Mafunzo yafyeka benchi lote Zenji

BAADA ya kushindwa kuiongoza Mafunzo kufikia malengo iliyokusudia msimu uliopita uongozi umeachana na makocha wake wawili – kocha mkuu, Sheha Khamis na msaidizi wake, Abdallah Bakari ‘Edo’.

Mafunzo msimu uliopita chini ya makocha hao ilimaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi 55 baada ya kushinda michezo 16, sare saba na kupoteza saba.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na kitengo cha habari cha klabu hiyo, majukumu ya ukocha kwa sasa yameshikwa na kocha msaidizi Haji Ramadhan Mwambe, ambaye atasimamia kikosi kwa muda hadi pale klabu itakapotangaza rasmi kocha mpya wa kudumu.

Mabadiliko hayo ni mikakati ya Mafunzo katika kuimarisha kikosi chake ili warejeshe makali yao katika ligi kuu Zanzibar ambao kwa miaka ya hivi karibuni yamepotea.

“Nafikiri tumefanya maamuzi sahihi hatujakurupuka mikakati yetu ni kuhakikisha timu inarejea kwenye ushindani na kutwaa mataji ya ndani kitu ambacho hakijafanyika kwa miaka ya karibuni,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, taarifa inaeleza kuwa tayari mazungumzo yameanza na makocha mbalimbali wenye uzoefu wa ndani na nje ya visiwa, jambo linaloashiria kuwa huenda klabu hiyo ikaleta jina kubwa la ukocha msimu huu.

Mashabiki wa tmu ya Mafunzo wamepokea mabadiliko hayo kwa mitazamo tofauti baadhi wakiamini ni hatua sahihi ya kurejesha morali ya timu, huku wengine wakisisitiza kuwa uongozi unapaswa kufanya uamuzi wa haraka kumpata kocha mpya.