Siri ufunguzi wa Soko la Kariakoo kupigwa danadana

Dar es Salaam. Imekuwa ni  ahadi hewa  ya kufunguliwa soko la Kariakoo, lililokuwa katika ukarabati kwa miaka mitatu tangu lilipoungua na kuteketeza mali zote za wafanyabiashara.

Soko hilo lililoungua mwaka 2021 ili kulijenga upya, Serikali ilitoa Sh28 bilioni kwa ajili ya  ujenzi huo .

Katika kipindi chote hicho wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao sokoni hapo, walihamishiwa katika masoko ya Kisutu, Karume na Machinga Complex ili kupisha ujenzi huo. 

Pamoja na watendaji kueleza hadi sasa soko limekamilika kwa asilimia 98  tayari  maeneo yote yameshakodishwa kwa ajili ya  kuanza tena biashara, lakini ahadi ya kulifungua imebaki kitendawili licha ya viongozi kusema litafunguliwa siku fulani na ikifika hamna kinachofanyika.

Agosti 25, 2025  katika mahojiano na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, AlbertChalamila ambaye ndio msimamizi mkuu,  Mwananchi ilitaka kujua sababu ya danadana hizo za tarehe, licha ya kiu walionao wafanyabiashara na wananchi wa Dar es Salaam kurejea tena kwa soko hilo.

Chalamila amesema mkandarasi aliyekuwa akijenga soko hilo kuna kiasi chake cha hela alikuwa hajamaliziwa, lakini zimepita kama wiki mbili wameshamalizana naye na wakati wowote kuanzia sasa atawakabidhi.

 “Ni kweli kila wakati tumekuwa tukitaja tarehe ya kulifungua lakini haifanyiki, hii ni kutokana na mkandarasi alikuwa bado hajatukabidhi soko rasmi kutokana na deni alilokuwa anatudai, lakini sasa tunashukuru tumemalizana naye na atatukabidhi muda wowote kuanzia sasa,” amesema Chalamila ambaye hakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha walichokuwa  wanadaiwa.

Pia, amesema baada ya kukamilika hilo, lengo ni soko hilo lifunguliwe kabla ya Septemba 15,2025 na kueleza wafanyabiashara tayari wameshaonesha maeneo  yao wakiwamo wale waliopata maeneo ya kukodi  kwa njia ya mnada wa mtandaoni.

Kuhusu malalamiko kwa wafanyabiashara waliokosa maeneo, Chalamila amesema waliowahakiki ndio wamekidhi vigezo.

Amesema asilimia 85 wanarejea kati ya wale waliokuwepo, hivyo kutokana na utaratibu mpya wa kuliendesha soko hilo, baadhi kwa uhalisia wanajikuta wanakosa sifa za kuwepo sokoni hapo.

“Uendeshaji wa soko kwa sasa ni tofauti na utakavyokuwa awali, huko nyuma ilikuwa mtu mmoja anaweza kuwa anamiliki maduka hata kumi, lakini hawa wote tumeshughulika nao, anapewa duka moja tu. Lakini  gharama za kukodi maduka zimepanda, hivyo ambaye hana uwezo lazima ajikute yupo nje,” amesema Chalamila.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuna maduka ya sokoni hapo, wafanyabiashara wameingia mkataba wa hadi Sh40 milioni kwa mwaka, fedha ambayo mfanyabiashara wa kawaida hawezi kuimudu.

Chalamila amesema kwa kuwa soko lina uwezo wa kuchukua watu 1500 sio kila mtu ataweza kupata na kutaka waliokosa kutafuta maeneo mengine kwa kuwa Kariakoo kila siku majengo yanajengwa yakiwamo ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) yaliyokuwa makazi ya watu na sasa yamebadilishwa kuwa ya biashara.

Pia, katika kituo cha biashara kilichopo Ubungo amesema nafasi bado zipo, hivyo wananchi wachangamkie fursa kwenda kupachukua na kufanya biashara zao huku akiwataka kwenye biashara wasiogope kuingia gharama ikiwamo ya ukodishaji maduka.

Katika mikakati hiyo, amesema wanasisitiza ujengwaji wa majengo makubwa ya biashara pembezoni mwa mji, kwa kuwa haitasaidia tu watu kupata maeneo bali itarahisisha wananchi kupata huduma badala ya wote kwenda Kariakoo.

 Chalamila amesema kwa Kariakoo pekee mpaka sasa kuna jumla ya maduka 3000 yakiwamo 400 ambayo yanajengwa katika jengo la DDC yanayomilikiwa na halmashauri, watu binafasi, taasisi na kampuni mbalimbali.

Kwa mara ya kwanza kutolewa kwa ahadi ya kulifungua soko hilo ilikuwa Aprili 2024;  uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo ambao ndio waendeshaji wa soko hilo, ulijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kusema, ujenzi wake umefikia asilimia 98 na kueleza lingeanza kazi rasmi mwezi mmoja baadaye (yaani Mei 2024).

Pia, katika mkutano huo, uongozi huo ulitoa utaratibu wa namna wafanyabiashara waliokuwepo hapo watakavyorejea na wengine wapya watakavyoingia na siku chache baadaye shirika hilo lilitoa majina ya watu waliopitishwa kurejea sokoni hapo, hatua ambayo wafanyabiashara hawakukubaliana nayo kwa kile walichosema wengi walikatwa katika orodha hiyo.

Kwa mujibu wa shirika hilo, soko  lilikuwa na wafanyabiashara zaidi ya 1600 lakini baada ya uhakiki wamebaini wenye sifa ya  kurejea ni 819.

Kigezo kikubwa  kilichotumika kuwarudisha wafanyabiashara hao ni kuwa na mkataba wa moja kwa moja wa shirika,  jambo lililopingwa na wafanyabiashara hao na kueleza, wengi walikuwa wapangaji japo wana risiti zote za kufanya malipo kwa shirika.

 Julai 5,2024,  Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Masoko Kariakoo, Hawa Ghasia alipofanya ziara sokoni hapo  kujionea maendeleo ya ujenzi wake ulipofikia, alisema namna walivyoona na kujidhihirisha, wafanyabiashara watarudishwa rasmi Agosti.

Hata hivyo, katika ziara hiyo, mwenyekiti huyo aliagiza ambao hawajajiona majina yao kwenda kusikilizwa, shughuli iliyofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja na kuvurugika katikati baada ya wengi kutoridhishwa.

Hali hiyo pia ilisababisha wafanyabiashara hao kufanya maandamano hadi  ofisi ndogo za Chama cha Mapinduzi (CCM) zilizopo  Mtaa wa Lumumba, kisha walikutana na Chalamila kumuelezea malalamiko yao.

Baada ya kuridhishwa na baadhi ya hoja, mkuu huyo wa mkoa aliagiza kushushwa mtandaoni kwa majina yote yaliyopitishwa  na kuahidi yatarejeshwa baada ya vyombo vya usalama na ofisi yake  kuyafanyia kazi  ili kujidhihirisha kupitishwa kwake.

Septemba 4, 2024 kamati hiyo iliyoundwa na mkuu huyo ilimkabidhi ripoti yake, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Arnatoglo.

Akipokea ripoti hiyo, Chalamila alisema alilazimika kuunda kamati hiyo ili kujiridhisha juu ya mchakato uliotumika kupata orodha ya majina ya awali ya wafanyabiashara hao.

Hatua hiyo, imechochewa na kile alichoeleza, unyeti wa eneo la soko la Kariakoo kwa masilahi ya Jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa jumla.

Januari 2025 Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Masoko Kariakoo, Hawa Ghasia alisema soko lingefunguliwa Februari 2025, baada ya kukamilisha kuwapanga wafanyabiashara .

Aprili 4, 2025, Ghasia wakati akimkabidhi meneja mpya wa shirika, Ashraph Yusufu Abdulkarim, ofisi aliahidi kuwa soko hilo lingefunguliwa ndani ya mwezi huo (Aprili) lakini haikuwa hivyo.

Kauli ya mwisho ya kufunguliwa kwa soko hilo ilitolewa tena Mei 28,2025 na Chalamila alipokuwa akizungumza kuhusu maendeleo ya soko hilo.

Alisema tayari soko limeshakamilika kwa  asilimia 98 na kinachofuata ni maandalizi ya kulifungua japo hakuweka wazi tarehe rasmi.

Katika mkutano huo pia aliagizwa kuondolewa kwa wamachinga waliopo barabara za kuingia sokoni hapo  ili kuziwacha barabara hizo wazi kuruhusu magari yanayoingia kushusha na kuchukua mizigo kirahisi jambo linaloonekana kutotekelezwa kwa kuwa, wafanyabiashara hao bado wapo hadi sasa.