KELELE na tetesi nyingi zilizokuwa zikimuhusisha mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize kutakiwa na timu mbalimbali za ndani na nje ya Afrika, zimezimwa rasmi na klabu hiyo baada ya kutangaza itaendelea kuwa naye, huku sababu ya uongozi kufanya uamuzi huo ukibainika.
Zilitajwa timu mbalimbali kubwa barani Afrika ikiwamo Zamalek ya Misri, Wydad Casablanca (Morocco) na Kaizer Chiefs (Afrika Kusini) kwamba zinaiwinda saini ya Mzize, pia mwisho iliibuka Al Asad ya Qatar iliyokuwa tayari kutoa kiasi cha Sh2 bilioni kukamilisha dili hiyo.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Mzize ambaye bado ana mkataba na klabu hiyo hadi 2027, ataendelea kuutumikia muda huo uliobaki, hivyo haendi popote.
Mtoa taarifa huyo alibainisha kuwa, sababu ya Yanga kufanya hivyo ni kwamba, uongozi umeona hauwezi kuruhusu kuwaachia wachezaji muhimu kwa wakati mmoja, hiyo ni baada ya kumuuza Stephane Aziz KI aliyesajiliwa na Wydad Casablanca.

Hata hivyo, mtoa taarifa huyo alisema licha ya Yanga kusajili wachezaji 11 kipindi hiki cha dirisha kubwa wakiwemo wa eneo la ushambuliaji Offen Chikola, Edmund John, Andy Boyeli na Celestin Ecua, lakini Mzize amebakishwa kwa mkakati maalum kwani msimu uliopita aliibeba zaidi timu kwa kufunga mabao mengi ndani ya Ligi Kuu Bara na kutetea ubingwa.
“Kama mnakumbuka Aziz KI ameuzwa wakati ambao alikuwa ni mchezaji muhimu ndani ya Yanga na msimu wa nyuma akitoka kuwa mfungaji bora,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.
“Mzize licha ya kwamba hakuwa mfungaji bora msimu uliopita, lakini ndiye ameibuka kinara wa ufungaji kwa wachezaji wazawa, sasa unawezaje kuruhusu Aziz KI na Mzize waondoke kwa pamoja.
“Siku zote timu yenye malengo makubwa inapambana kuwabakisha wachezaji wake muhimu kama ikiona haina ulazima wa kuwauza, ndiyo maana baada ya kumuuza Aziz KI, tumemuongezea mkataba Pacome Zouzoua na kumzuia Mzize asiondoke kwani huwezi jua kitakachotokea kwa wachezaji wapya licha ya kwamba huko walipotoka wamefanya vizuri.”

Uamuzi wa Mzize kubaki unaendana na kile kilichoripotiwa na Mwanaspoti kumuhusu kiungo Khalid Aucho ambaye licha ya kuachana na timu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu wa 20254-2025 na kutua Singida Black Stars, lakini huenda dirisha dogo akarudishwa kufuatia viungo waliosajiliwa kuziba pengo lake kudaiwa bado hawajaonesha kitu cha tofauti. Kiungo wa eneo la ukabaji alilokuwa akicheza Aucho, aliyesajiliwa ni Moussa Bala Conte kutoka CS Sfaxien.
Kwa upande wa wachezaji wapya katika eneo la kushambuliaji ni Celestin Ecua aliyetokea Zoman ya Ivory Coast ambapo msimu uliopita alifunga mabao 13 na asisti 12 kwenye Ligi Kuu ya Ivory Coast.
Offen Chikola ambaye ni winga mzawa, ametokea Tabora United na msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Bara alifunga mabao saba na asisti mbili.
Kwa upande wa mshambuliaji Andy Boyeli raia wa DR Congo, ametokea Sekhukhune United ya Afrika Kusini akiwa amefunga mabao sita katika mechi 25 za Ligi Kuu Afrika Kusini msimu uliopita akicheza kwa dakika 1368, huku Edmund John hakufunga.
Takwimu zinaonyesha msimu uliopita, Mzize ndiye mchezaji pekee wa Yanga aliyecheza mechi zote 30 za Ligi Kuu Bara, akihusika katika mabao 20 baada ya kufunga mabao 14 na kuasisti sita. Jumla aliitumikia Yanga kwa dakika 1,877. Nyuma yake alikuwa Mzimbabwe, Prince Dube aliyefunga mabao 13 na asisti nane katika mechi 27 za ligi kwa dakika 1,829.

Kiungo fundi wa boli Pacome Zouzoua, alicheza mechi 26 kati ya 30 akiitumikia klabu hiyo ya Wananchi kwa dakika 1,614, akifunga mabao 12 na kuasisti 10, huku Aziz KI hadi anaondoka akicheza mechi yake ya mwisho Mei 18, 2025, alicheza mechi 25 za ligi kwa dakika 1,676, akifunga mabao tisa na asisti saba.
Mzize aliyepandishwa timu ya wakubwa ya Yanga msimu wa 2022-2023, hadi sasa amecheza Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu akifunga jumla ya mabao 25. Katika msimu wa kwanza alifunga mabao sita na asisti moja, kisha 2023-2024 akafunga mabao sita na asisti saba na 2024-2025 amepachika mabao 14 na asisti sita.
Kukua kwa kiwango hicho katika ufungaji, ndiyo imezifanya klabu nyingi kumuwinda. Mbali na zilizotajwa huko juu, pia Umm Salal ya Qatar iliingiza mkono wake.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka Yanga, Umm Salal ilitoa ofa ya Dola za Marekani 900,000 (Sh2.2 bilioni) pamoja na mshahara wa Dola 20,000 (Sh50 milioni) kwa mwezi kwa mchezaji huyo.
Kwa upande wa Esperance, ilikuwa tayari kutoa ofa ya Dola 1 Milioni (Sh2.6 milioni).

“Mzize ataendelea kubaki ndani ya Yanga kuutumikia mkataba wake wa miaka miwili ambapo ni 2025-2026 na 2026-2027, hivyo haendi popote,” alisema Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe.
Kamwe alisema Mzize aliyetoka kwenye majukumu ya kuichezea Taifa Stars kwenye michuano ya CHAN 2024 akifunga mabao mawili, kwa sasa amepewa mapumziko na akimaliza muda wake ataingia kambini kuendelea na maandalizi ya msimu ujao kuitumikia Yanga.