NGALIMANAYO: NIPO TAYARI KUIHUDUMIA KATA YA MJINI KWA MOYO WANGU WOTE.

Songea_Ruvuma.

Mgombea udiwani wa Kata ya Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mathew Ngalimanayo, amerejesha fomu ya uteuzi  Tukio hilo limevuta hisia za wanachama wa kata hiyo, ambao walijitokeza kwa wingi kumuunga mkono kwa furaha na mshikamano wa hali ya juu.

Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Ngalimanayo alisema: “Nipo tayari kulitumikia taifa kupitia nafasi ya udiwani, kwa kushirikiana kwa karibu na wananchi wa Kata ya Mjini. Nitaleta maendeleo ya kweli kwa kuzingatia mahitaji yao halisi na kwa kushirikiana nao bega kwa bega.”

Aidha, amewashukuru wanachama kwa kumuamini tangu alipochukua fomu hadi siku ya kuirejesha, akisema kuwa umoja wao ni ishara ya ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao, ameahidi kuwatumikia kwa uaminifu, uwazi na moyo wa kizalendo.

Ngalimanayo amesisitiza azma yake ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wa Kata ya Mjini, Ametoa wito kwa wakazi wa kata hiyo kuachana na siasa za maneno na badala yake kuelekeza nguvu katika harakati za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Ameeleza kuwa kipaumbele chake ni kuendeleza amani na utulivu uliopo, huku akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila mshikamano na ushirikiano kati ya viongozi na wananchi.

Aidha amewataka wananchi kuendelea kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi ambacho amesema kina sera madhubuti za kuwaletea wananchi maendeleo, amewahimiza kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ili kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo.

Shamrashamra za tukio hilo zilitawaliwa na ngoma za jadi, mavazi ya kijani na njano, pamoja na nyuso za furaha kutoka kwa wananchi waliojitokeza kumuunga mkono.