Chunya. Serikali Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya imeonya jamii ya wafugaji kuachana na dhana ya mila potofu kuhusishwa kwenye kampeni ya utoaji wa chanjo ya mifugo.
Hatua hiyo imetajwa kuchangia kukwamisha mikakati ya Serikali na kuzorotesha ustawi wa mifugo na uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na Taifa kwa ujumla.
Katibu Tawala Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Anakret Michombero amesema leo Jumanne Agosti 26, 2025 baada ya kuzindua kampeni ya utoaji wa chanzo ya mifugo na uvalishaji heleni za utambuzi.
Amesema zaidi ya mifugo 170,000 wilayani humo inatarajiwa kuchanjwa huku ng’ombe 200,000 tayari wamevishwa helena za utambuzi, lakini pia asilimia 95 ya kitoweo cha kuku zimechanjwa.
“Kuna imani potofu miongoni mwa jamii kuwa wakichanja mifugo inakufa hiyo ni dhana potofu ya vizazi na vizazi, lakini mnapaswa kutambua chanjo hiyo ni muhimu kwa kulinda mifugo yenu ambayo ni faida kwa baadaye na familia zenu,” amesema.
Michombero amekemea dhana potofu na kuwasihi wafugaji kuchangamkia fursa ya kuchanja mifugo ili kufikia malengo ya Serikali na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu ili kuleta mabadiliko katika sekta ya mifugo nchini.
“Kwa kutambua umuhimu wa chanjo na uvalishaji heleni Serikali imetenga siku maalum kwa ajili ya zoezi hilo ni vyema sasa jamii ya wafugaji maeneo ya pembezoni kufikisha mifugo kwenye maeneo yaliyotengwa,” amesema.
Katika hatua nyingine amewataka wafugaji kuisaidia Serikali kutoa taarifa za siri za baadhi yao kuingia kinyemela bila kufuata utaratibu na miongozo lengo ni kudhibiti uvamizi wa maeneo ya malisho.
“Pia tutazuia mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayotokana na mwingiliano wa mifugo kutoka maeneo mengine nje ya Wilaya ya Chunya,”amesema.
Ofisa Mifugo Wilaya ya Chunya, Dk Benedictor Matogo amewema wameweka mikakati ya kufikia mifugo 170,000 katika kata zote Wilaya ya Chunya baada ya kuzindua zoezi hilo.
Amesema mbali na kutoa chanjo na heleni tutaendelea kutoa elimu kwa wafugaji kutumia mbinu bora za ufugaji. Pia malisho hususani unenepeshaji lengo ni kuleta tija kubwa katika sekta ya mifugo.
“Kimsingi tunamshukuru Serikali kwa hatua hii kubwa, lakini kutufikishia vifaa vinavyo tumika katika kutoa chanjo na uvishani wa heleni kwenye mifugo hususani ng’ombe,” amesema.
Shija Mathias Mkazi wa Kijiji cha Mapula Wilaya ya Mbarali ameshauri Serikali kupitia Wizara ya mifugo kuweka kipaumbele kampeni hiyo kuwafikia jamii ya wafugaji katika maeneo ya pembezoni.
“Tunatambua idadi kubwa ya mifugo ipo pembezoni, lakini pia kuangalia namna ya kudhibiti uingizwaji holela kutoka mikoa mbalimbali nchini,” amesema.