Watumishi Mkinga waonywa lugha chafu wanapotoa huduma

Mkinga. Watumishi wa Serikali wilayani Mkinga, mkoani Tanga, wameonywa kuepuka matumizi ya lugha za matusi au dharau wanapotoa huduma kwa wananchi, kwani tabia hiyo inaweza kuathiri utoaji wa huduma bora katika ofisi za umma.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Omari Mashaka, wakati wa mafunzo elekezi kwa watumishi wa halmashauri hiyo yaliyofanyika jana Agosti 26, 2025.

Mashaka amesema ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kuwa mkweli, mwadilifu na mwenye nidhamu ya kazi muda wote.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Omari Mashaka akiongea na watumishi wa ofisi hiyo kwenye mafunzo maalum.Picha na Rajabu Athumani

Aidha, aliwasisitiza watumishi kushughulikia changamoto wanazokumbana nazo kwa kuwasiliana na viongozi wao wa ngazi za juu, badala ya kutoa huduma kwa hasira au lugha isiyofaa.

Mashaka amesema mafunzo hayo elekezi yamelenga kuwajengea uwezo watumishi wapya pamoja na walioajiriwa awali katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, kwa lengo la kuwaimarisha katika maeneo ya maadili ya kazi, uwajibikaji, utoaji wa huduma bora, pamoja na utendaji kazi kwa kuzingatia miongozo na taratibu za Serikali.

Ameeleza kuwa si jambo jema kwa mwananchi anapokwenda kupata huduma katika idara mbalimbali kama afya, elimu na nyinginezo, kukumbana na lugha mbaya au kauli zisizofaa kutoka kwa mtumishi ambaye anapaswa kumsaidia.

Mashaka amesisitiza kuwa hali hiyo huathiri kwa kiasi kikubwa imani ya wananchi kwa taasisi za umma na inapaswa kukemewa.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga imepokea watumishi wapya 65, ambapo Serikali imelenga kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia miongozo ya utumishi wa umma.

“Zingatieni maadili ya watumishi wa umma na mtambue kuwa nyie ni sehemu ya jamii, hivyo mnatakiwa kushirikiana nao kwa kutoa huduma kwa uadilifu na uaminifu mkubwa, msitoe lugha za matusi au kashfa kwa wananchi, hayo ni makosa na miongozo yetu hairuhusu mnakuwa mfano wa nidhamu, mshikamano na kufanya kazi kwa kushirikiana.

“Serikali inatarajia kuona matokeo chanya kupitia ninyi.” amesema Mashaka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Jane Isarara amewataka watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wakiwa kwenye mafunzo maalum ya maadili ya kazi.Picha na Rajabu Athumani.

Ameonya kuwa mtumishi yeyote atakayekiuka maadili hayo atachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi.

Isarara amefafanua kuwa kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma zinahusisha bidii kazini, utoaji wa huduma bora bila upendeleo, matumizi sahihi ya taarifa, kuepuka vitendo vya rushwa, pamoja na kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoweza kusababisha migongano kazini au kuvuruga taswira ya taasisi.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wenzake, Andrea Amaniel amesema wamepokea mafunzo hayo kwa mikono miwili na wamejipanga kuyatumia katika utendaji wao wa kila siku.