Dk Biteko aumizwa na wenyeviti wa bodi na watendaji wanaosigana

Arusha. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameeleza namna anavyoumizwa na wenyeviti wa bodi, watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kutoka taasisi moja kuvutana, badala ya kufanya kazi kwa umoja, upendo na kutanguliza masilahi ya Taifa mbele.

Amesema watendaji hao wanapaswa kutambua Watanzania zaidi ya milioni 60 wanawategemea hivyo wana wajibu wa kusimamia taasisi na mashirika yao vizuri, ili kuondoa umaskini kwa wananchi kwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Dk Biteko ameyasema hayo jana Jumanne Agosti 26, 2025 jijini Arusha alipokuwa akifunga kikao kazi cha tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma nchini (CEO’s forum 2025).

Amesema kiongozi bora hapimwi kwa maneno na mipango bali hupimwa kwa vitendo na matokeo, hivyo wanapaswa kuwa na umoja kwani utengano ni udhaifu.

“Muendelee kusimamia taasisi zenu, hakuna jambo linaniuma kwa kweli na hili naomba nilizungumze polepole. Unakuta eti mtendaji wa taasisi na Mwenyekiti wake wanavutana kwa jambo gani, wote mko pale kwa ajili ya kukuza taasisi yenu, niwaombe mkafanye kazi kwa upendo katika taasisi zenu,” amesema.

Dk Biteko amesema watendaji hao wana dhamana kubwa ya kuhakikisha wanaongeza ufanisi na kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi wote, ikiwemo kuacha kuvutana na badala yake wafanye kazi kwa kushirikiana ili kuwatumikia Watanzania.

“Sisi Watanzania milioni 60 tunalitegemea kundi hili kubadilishia maisha yetu kupitia kazi zenu, kama tunazungumza umaskini wa watu, Serikali anapaswa kuwa kiongozi wa kwanza kuondolea watu umaskini kwa kutumia taasisi na mashirika yake kwa kutoa huduma bora na kukuza uchumi,” amesema.

“Mkaseme kidogo mtende zaidi tumewekwa kwenye makundi mbalimbali wako wengi wanaosema acheni waseme ninyi fanyeni kazi. Muendelee kusimamia taasisi na mashirika,” amesema.

Dk Biteko amezitaka taasisi na mashirika hayo kuwa mabalozi kwa sekta binafsi kwani kuna baadhi ya taasisi na mashirika hayo yanalipiwa na Serikali hadi mishahara, ila kuna taasisi za sekta binafsi zinazofanya vizuri.

“Mmepiga hatua, mimi nafahamu mabadiliko mahali popote huwa yana tabia ya kupingwa, ukileta jambo jipya kwenye jamii yoyote badala ya watu kushughulika nalo watashughulika na mtu ili wakae kwenye hali waliyozoea, endeleeni na mabadiliko mliyoanza,” amesema.

Amesema katika maelekezo ya kila taasisi kuboresha utendaji na kuongeza uchangiaji wa mfuko mkuu, kwa kipindi cha mwaka 2024 taasisi mbalimbali zimeongeza michango yao katika mfuko huo.

“Taasisi ya TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania) ilikuwa na ongezeko la uchangiaji la asilimia 100 kutoka kuchangia Sh5.5 bilioni kwa mwaka 2023/24 hadi Sh11.1 bilioni kwa mwaka 2024/25. Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ikiwa na ongezeko la uchangiaji la asilimia 363 kutoka kuchangia Sh1.2 bilioni mwaka huo hadi kufikia Sh5.5 bilioni,” amesema.

Awali, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Stansalus  Nyongo amesema kikao hicho cha siku nne kimeshirikisha washiriki zaidi ya 650 na wamejadiliana masuala mbalimbali ya kuendesha taasisi hizo.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia mageuzi hayo kwa karibu kuhakikisha taasisi na mashirika ya umma nchini yanachangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa, sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ambayo inalenga kufikia uchumi wa kati na wa juu.