Dar es Salaam. Kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo Alhamisi,
Agosti 28, 2025 inatajwa mahakamani kwa ajili ya maelekezo maalumu kuhusiana na usikilizwaji.
Katika hatua hiyo pande zote zinatarajiwa kuandaa hoja zinazobishaniwa, kutokana na madai yaliyoainishwa kwenye kesi hiyo, ambazo zitaiongoza Mahakama kufikia uamuzi, kulingana na ushahidi utakaotolewa na pande zote, idadi ya mashahidi wa pande zote na muda wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Kesi hiyo ya madai ya mwaka 2025 imefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na sheria ya vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho.
Pia, wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo wanaomba Mahakama hiyo itoe hukumu na kutamka kwamba walalamikiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.
Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Amri nyingine wanazoomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.
Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na iwaamuru wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo.
Sambamba na kesi hiyo pia walalamikaji hao walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakiiomba Mahakama hiyo itoe amri ya kuwazuia kufanya shughuli zozote za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo ya msingi itakapoamuliwa.
Shauri hilo lilisikilizwa upande mmoja baada ya mmoja wa mawakili wa Chadema aliyefika mahakamani hapo siku hiyo, Jebra Kambole kujitoa muda mfupi baada ya Mahakama kutupilia mbali kiapo kinzani cha wadaiwa, kilichokuwa kinapinga maombi hayo, kutokana na kasoro za kisheria.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa Juni 10, 2025 ilikubaliana na hoja za walalamikaji hivyo ilikizuia kwa muda chama hicho kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali zake mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Walalamikiwa walifungua shauri la marejeo, wakiiomba Mahakama hiyo iondoe amri zake hizo wakidai zilitolewa isivyo halali.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, pamoja na mambo mengine walalamikaji walifafanua hawakupewa haki ya kusikilizwa baada ya wakili wao kujiondoa katika kesi.
Hata hivyo, hoja zao zilipingwa na jopo la mawakili wa walalamikaji, Shaban Marijani, Gido Semfukwe na Alvan Fidelis, wakidai hoja zao hazina mashiko na walipewa nafasi ya kusikilizwa lakini hawakuitumia wenyewe.
Jaji Mwanga katika uamuzi wake alioutoa Agosti 18, 2025, alitupilia mbali shauri hilo baada ya kukataa hoja za chama hicho, kuwa hazikuwa na mashiko kisheria.
Kwanza Jaji Mwanga alisema si dhambi shauri kusikilizwa upande mmoja.
Pia, alisema walalamikaji hao walipewa fursa hiyo ya kusikilizwa lakini hawakutaka kutumia wenyewe, akibainisha wakati Mahakama inapanga tarehe ya usikilizwaji wa maombi hayo ya zuio walalamikiwa pamoja na mawakili wao walikuwepo mahakamani lakini siku ya usikilizwaji hawakufika.
Hivyo alisema halikuwa jukumu la mahakama kuwatafuta walalamikiwa mahali walikokuwa baada ya wakili wao kujitoa.
Uamuzi huo unakifanya chama hicho kuendelea na kifungo hicho mpaka kesi hiyo itakapomalizika au kama itakavyoamuriwa vinginevyo na mamlaka nyingine.
Awali, walalamikiwa walipambana kupangua kesi hiyo kabla ya kufikia hatua ya usikilizwaji, kwa njia za kiufundi bila mafanikio.
Kwanza waliweka pingamizi la ya kesi ya msingi na dhidi ya shauri dogo la maombi ya amri za zuio la muda wakiiomba mahakama iyatupilie mbali bila kuyasikiliza wakibainisha sababu mbalimbali walizodai kuwa ni kasoro za kisheria, lakini yote yalitupiliwa mbali.
Kisha wakaandika barua ya kumkataa Jaji Mwanga kwa madai hawana imani naye kuwa atawatendea haki, huku pia wakifungua shauri hilo la marejeo kuiomba mahakama iondoe amri zake hizo za zuio.
Jaji Mwanga baada ya kusikiliza hoja zao za kumkataa katika uamuzi wake aliwagomea akieleza sababu walizozitoa hazikuwa na mashiko kwani si miongoni mwa za kisheria za kumfanya Jaji au hakimu ajiondoe kwenye kesi.
Hivyo aliamua ataendelea kusikiliza kesi hiyo, ndipo akapanga tarehe ya kusikiliza shauri lao la marejeo dhidi ya amri zake za zuio ambalo pia alilitupilia mbali.
Endelea kufuatilia Mwananchi