Dodoma. Kunje Ngombale wa AAFP ni kama hakuamini lakini ikawa kweli.
Kunje ni mgombea kiti cha Rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambaye amefika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), jijini Dar es Salaam kukamilisha taratibu za uteuzi.
Amefika akiwa kwenye msafara wa magari mawili akiwa na mgombea mwenza wake, Chumu Abdallah Juma na Katibu Mkuu wa chama hicho, Rashid Rai na moja kwa moja aliingia ndani ya ukumbi.

Wakati anatoka ndani ya ukumbi, gari zake mbili zilisogea karibu na eneo la lango kuu kwa lengo la kumsubiri mgombea wao.
Hata hivyo, alikuja mmoja wa watumishi na kuwataka madereva hao waondoe magari yao kitendo kilichochukua dakika kadhaa wakihoji kwa nini watoke hadi ofisa mwingine alipowafuata na kuwapa ufafanuzi.
Mara mgombea alipotoka nje, alikuta mbele yake kuna gari jipya na akataka kulipita kuelekea mahali yalipoegeshwa magari waliyokuja nayo.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima amemweleza mgombea kuwa Serikali inamkabidhi gari na mlinzi kwa ajili ya matumizi ya kampeni.
Kunje amemtazama Katibu Mkuu, Rai na mgombea mwenza, Chumu Abdallah Juma kisha akatabasamu na kutaka kufungua mlango, akaelezwa kuwa mlinzi atafanya kazi hiyo.
Baada ya hapo amefunguliwa mlango akaingia kwenye gari na kufungwa mkanda kisha wakaondoka.
Kampeni za uchaguzi mkuu zinaanza kesho Alhamisi, Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025. Jumatano ya Oktoba 29, 2025 itakuwa siku ya upigaji kura.