KABLA ya kusubiri mchezaji kumuona uwanjani akicheza, kitu cha kwanza kinachotambulisha ubora au udhaifu aliona ni takwimu zake. Masuala ya kufeli au kuingia kwenye mfumo wa kocha, hutokea mbele ya safari, lakini takwimu zikiwekwa mezani, unaweza kusema moja kwa moja kwamba hii ni mali au tumepigwa.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, Yanga SC, wamefanya usafi kidogo kwenye kikosi chake kuelekea msimu wa 2025-2026. Katika usafi ilioufanya kuna kitu cha ziada imekiongeza.
Achana na hadithi ya kubeba makombe matano msimu uliopita 2024-2025 kuanzia pre-season hadi mashindano maalumu, kitu unachotakiwa kufahamu ni kwamba Yanga ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huo.
Katika mechi 30 ilizocheza, ilifunga mabao 83, ikiizidi Simba mabao 14 kwani ilifunga 69, huku Azam ikitikisa nyavu za wapinzani mara 56 na kushika nafasi ya tatu.

Yanga katika mabao hayo 83, matatu yalitokana na wapinzani kujifunga ambao ni Kelvin Kijili (Simba), Jackson Shiga (Fountain Gate) na Joash Onyango (Dodoma Jiji). 80 yaliyobaki yalifungwa na wachezaji 14 kati ya 29 waliovuja jasho kupambania ubingwa huo.
Ukweli usiofichika ni kwamba, takwimu zina nafasi kubwa katika kuonesha thamani ya mchezaji ndani ya timu.
Ukiangalia katika mabadiliko ya kikosi iliyoyafanya Yanga, wachezaji walioondoka walikuwa sehemu ya mchango wa mabao 19, huku wale walioingia wakiwa na jumla ya mabao 37 waliyofunga huko walikokuwa.
Kuna listi ya wachezaji tisa ambao walikuwa na kikosi hicho msimu uliopita, lakini hawatakuwepo msimu ujao. Wapo waliouzwa na walioachwa baada ya mikataba yao kumalizika. Lakini pia kuna mmoja amewekwa pembeni kutokana na kuuguza majeraha ya muda mrefu.
Kati ya nyota hao tisa, watano pekee ndiyo waliokuwa na mchango wa jumla ya mabao 20 ambao ni Aziz Ki (9), Clatous Chama (6), Kennedy Musonda (3) na Khalid Aucho (1) ambao wote waliondoka mwishoni mwa msimu. Mwingine ni Jean Baleke aliyeondoka dirisha dogo akiwa na bao moja.
Mwamba wa Burkina Faso, Stephane Aziz KI ameuzwa kwenda Wydad Casablanca ya Morocco na hadi anaondoka kikosini hapo akiwa amecheza mechi 25 kati ya 30 za ligi, alikuwa amefunga mabao tisa. Umuhimu wake ndani ya timu ulikuwa mkubwa ndiyo maana alitumika kwa dakika 1,676, huku akitoa asisti saba.

Clatous Chama mkataba wake ulimalizika, akiwa ameitumikia timu hiyo kwa msimu mmoja pekee akitokea Simba. Hakuondoka kinyonge kwani alifunga mabao sita katika mechi 24 kati ya 30 za ligi, akitumika kwa dakika 957 pekee. Pia alitoa asisti tatu.
Kennedy Musonda aliyekuwa akicheza eneo la ushambuliaji, ameondoka Yanga baada ya mkataba kumalizika, huku akiwa amefunga mabao matatu akicheza kwa dakika 369. Hakuwa na asisti.
Khalid Aucho aliyejiunga na Singida Black Stars baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika, alifunga bao moja katika mechi 22 za Ligi Kuu Bara msimu uliopita alipocheza kwa dakika 1,735. Pia alitoa asisti moja. Kwa upande wa Jean Baleke aliyefunga bao moja pekee, alicheza mechi tano kwa dakika 188 tu.
Wakati nyota hao wanne wakiwa na mchango wa mabao 19, wengine wanne ambao hawakuwa na mchango wa bao lolote ni Kouassi Attohoula Yao aliyecheza mechi saba kwa dakika 538. Huyu majeraha ya muda mrefu aliyonayo, Yanga imeona imtoe kwenye mfumo ili apone vizuri, huku nafasi yake ikichukuliwa na nyota mwingine wa kimataifa.
Nickson Kibabage amepelekwa kwa mkopo wa msimu mzima kuitumikia Singida Black Stars. Ndani ya Yanga alicheza mechi 12 za ligi kwa dakika 889 bila bao wala asisti.
Jonas Mkude naye mkataba umemalizika akiwa ameitumikia Yanga kwa misimu miwili. Msimu wa mwisho kwenye ligi alicheza mechi tatu pekee kwa dakika 33.

Jonathan Ikangalombo aliyeingia dirisha dogo, naye hatakuwa ndani ya Yanga. Alifanikiwa kucheza mechi sita za ligi, hakufunga bao zaidi ya kutoa asisti mbili.
Waliosema toa kitu weka kitu, hawakukosea kwani Yanga ilichofanya ni kushusha balaa zaidi ya wale walioondoka kufuatia kusajili wachezaji 11 ambao huko walikokuwa kwa ujumla walifunga mabao 39.
Kati ya nyota wapya, Celestin Ecua, namba zake ndiyo zipo juu zaidi kwani alifunga mabao 15 na asisti 15 kwenye Ligi Kuu ya Ivory Coast. Kumbuka msimu uliopita nyota huyo raia wa Ivory Coast alikuwa akiichezea ASEC Mimosas kwa mkopo kutokea Zoman zote za nchini kwao.
Mwingine ni Lassine Kouma aliyetokea Stade Malien ya Mali akifunga mabao saba na asisti tisa kwenye ligi ya huko kwao akiwa anacheza eneo la kiungo mshambuliaji.
Offen Chikola ambaye ni winga mzawa, ametokea Tabora United na msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Bara alifunga mabao saba na asisti mbili.
Kwa upande wa mshambuliaji Andy Boyeli raia wa DR Congo, ametokea Sekhukhune United ya Afrika Kusini akiwa amefunga mabao sita katika mechi 25 za Ligi Kuu Afrika Kusini msimu uliopita akicheza kwa dakika 1368.
Wengine wapya wenye mabao ni beki Mghana Frank Assinki aliyecheza mechi 11 za Ligi Kuu Bara kwa dakika 944 akiwa anaitumikia Singida Black Stars na kufunga bao moja. Mohamed Hussein aliyetokea Simba, alifunga bao moja Ligi Kuu Bara msimu uliopita akicheza mechi 28 kwa dakika 1,802 akitoa asisti nne.
Moussa Balla Conte kutoka CS Sfaxien, Mohamed Doumbia (SC Majestic), Edmund John (Singida Black Stars), Abdulnassir Mohamed Abdallah ‘Casemiro’ na Abubakar Nizar Othuman ‘Ninju’ wote wakitokea Mlandege FC ya Zanzibar.

Ujio wa wachezaji hao wapya, unaifanya Yanga kuongeza wigo wa kupatikana kwa mabao kwani waliokuwepo wana uwezo wa kufunga na kutengeneza, hilo lilijidhihirisha msimu uliopita.
Wachezaji ambao msimu uliopita walifunga mabao na wataendelea kuwepo ndani ya kikosi hicho ni Chadrack Boka (1), Ibrahim Hamad ‘Bacca’ (5), Israel Mwenda (3), Maxi Nzengeli (6), Pacome Zouzoua (12), Mudathir Yahya (3), Duke Abuya (3), Clement Mzize (14) na Prince Dube (13).