Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimeingia vitani na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) baada ya mgombea wake wa urais, Luhaga Mpina kuenguliwa katika mchakato wa uchaguzi mkuu, hatua iliyokilazimu chama hicho kwenda mahakamani kupinga uamuzi huo kikidai ni batili na unadumaza misingi ya demokrasia.
Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, pingamizi dhidi ya uteuzi wa mgombea wa urais na makamu wa rais linaweza kuwasilishwa na mgombea mwingine, Msajili wa Vyama vya Siasa au Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Pingamizi kutoka kwa Msajili linapaswa kuhusiana na Sheria ya Gharama za Uchaguzi pekee, na huwasilishwa ndani ya siku 14 tangu uteuzi. Kwa upande wa mgombea mwingine au Mwanasheria Mkuu, pingamizi huwasilishwa kwa Tume si zaidi ya saa 10:00 alasiri ya siku inayofuata baada ya uteuzi.
Baada ya pingamizi kuwasilishwa, Tume inatakiwa kumjulisha mgombea kwa maandishi na kumpa saa 24 ajibu. Baada ya kupitia hoja zote, Tume hutoa uamuzi kwa maandishi ikieleza sababu.
Endapo Tume itakubaliana na pingamizi, jina la mgombea huyo hufutwa kwenye orodha ya wagombea walioteuliwa, hivyo kuondolewa rasmi kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Hatua dhidi ya Mpina imechukuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kumwengua kwenye orodha ya wagombea sambamba na kumzuia kurejesha fomu alizopewa kwa ajili ya kuomba uteuzi. Tume imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, iliyowasilishwa kwake ikibainisha kuwa Mpina hakuteuliwa kihalali ndani ya chama chake, kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na kada wa ACT-Wazalendo, Monalisa Ndala.
Monalisa alilalamika kwamba Mpina aliteuliwa kuwa mgombea kinyume na kanuni zinazotaka kabla ya uteuzi awe ametimiza mwezi mmoja ndani ya chama, baada ya kuhamia kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM).
Jana Jumanne Agosti 26, 2025 INEC ilimwandikia Katika Mkuu wa ACT – Wazalendo kumfahamisha kuhusu kutengua uteuzi wa Mpina wa kugombea urais na kuwa imeifuta barua iliyoitoa kwa mgombea huyo, kuhusu urejeshaji wa fomu za uteuzi, huku ikikishauri chama hicho kuteua mgombea mwingine.
Kwa hatua hiyo, hata mgombea mwenza wake, Fatma Fereji amepoteza nafasi hiyo
Kwa mujibu wa barua ya INEC iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Tume hiyo, Ramadhan Kailima kwenda kwa Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, uamuzi huo umechukuliwa baada ya taarifa ya Msajili iliyobatilisha uamuzi wa mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo uliomteua Mpina kuwania nafasi hiyo.
Zaidi ya hayo, Tume imemzuia Mpina asifike kwenye ofisi zake jijini Dodoma leo Agosti 27 kwa ajili ya uteuzi, uamuzi ambao chama hicho kimeupinga kwa taarifa rasmi na wagombea hao wamefika kwenye ofisi hizo na kuzuiliwa getini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Agosti 27, 2025, Mwanasheria Mkuu wa ACT – Wazalendo, Omar Issa Shaaban amesema tayari chama hicho kimewaelekeza mawakili wake kufungua shauri mahakamani kupinga uamuzi huo.
“Tumeshaelekeza kufunguliwa kwa kesi mahakamani, tunataka Mahakama itoe tafsiri ya uamuzi wa INEC na amri juu ya maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa,” amesema Shaaban.
Amesema kinachowaumiza zaidi, ni kuwa INEC ikiwa chombo huru, inakuwaje inapokea maagizo ya taasisi nyingine ya Serikali na kuyatolea uamuzi bila ya chama hicho kusikilizwa, hatua aliyodai inabagaza demokrasia.
Shaaban amesisitiza kuwa ACT-Wazalendo haina mpango wa kuteua mgombea mwingine wa urais zaidi ya Mpina na kwamba, wanaamini uamuzi wa INEC ni batili na unakwenda kinyume cha Katiba na sheria na kanuni.
“Mgombea wetu ataendelea na mchakato wa kurudisha fomu kama Katiba inavyoelekeza. Tunaamini amri ya juu ni ya Mahakama na itaenziwa na kuheshimiwa na mamlaka zote,” ameongeza.
Chama hicho kimedai kuwa kitendo cha INEC ni kama “kituko cha mwaka,” kikidai kuwa Tume hiyo ilitumia barua ya Msajili kama msingi wa kumzuia Mpina kurejesha fomu, licha ya Msajili kutokutoa tamko la moja kwa moja la kutengua uteuzi wa mgombea huyo.
“Hakuna kifungu cha Katiba kinachoipatia INEC mamlaka ya kumpokonya mgombea haki ya kurejesha fomu. Ni mara ya kwanza tunaona jambo kama hili duniani,” amedai Shaaban.
Mwanasheria huyo, amehoji sababu ya INEC kutokuweka utaratibu wa kupokea au kusikiliza pingamizi kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, badala ya kuchukua hatua kwa barua ambayo si rasmi katika muktadha wa kisheria.
“INEC imeamua kutekeleza maagizo kutoka kwa barua ya Msajili bila hata kusikiliza upande wetu. Huu ni ukiukwaji wa haki wa hali ya juu,” amesisitiza.
Hata hivyo waandishi walivyotaka kupata ufafanuzi wa INEC, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima amesema leo wanapokea fomu za uteuzi na siyo siku ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Uamuzi huo umeibua hisia tofauti za wachambuzi wa siasa wakisema kilichotokea kinaibua maswali na mafunzo muhimu.
Akizungumzia hilo, Dk George Kahangwa, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ameeleza wasiwasi kuhusu kasi ya mchakato wa hatua hizo, akisema haukutoa nafasi ya pingamizi za wazi kabla ya utekelezaji.
“Mambo haya yameenda kwa kasi ya ajabu tofauti na ilivyozoeleka. Walau angepewa nafasi ya kuweka pingamizi. Kwenda mahakamani ni hatua mojawapo, lakini haitasimamisha mchakato,” amesema Dk Kahangwa.
Amesema kwa sasa Watanzania wanashuhudia kipindi kigumu ambapo harakati za kugombea nafasi zimejaa changamoto na mazingira tata, akitolea mfano mgombea Mpina kuenguliwa kwa namna isiyo ya kawaida.
“Hatukuwahi kushuhudia katika historia ya siasa za vyama vingi nchini, mgombea kuondolewa kwa namna hii. Hii ni ishara kuwa hali inabadilika na siasa zinachukua sura mpya,” amesema mwanazuoni huyo aliyewahi kujitosa kwenye mbio za urais kupitia NCCR-Mageuzi.
Hata hivyo, amesema kuna somo la msingi ambalo vyama vya upinzani vinapaswa kulijifunza la kujenga viongozi wao wa ndani, badala ya kuwategemea waliotoka katika vyama vingine.
“Ina maana hawawezi kutengeneza watu maarufu ndani ya chama? Kwa mfano, kama kweli huu ni mchezo wa kupanga, basi waache kutegemea waliohamia kutoka kwingine. Hii ni mara ya nne wanapokea pigo kama hili,” amesisitiza.
Dk Kahangwa amewashauri viongozi wa vyama vya upinzani kuwa na mikakati ya muda mrefu ya kuandaa wagombea wao badala ya kutegemea njia za mkato, huku akionya kuwa kukimbilia mahakamani mara kwa mara hakutaleta suluhisho la kudumu.
Amesema pia ni muhimu vyama kutambua kuwa, Msajili wa Vyama na Mwenyekiti wa INEC wameteuliwa na mamlaka moja, hivyo kabla ya kuingia kwenye uchaguzi ni vyema kutafuta makubaliano na wadau badala ya kusubiri migogoro.
Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Revocatus Kabobe amesema kilichotokea kinaacha maswali ndani ya ACT-Wazalendo.
“Yawezekana Mpina kuna baadhi ya wanachama wa ACT hawakumtaka au wakati anajitosa kugombea hawakukubaliana wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama, ndiyo sababu miongoni mwao wakamwekea pingamizi.
“Nikisema busara itumike kwa kilichotokea, nitakuwa nakwenda kinyume na utaratibu, maana ACT ni kama imejikaanga yenyewe kwa kumchagua Mpina, lakini taratibu zao za ndani zinakataa.
“Alichokifanya msajili ni kutafsiri kanuni ambazo wenyewe kama chama walijiwekea, kanuni ni zao na aliyemwekea Mpina pingamizi ni mwanachama mwenzao.
“Ambacho naweza kushauri ni kwamba hakuna namna zaidi ya kufuata taratibu na kwenda kwenye kile walichokubaliana kabla,” amesema.
Mchambuzi mwingine, Hamduni Marcel amesema vyama vya siasa vinapaswa kuelewa mamlaka ya Ofisi ya Msajili wakitambua kuwa ofisi hiyo inafanya kazi kwa ukaribu na taasisi nyingine kama INEC.
“Msajili wa vyama vya siasa ndiye mwenye taarifa rasmi za vyama. Anasajili vyama, anahifadhi katiba na mabadiliko yake na ana orodha ya vyama vyote vilivyosajiliwa. Hivyo ni sahihi kuwa ofisi hiyo ndio ya kwanza kushughulikia migogoro ya ndani ya chama,” amesema Marcel.