Watano wafariki ajalini Tunduma, watatu wajeruhiwa

Songwe. Watu watano wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha gari la kubeba abiria aina ya Toyota Hiace na gari la mizigo katika eneo la Chapwa, Halmashauri ya Mji wa Tunduma mkoani Songwe.

Ajali hiyo imetokea leo Agosti 27,2025 saa moja asubuhi, baada ya dereva wa gari aina ya Toyota Hiace kugongana na gari la mizigo.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agustino Senga amesema katika ajali hiyo watu watano wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa. “Miili mitatu kati ya mitano imetambuliwa.”

Kamanda Senga amewataja waliofariki dunia kwenye ajali hiyo kuwa ni Brashimu Msangawale (31), Richard Kashililika (38) na Yotham Mwampashi (71) huku miili miwili ya wanaume haijatambuliwa.

Amewataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni Zaituni Mill (24)na  Bowazi Ndabila.

Kamanda Senga ametumia nafasi hiyo pia  kuwaasa madereva kuchukua tahadhari pindi wawapo barabarani ili kuepusha vifo vinavyoweza kuepukika.

“Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la Hiace kusimama ghafla bila kuchukua tahadhari kwa lengo la kubeba abiria.”

Amesema baada ya ajali hiyo dereva wa gari hilo alikimbia na Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta.

Kwa upande wake shuhuda wa ajali hiyo, Hamisi Mwasumbi amedai dereva wa Hiace hakuangalia nyuma wakati anasimama kubeba abiria kitendo na kusababisha ajali hiyo.

“Ninachoshukuru dereva wa gari la mizigo alikuwa mwendo wa taratibu angekuwa na spidi kali abiria wa Hiace wangekufa wote, hivyo niwasihi madereva wawe makini pindi wanapoendesha vyombo vya moto,” amesema Mwasumbi.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa eneo hilo wameiomba Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania  (Tanroads) kuongeza ukubwa wa eneo hilo kwa lengo la kupunguza ajali madereva wanapopakia abiria.