NIKAGEUKA na kumtazama mtu huyo aliyekuwa nyuma yangu na kumuuliza.
“Ndiye yeye….amepatwa na nini sijui…?”
“Inaonekana amejinyonga au amenyongwa.”
“Ndiyo maana tangu jana sijamuona. Kumbe…!”
Nikageuza uso tena na kuitazama ile maiti iliyokuwa inaning’inia.
“Kama si wewe nisingetambua kama yeye ndiye Frank. Huyu jamaa anaishi na nani humu ndani?”
“Anaishi peke yake. Aliwahi kuniambia kuwa aliachana na mke wake lakini alikuwa na mpango wa kuoa tena.”
Nikashusha pumzi ndefu na kutoa kitambulisho changu na kumuonyesha mtu huyo.
“Mimi ni ofisa wa polisi. Nilielekezwa nije hapa kwa ajili ya kuonana na huyu mtu. Nilikuwa na mahojiano naye. Sasa kwa vile wewe ni mkazi wa nyumba hii ninataka unisaidie kitu kimoja.”
“Mimi ni mkazi wa nyumba hii sawa, lakini kila mtu anaishi upande wake.”
“Ninajua. Suala ninalokuhitajia wewe ni la ushahidi.”
“Kwamba huyu ndiye Frank na pili umeshuhudia mwili wake ukining’inia kwenye kitanzi,”
“Kushuhudia nimeshuhudia.”
“Subiri nipige simu polisi halafu tutaongea.”
Nilitoa simu yangu nikampigia mkuu wa kituo cha polisi cha Chumbageni na kumueleza tukio lililokuwa limejiri na kuomba msaada wa polisi.
Baada ya kuzungumza na mkuu wa kituo huyo nilimuuliza yule mtu niliyekuwa naye.
“Naitwa Elias Mambo.”
Elias aligutuka alipoona ninatoa notibuku na kuandika jina lake.
“Tuingie,” nikamwambia.
Tukaingia katika ile nyumba.
“Huyu jamaa anafanya kazi wapi?”
“Alivyonifahamisha yeye mwenyewe ni mtaalamu wa umeme.”
“Anafanya kazi zake binafsi?”
“Unajua mimi mwenyewe nina wiki tatu tu tangu nimehamia katika nyumba hii. Kwa hiyo watu wote humu ndani ninawafahamu kijuu juu tu.”
Dakika chache baadaye, polisi sita kutoka kituo cha polisi cha Chumbageni waliingia katika nyumba ya Frank.
“Kumetokea nini?” mmoja wa polisi hao ambaye alikuwa ni koplo akaniuliza.
Nikawaeleza kilichojiri. Polisi wenzangu nao wakashangaa. Walishangaa kwa sababu huyo mtu aliyenyongwa au kujinyonga nilimfuata kwa tatizo la mwenzake ambaye naye alinyongwa.
Polisi walianza kuupiga picha mwili wa mtu huyo ukiwa bado unaning’inia. Baada ya hapo tukapanda kwenye meza na stuli na kuushusha chini. Tulipokiondoa kitanzi kwenye shingo yake tukaona kipande cha karafasi kilichokuwa kimekunjwa.
Kwa vile kicheo mimi ndiye niliyekuwa mkubwa miongoni mwa wanausalama tuliokuwa pale, nikakichukua kile kikaratasi na kukikunjua.
Nikashituka, macho yangu yalipokutana na maandishi ya wino mwekundu yaliyosomeka.
Chini ya maandishi hayo palikuwa na alama ya dole gumba kisha kulikuwa na sahihi.
Mwandiko ulikuwa ni kama ule uliokuwa kwenye kipande cha karatasi tulichokikuta kwenye shingo ya maiti ya Lazaro. Kadhalika sahihi yake ilikuwa ile ile.
Hapo sikupata shaka yoyote kwamba Frank alikuwa amenyongwa na aliyemnyonga yeye ndiye aliyemnyonga Lazaro.
Pia sikupata shaka yoyote kwamba Frank alikuwa mmoja wa watu walioandikwa katika kipande cha karatasi cha kwanza kilichoandikwa BADO WATATU.
Na ndio maana baada ya Frank kufa kipande cha karatasi alichokutwa nacho kimeandikwa BADO WAWILI. Utaona kwamba Frank alikuwa amepunguza hesabu ya watu watatu.
Hapo hapo nikajiuliza yuko wapi huyu mtu anayeua hawa watu na anawaua kwa sababu gani?
Pia nikajiuliza hao watu wawili ambao wamebaki ni kina nani na watauawa lini?
Kusema kweli nilijisikia vibaya kuona nilishindwa kuzuia vifo vya watu hao walionyongwa na pia nikajiambia nitasikia vibaya sana kama watu hao wawili ambao hata hivyo sikujua walikuwa kina nani, nao watanyongwa.
Niliwaonyesha kile kipande cha karatasi polisi wenzangu pamoja na yule shahidi wetu ambaye aliniambia anaitwa Elias.
“Hao ‘wawili’ ni kina nani?” Elias akauliza baada ya kukisoma kikaratasi hicho.
“Hatujawafahamu bado,” nikamjibu na kuongeza;
“Kama tungewafahamu tungechukua hatua za kuokoa maisha yao.”
Nikamuona Elias amepata shaka kama vile alihisi na yeye yumo.
“Hawa watu wanaouawa wanajuana. Huyu aliyenyongwa leo alikuwa anafahamiana na mtu aliyenyongwa juzi. Inaonekana kwamba kuna walengwa maalum lakini tutaendelea na uchunguzi ili tupate sababu na kiini cha mauaji haya.”
“Nilikuwa nimepatwa na wasiwasi juu ya hatima yetu.”
“Tunaamini kwamba kuna walengwa maalum, si kila mtu.”
Wakati nazungumza na Elias, polisi walikuwa wakiupiga picha ule mwili wa Frank.
Baada ya kuupiga picha mwiuli huo niliupekua mifukoni nikakuta pochi iliyokuwa na pesa shilingi elfu tisini, funguo nilizohisi kuwa zilikuwa za nyumba pamoja na leseni ya kuendesha iliyokuwa na jina la Athony Hiza Frank.
Vitu hivyo nilivitia mfukoni mwangu nikaagiza polisi wannne waupeleke ule mwili hospitali ya Bombo.
Mimi na polisi tuliobaki tulifanya upekuzi ndani ya ile nyumba. Baada ya upekuzi wetu uliochukua karibu saa moja tulitoka na kufunga mlango. Nilichukua namba ya simu ya Elias na mimi nikampa namba yangu.
“Nitakapokuhitaji nitakupigia ili uje uandikishe maelezo yako kuhusu zoezi zima ulilolishuhudia hapa,” nikamwambia Elias.
Baada ya hapo nikaagana naye na sisi tukaondoka. Kwanza nilikwenda ofisini kwa ofisa upelelezi wa mkoa nikamueleza kuhusu lile tukio. Tayari na yeye allikuwa ameshapata taarifa, akaniambia tukio hilo lilimshangaza hata yeye.
“Hiki kikaratasi tulichokikuta kwenye shingo ya marehemu kinaoyesha kwamba aliyemnyonga mtu huyu ndiye aliyemnyonga yule wa kwanza.”
“Katika kile kikaratasi cha kwanza kulikuwa na maelezo ‘bado watatu’ sasa katika hiki kuna maelezo ‘bado wawili…”
“Ameandika ‘bado wawili’ baada ya kumnyonga huyu wa leo.”
“Uchunguzi wako haukuweza kuwabaini watu hawa wanaokusudiwa hapa?”
“Ninasikitika afande kusema kwamba haitakuwa rahisi kuwabaini katika dakika za mapema lakini nitajitahidi niwagundue hawa watu.”
“Na ni lazima pia utafute sababu za huyu mtu kufanya mauaji haya. Lazima atakuwa na kisasi na hawa watu!”
“Ninahisi itakuwa ni hivyo. Hakuna mtu anayeua watu bure bure. Lakini kitu ambacho kimenitia hofu ni kusikia kwamba mtu aliyeuawa mara ya kwanza alishanyongwa mwaka mmoja uliopita. Kama itakuwa ni hivyo mtu huyu atakuwa ni wa aina gani?”
“Sasa hii ni kazi yako wewe. Wewe ndiye mpelelezi wa kesi hii. Wewe ndiye utakayetuambia sisi kwanini mtu aliyenyongwa mara ya kwanza aonekane alishanyongwa mwaka mmoja uliopita!”
“Acha nikaonane na Ibrahim.”
Nikatoka ofisini mwa afande huyo. Nikajipakia kwenye gari na kuelekea kituo cha polisi cha Chumbageni.
Nilipofika niliacha gari nikaingia ofisini kwa sajin Meja Ibrahim.
“Kuna tukio jingine llililotokea,” nilimwambia Sajin Meja huyo lakini na akaniambia hapo hapo.
“Nimesikia kuna mtu mwingine aliyenyongwa leo?”
“Ndiyo hilo tukio ninalotaka kukwambia.”
Nikakaa kwenye kiti na kukiweka kile kipande cha karatasi juu ya meza.
“Aliyemnyonga mtu wa kwanza ndiye huyo huyo aliyemnyonga huyu wa pili. Tazama kikaratasi hicho.”
“Hiki si ndio kile ulichoniletea juzi?” Sajin Meja Ibrahim aliniuliza huku akikishika kikaratasi hicho.
“Hapana. Hicho ni cha leo. Tulikikuta kwenye maiti ya leo.”
Sajin Meja Ibrahim alikisoma na kugutuka.
“Aliyekiandika hiki ndiye yule yule aliyekiandika kile cha kwanza.”
“Nataka uichunguze hiyo alama ya dole kama inafanana na ile ya kwanza.”
“Utanipa muda wa kama saa moja hivi.”
“Halafu kuna kitu kingine nataka nikueleze.”
“Nitakapokuja tena nataka twende hospitali ukachukue alama za marehemu niziweke katika kumbukumbu zangu.”
“Ninaweza kukupa msaidizi wangu uende naye.”
“Basi ni vizuri niende naye hivi sasa.”
Sajin Meja Ibrahim aliinuka kwenye kiti akatoka mle ofisini. Baada ya muda kidogo alirudi akiwa amefuatana na polisi mmoja aliyekuwa amevaa kiraia ambaye alikuwa ameshika kifaa cha kuchukulia alama za vidole.
“Utakwenda na afande hospitalini ukachukue alama za vidole za marehemu,” Ibrahim alimwambia polisi huyo.
“Sawa. Twenzetu afande” Polisi huyo akaniambia.
Nikainuka kwenye kiti na kutoka na polisi huyo. Tulijipakia kwenye gari na kuelekea hospitali ya Bombo.
Tulipofika tulikwenda katika chumba cha maiti ambako tulitolewa maiti ya Frank. Polisi huyo akachukua alama za vidole za maiti ya Frank kisha tukatoka.
Tuliporudi kituoni nilimuacha polisi huyo nikaenda ofisini kwangu ambako nilifungua faili jingine la uchunguzi ya mauaji ya Frank ambalo niliweka maelezo yangu. Yakabaki maelezo ya wale polisi wengine pamoja na ya shahidi wetu ambaye alikuwa ni Frank.
Wakati nalifunga faili hilo Ibrahim akanipigia simu.
“Afande uko wapi?” akaniuliza.
“Niko ofisini kwangu.”
“Nije huko au utakuja wewe?”
“Ni vizuri mimi nije huko.”
“Sawa. Njoo sasa hivi. Nakusubiri.”
Nikainuka na kutoka. Dakika chache tu baadaye nikausukuma mlango wa ofisi ya Ibrahim na kuingia.
Inaendelea…