SIMBA jana ilicheza mechi ya mwisho ya kirafiki ikiwa kambini Misri, lakini kuna taarifa ya kushtusha baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids kuwaambia mabosi wa klabu hiyo kwamba anahitaji mashine nyingine mpya ya kufungia usajili wa kikosi hicho.
Simba imeshasajili wachezaji kama 10 hadi sasa wakiwamo sita wa kigeni, lakini kocha Fadlu alisema bado anahitaji mchezaji mmoja katika dirisha hili la usajili ambaye ataongeza nguvu katika eneo la kiungo mshambuliaji kuisaidia timu hiyo kuwa bora na kuweza kuishusha Yanga kwenye nafasi iliyopo sasa.
Fadlu ni kama amemtumia ujumbe mdhamini wa klabu hiyo ‘Jayruty’ kuwa ni wakati wake kufanya kile alichokiahidi kwa kumsajilia mchezaji bora namba 10 ambaye atasaidiana na Jean Charles Ahoua ambaye alimaliza kinara wa upachikaji mabao msimu uliopita.

Kocha amefunguka hayo baada ya timu yake juzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wadi Deglas FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri, huku akiweka wazi kuna mambo mazuri anayaona kutoka kwa wachezaji wake lakini bado kuna kazi ya kufanya hasa kwenye eneo la umaliziaji.
Fadlu alisema licha ya mazuri aliyoyaona kwa wachezaji wake bado kuna mambo madogo ya mwisho ambayo lazima wayarekebishe ili waweze kwenda sambamba na timu nyingine kwenye ushindani hasa Yanga ambayo imekuwa bora kwa misimu minne mfululizo.

“Bado tunatafuta mchezaji mmoja bora namba 10 ambaye atakuwa ni mbunifu atakayetupa ubora kwa kusambaza pasi nzuri ndani ya 18 kuwarahisishia washambuliaji wa mwisho kufunga,” alisema kocha huyo katika mahojiano maalumu yaliyofanywa na mtandao wa klabu hiyo na kuongeza;
“Mchezaji aina kama hiyo tunamkosa katika mechi kubwa, kwenye fainali, kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Yanga, hivyo ni muda sahihi kumpata mchezaji huyo, tumepata msaada mkubwa kutoka kwa rais, wa timu, na ametuongeza sana katika usajili, pamoja na skauti na timu ya usajili.”

Fadlu alisema katika hatua hii ya mwisho ya dirisha la uhamisho, mdhamini wao ‘Jayruty’ ataweza kuonyesha uwezo na kuwasaidia kupata uhamisho wa mchezaji mmoja mkubwa mbunifu, mchezaji atakaebadilisha mchezo katika sehemu ya mwisho ya uwanja.
Alisema anaamini kabla ya dirisha kufungwa watakuwa wamefanikisha hilo.

Kocha huyo msimu huu ndiye aliyesimamia sajili za wachezaji waliosajiliwa hadi sasa ambao ni pamoja na Jonathan Sowah, Neo Maema, Rushine De Reuck, Naby Camara, Morice Abraham, Antony Mligo, Mohamed Bajaber, Charles Semfuko na Alassane Kante.
Timu hiyo jana jioni ilicheza mechi ya mwisho ya kujipima nguvu dhidi ya Fassel ya Misri kabla ya leo kuanza safari ya kurejea nchini kujiandaa na Tamasha ya Simba Day na mechi ya Ngao ya Jamii zitakazopigwa mwezi ujao.