Msafara wa mtiania wa urais wa Chama cha ACT –Wazalendo, Luhaga Mpina amezuiwa kuingia ndani ya jengo la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma.
Msafara huo ulifika saa 6 mchana ya leo Jumatano, Agosti 27, 2025 ambapo askari kanzu na waliovalia sare wamelifunga geti la ofisi hizo ili asiingie.
Jana Jumanne, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima alimwandikia barua Katibu Mkuu wa chama hicho ikieleza kwamba tume hiyo barua yake ya awali ya Agosti 15, 2025 yenye kumbukumbu namba (Kumb. Na. CBA.75/162/01A/229) iliyohusu urejeshaji wa fomu za uteuzi wa Mpina na kueleza kuwa hatapaswa kufika katika ofisi za Tume kwa ajili ya uteuzi uliopangwa kufanyika leo Jumatano, Agosti 27, 2025.
Barua hiyo imeeleza uamuzi huo umechukuliwa baada ya taarifa kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyobatilisha mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Agosti 6, 2025, ambao ulimteua Mpina kuwa mgombea urais.
Barua hiyo ya INEC, iliyoanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, imeeleza;
“Napenda kukujulisha kwamba, tumepokea nakala ya barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ikieleza amebatilisha uamuzi wa Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo kwa sababu ya mgombea kukosa sifa za kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.”
Vilevile, imetoa wito kwa ACT-Wazalendo kuteua mgombea mwingine mwenye sifa stahiki ili mchakato wa uteuzi uweze kuendelea kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi. Aidha, ulimtaka mgombea huyo asifike ofisi hizo za INEC.