ni yale makubwa zaidi.
Ndio maana nasisitiza kila swali lijibiwe, na kila changamoto itatuliwe kabla ya malalamiko. Ningelikuwa mtabiri ningesema “kura hewa, usajili mara mbili na majina hewa kwenye daftari zitakuwa changamoto kuu”.
Wasiwasi wangu ni sisi kuingia kwenye historia mbaya kama ilivyokuwa kwa wenzetu. Katika ripoti zinazosomeka duniani, Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe ilisajili zaidi ya watu milioni 5.8 kupiga kura mwaka 2018.
Lakini sensa yao ilionesha wapigakura walikuwa chini ya milioni 5.5. Kwa maoni yangu, Tume yao ilipaswa “kuongea vizuri” na wananchi maana sidhani kuwa waliweza kujieleza. Kituko hicho kilikifuata kile cha Equatorial Guinea mwaka 2016. Wapigakura walioripotiwa walikuwa 325,548 karibu sawa na watu wote wa umri wa kupiga kura. Mwisho wa yote Rais Teodoro alipata ushindi wa kishindo wa asilimia 92.7 ya kura zote.
Maswali yalikuwa je, ni wapigakura wote walijiandikisha? Kama wote walijiandikisha, wote walipiga? Hakuna kura zilizoharibika?
Matukio haya yananikumbusha mwamba wa kuitwa Charles King. Mwaka 1927 nchini Liberia, huyu bingwa alishinda kwa kura zilizozidi idadi ya watu.
Waliojiandikisha walikuwa 15,000 lakini bingwa alishinda kwa kishindo cha kura 243,000 kulinganisha na kura alizopata mpinzani wake 9000.
Ikumbukwe kwa miaka hiyo nchi ile haikuwa na idadi kubwa ya watu kutokana na athari za utumwa. Hivyo kura alizopata mshindi zilizidi idadi ya raia.
Kwa wenzetu hawa, bila shaka walikutana na maswali na malalamiko kabla ya kuingia kwenye rekodi. Haitoshi kwa Tume kukanusha “madai” tu, inapaswa kujua vyanzo vya vumi hizi na kuviweka hadharani.
Mjue adui yao kabla ya kuingia vitani, utakuwa na wepesi wa kuondoa malalamiko ya Watanzania. Vinginevyo rekodi kama za wenzetu zitatuhusu.