Mwendokasi Mbagala kufanya kazi sambamba na daladala

Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku nne kabla ya kuanza rasmi kwa huduma ya mabasi yaendayo haraka (BRT) barabara ya Mbagala, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) imesema daladala zinazotoa huduma katika barabara hiyo zitaendelea kufanya safari zake kama kawaida.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Agosti 27, 2025, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Johansen Kahatano amesema tofauti na ilivyokuwa katika mradi wa awamu ya kwanza uliokuwa ukitumia Barabara ya Morogoro kutoka Kimara, safari hii daladala hazitaondolewa kwa wakati mmoja.

Ikumbukwe kuwa, wakati mradi wa kwanza ulipoanza, daladala zaidi ya 8,000 ziliondolewa barabarani ili kupisha mwendokasi.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dk Athuman Kihamia, huduma ya mwendokasi barabara ya Mbagala inatarajiwa kuanza Septemba Mosi mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya awamu ya pili ya mradi huo.

Kahatano amesema hatua ya kutoondoa daladala zote kwa mara moja, inalenga kuhakikisha huduma ya usafiri haikatiki.

“Safari hii hatutaziondoa daladala zote kwa wakati mmoja kama ilivyokuwa kwa njia ya Kimara, bali tutaendelea kupunguza taratibu kadiri idadi ya mabasi ya mwendokasi itakavyokuwa ikiongezeka barabarani,” amesema.

Hadi sasa, mabasi 99 kati ya 255 yanayotarajiwa kuanza kutoa huduma katika barabara ya Mbagala, yamewasili nchini kupitia kampuni ya Mofat ambayo ilishinda zabuni ya kuleta mabasi hayo. Taratibu za kuyatoa bandarini zikiwamo za kikodi zinaendelea.

Kwa mujibu wa mpango wa DART, awamu ya pili ya mradi wa BRT inatarajiwa kutumia jumla ya mabasi 755, ambayo yataingizwa kwa awamu.

Wananchi na wadau wa usafirishaji wamekuwa wakiomba daladala zisiondolewe haraka, wakihofia matatizo ya usafiri kutokana na wingi wa abiria wanaotumia barabara ya Mbagala. “Tunaiomba Serikali wasiondoe daladala mapema, kwa sababu Mbagala ni eneo lenye watu wengi, wasubiri kwanza kuhakikisha mabasi ya mwendokasi yanatosha,” amesema Hussein Kiza, mkazi wa Mbagala.

Mmoja wa madereva wa daladala, aliyejitambulisha kwa jina moja la Clemence, amesema alikuwa na wasiwasi baada ya kusikia mabasi hayo yataanza kazi, lakini amefarijika kuona kibali chake cha kufanya safari kimeongezewa mwaka mmoja zaidi.

Kwa upande mwingine, Latra imeendelea kuruhusu taratibu kurudi kwa baadhi ya daladala kwenye barabara ya Morogoro ili kupunguza changamoto za usafiri. Hadi sasa, bado kuna daladala zinazofanya safari zake kati ya Mbezi–Mwananyamala na Mbezi–Mnazi Mmoja.

Historia ya mradi wa mwendokasi inaonesha kuwa awamu ya kwanza iliyopaswa kuwa na mabasi 305, ilianza na mabasi 140 pekee mwaka 2016.

Baadaye yaliongezwa mengine 70 mwaka 2021, na kufikisha jumla ya mabasi 210, lakini yanayotoa huduma kwa sasa hayazidi 60 kutokana na uchakavu. Hali hiyo imechangia abiria kukaa muda mrefu vituoni.

Kabla ya kuanza kwa mradi wa kwanza wamiliki wa daladala walilipwa fidia ya Sh4 milioni kwa kila gari na Sh3 milioni walipokea moja kwa moja na Sh1 milioni ziliingizwa kwenye hisa za kampuni ya UDART, chini ya mwekezaji wa wakati huo, Robert Kisena.

“Wakati ule tulishirikishwa kwa karibu na DART pamoja na mwekezaji, tofauti na sasa ambapo taarifa nyingi tunazisikia mitandaoni au kuzisoma kwenye magazeti kama watu wengine,” amesema Gharib Mohamed aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Mkoa wa Dar es Salaam (Uwadar).