Upelelezi bado shauri la wizi Benki ya Equity

Dar es Salaam. Washtakiwa 11 wanaokabiliwa na mashtaka 20, yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni kwa udanganyifu mali ya Benki ya Equity Tanzania Limited, wataendelea kusalia rumande hadi Septemba 9, 2025 kesi itakapotajwa.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa shauri hilo la uhujumu uchumi kutokamilika, huku mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa pamoja washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 18447 ya mwaka 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa hao ni Jasmine Elphas, aliyekuwa ofisa wa benki hiyo makao makuu na mfanyabiashara Fredrick Ogenga. Wengine ni Caroline Masayanyika na Lilian Koka, waliokuwa maofisa wa benki hiyo makao makuu.

Wamo pia Halifa Maina, Kaizilege Mohamed, Daudi Fata, Mrisho Mrisho, Neema Paul, Claude Beda na Jefferson Ogenga, ambao wote ni wafanyabiashara.

Leo Jumatano, Agosti 27, 2025 Wakili wa Serikali Mwandamizi, Neema Moshi ameieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika.

Neema ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Kutokana na upelelezi kutokukamilika, Kiswaga aliahirisha kesi hadi Septemba 9, 2025 itakapotajwa. Kesi hiyo imeahirishwa kwa njia ya video, washtakiwa wakiwa rumande.

Katika hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kati ya Agosti 30, 2024 na Juni 28, 2025 katika maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam, waliongoza genge la uharifu na kujipatia Sh5.7 bilioni mali ya Benki ya Equity Tanzania Limited.

Katika tarehe hizo, Jasmine na Ogenga, wakiwa ndani ya makao makuu ya Benki ya Equity iliyopo Ilala, wanadaiwa kuiba Sh3.6 bilioni zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika akaunti ya Clearing and Settlement mali ya Benki ya Equity.

Caroline anadaiwa katika tarehe hizo, akiwa makao makuu ya benki, aliiba Sh728 milioni mali ya benki hiyo.

Lilian anadaiwa kati ya Februari 28 na Aprili 2, 2025 makao makuu ya benki hiyo, aliiba Sh26 milioni. Vilevile, kati ya Januari mosi na Aprili 24, 2025 katika benki hiyo, Maina anadaiwa kuiba Sh101 milioni mali ya benki.

Inadaiwa kati ya Januari 22 na Aprili 24, 2025 katika ofisi hizo, Mohamed aliiba Sh57 milioni, huku Fata akidaiwa kuiba Sh758 milioni, tukio analodaiwa kutenda kati ya Novemba 2, 2024 na Mei 25, 2025.

Mahakama ilieleza kati ya Januari 9 na Mei 25, 2025, makao makuu ya benki hiyo, Mrisho aliiba Sh211 milioni, mali ya benki.

Upande wa mashtaka ulidai kati ya Januari 9 na Mei 28, 2025, makao makuu ya benki hiyo, Neema aliiba Sh32 milioni mali ya benki, huku siku na eneo hilo, Beda akidaiwa kuiba Sh108 milioni.

Mbali ya hayo, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 10 ya utakatishaji wa fedha walizodaiwa kuiba.