MSHAMBULIAJI na nahodha wa Timu ya taifa ya Wanawake, Twiga Stars Opah Clement ametambulishwa kwenye kikosi cha SD Eibar inayoshiriki Ligi Kuu Hispania maarufu Liga F.
Ametambulishwa kikosini hapo akitokea FC Juarez ya Mexico aliyoitumikia kwa msimu mmoja akicheza mechi sita kati bila ya kufunga bao wala asisti.
Nyota huyo wa kimaaifa wa Tanzania anakuwa mchezaji wa kwanza kujiunga na timu inayoshiriki ligi hiyo ambayo inashika nafasi yapili kwa ubora barani Ulaya.
Eibar ambayo msimu uliopita ilimaliza nafasi ya saba katika ligi ya Hispania inamsajili Opa kwa ajili ya kuboresha safu yao ya ushambuliaji ambayo msimu uliopita haikufanya vizuri kwani ilikuwa miongoni mwa timu zilizofunga mabao machache.
Kabla ya kutua kikosi hicho, Opa ambaye alianza safari yake ya kucheza soka nje ya mipaka ya Tanzania kupitia KayseriSpor ya Uturuki, amewahi kupita pia Beskitas, Henan Jianye(China) na Juarez(Mexico).
Amesaini mkataba wa mwaka mmoja na timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1991 kama Eibartarrak FT kabla ya baadae kubadilishwa na kuitwa rasmi Eibar.