DKT. ASHATU KIJAJI AREJESHA FOMU YA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KONDOA

……………

 Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kondoa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Ashatu Kijaji, amesema hana mashaka na ushindi wa chama chake katika uchaguzi ujao kutokana na kazi kubwa aliyoifanya kwa kushirikiana na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali tangu aingie madarakani.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo leo Agosti 27, 2025, mara baada ya kurejesha fomu ya uteuzi wa kugombea Ubunge katika jimbo la kondoa kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mkoani Dodoma.

Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Dkt. Kijaji amesema ana imani kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itatekeleza wajibu wake kwa haki na uwazi, huku akitarajia kutangazwa rasmi kuwa mgombea ifikapo saa 10 jioni leo.

Aidha, Dkt. Kijaji amewashukuru viongozi wa juu wa CCM pamoja na wanachama wa chama hicho kwa imani waliyoionesha kwake kwa mara nyingine, akisema yupo tayari kurejea tena bungeni kuendeleza kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo la Kondoa.

Dkt. Kijaji amewahi kuhudumu kama Mbunge wa Kondoa na pia kushika nafasi mbalimbali serikalini, ikiwa ni pamoja na kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na waziri wa Mifugo na Uvuvi katika awamu zilizopita.