Mikakati ya kupunguza utegemezi wa kuni kwa wakimbizi Kigoma yaanza kutekelezwa

Kigoma. Mkoani Kigoma, ambapo maelfu ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi wamepatiwa hifadhi, changamoto kubwa imekuwa utegemezi wa kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.

Hali hiyo inasababisha uharibifu mkubwa wa misitu na kuongeza hatari za kiusalama kwa wanawake na watoto wanaolazimika kutembea umbali mrefu kutafuta kuni.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), kufikia Julai 2025, Tanzania ilikuwa na wakimbizi 190,809, wengi wao wakiwa wamehifadhiwa kwenye kambi za Nyarugusu na Nduta.

Wingi wa watu hao umesababisha mahitaji makubwa ya nishati ya kupikia, huku kuni zikitumika kama chanzo kikuu.

Utafiti wa mwaka 2017 wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shirika la Denmark Technical University (DTU) ulibaini kuwa asilimia 85 ya wakimbizi Kusini mwa Jangwa la Sahara hawamudu gharama za nishati safi.

Katika kambi ya Nyarugusu iliyopo Kigoma, wakimbizi hutumia wastani wa saa 19 kwa wiki kutafuta kuni na zaidi ya saa sita kwa siku kupika.

“Kutumia gesi au umeme kungepunguza muda huo hadi saa mbili pekee, jambo ambalo lingeongeza tija na kupunguza hatari za kiafya na usalama,” inaeleza utafiti huo.

Ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, UNHCR, kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali, imeanzisha kampeni za elimu na usambazaji wa teknolojia rafiki wa mazingira.

Ofisa Mazingira wa UNHCR Kigoma, Godfrey Mchunguzi, anasema zaidi ya majiko banifu 2,000 yamegawanywa, 1,400 kwa wakimbizi na 600 kwa wakazi wa vijiji jirani.

“Majiko haya yanatumia kuni chache, na kuni moja inaweza kuiva chakula kizima. Hii inapunguza gharama kwa familia na inalinda misitu,” anasema.

Aidha, shirika hilo limeweka mifumo ya nishati ya jua kwa ajili ya majiko ya umeme (Electric Pressure Cooker) kwenye hospitali na vituo vya afya ndani ya kambi.

Kwenye kambi ya Nyarugusu, mifumo hiyo inatumika kupikia maharage kwenye hospitali kuu na vituo vya afya, hatua inayopunguza utegemezi wa kuni na gesi.

Serikali, kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), inalenga kuhakikisha angalau asilimia 80 ya kaya zinatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Kigoma ni miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele kutokana na wingi wa wakimbizi na changamoto za uharibifu wa mazingira.

Mei 2025, UNHCR, UNEP na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) walizindua mradi wa miaka mitano wenye thamani ya Dola milioni 19 (takribani Sh50 bilioni) kwa ajili ya kujenga ustahimilivu wa tabianchi Kigoma.

Sehemu ya mradi huo inalenga kuimarisha upatikanaji wa nishati safi na kuelimisha jamii kuhusu majiko banifu na mkaa mbadala.

Hata hivyo, jitihada hizi bado zinakabiliwa na changamoto ya ufadhili wa kudumu. Baadhi ya miradi inakoma kutokana na kusuasua kwa wafadhili, jambo linalohatarisha uthabiti wa mipango ya muda mrefu.

Wadau wanasema kuna haja ya Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kushirikiana zaidi ili kuongeza uwekezaji katika miradi ya nishati safi.

Kwa kufanya hivyo, jamii za wakimbizi na wenyeji wa Kigoma zitaweza kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kulinda misitu na kuboresha usalama wa wanawake na watoto wanaobeba mzigo mkubwa wa kuchoma na kutafuta nishati ya kupikia.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.