Bado Watatu – 11 | Mwanaspoti

“AFANDE kama ulivyosema alama za dole gumba ni zile zile za kwanza. Hii imethibitisha kwamba muuaji ni mtu yule yule,” Ibrahim akaniambia kabla sijakaa kwenye kiti.

Nilipokaa nikamuuliza: “Na zile alama za marehemu mmeshazichunguza?”

“Tumezichunguza kujua kama ni mtu ambaye tuna rekodi naye lakini tumepata matokeo ya kushangaza kama yale tuliyoyapata mwanzo ndio maana nimekuita.”

“Haya mambo ni ya ajabu sana. Unajua huyu mtu pia aliwahi kuhukumiwa kwa kesi ya mauaji hapa hapa Tanga. Baada ya kugundua hilo nimelitafuta faili lake na nimelipata, anaitwa Athony Unyeke. Faili lake hili hapa linaonyesha na yeye alihukumiwa kunyonngwa mwaka jana!”

“Lakini huyu leseni yake inaonyesha anaitwa Anthony Hiza Frank.”

“Katika hili faili kuna jina la Anthony Unyeke.”

“Hebu nipatie hilo faili.”

Nikalichukua faili hilo na kulipitia haraka haraka. Lilikuwa ni faili la mashitaka ya mwaka uliopita ambapo Athony Unyeke alishitakiwa yeye na ndugu yake aliyeitwa Lerry Unyeke kwa kosa la mauaji. Hukumu iliyotoka mwaka uliopita ilikuwa wanyongwe kwa kitanzi mapaka wafe.

“Hapa kuna kitu kimeanza kunitatanisha!”

“Unakumbuka yule mtu aliyenyongwa mara ya kwanza jina lake liliandikwa Ramadhani Unyeke?”

“Kuna uhusiano gani katika hili jina Unyeke.”

“Hapa inaonekana kama vile hawa watu wana uhusiano wa kindugu. Yule wa kwanza alikuwa Ramadhani Unyeke. Huyu wa pili Anthony Unyeke na alishitakiwa pamoja na Lerry Unyeke. Utaona hapa kuna uhusiano.”

“Lakini sasa wote wana majina mengine. Wa kwanza tuliambiwa anaitwa John Lazaro. Huyu wa pili niliambiwa ni Frank na tutakapomgundua huyo wa tatu, ninaamini kwamba tutamkuta na jina jingine.”

“Lazima patakuwa pana kitu kimejificha. Hawa watu ni ndugu.”

“Kwa hiyo unataka niamini kuwa hata hao wawili walioandaliwa kuuawa watakuwa ni ndugu na hawa?”

Pakapita kimya cha sekunde kadhaa. Nilikuwa nimenyamza nikiwaza na Sajin Meja Ibrahim naye alikuwa akiwaza.

“Lile faili la Ramadhani Unyeke bado upo nalo?”

“Sijalirudisha bado.”

“Tafadhali nipatie. Nitalichukua na hili ili nikasome vizuri mashitaka yao.”

Sajin Meja Ibrahim alinitolea faili la Ramadhani Unyeke. Nikalichukua na lile lililokuwa juu ya meza yake kisha nikamuaga na kuondoka nayo.

Nilikwenda ofisini kwangu na kuanza kuyasoma yale mafaili kwa kirefu. Nikagundua kwamba katika uchunguzi wa polisi kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wakituhumiwa kwa kufanya kosa la mauji. Kwa mujibu wa mafaili yote mawili, watu hao walituhumiwa kumuua mtu aliyekuwa anaitwa Thomas Christopher na kisha kumzika.

Walitofautiana katika kukamatwa. Aliyekamatwa kwanza alikuwa Ramadhani Unyeke akashitakiwa wakati wenzake walikuwa wakiendelea kutafutwa.

Baadaye walikamatwa Athony Unyeke na Lery Unyeke nao wakashitakiwa wakati mwenzao alishatolewa hukumu ya kunyongwa.

Wao walifunguliwa faili la peke yao kama ambavyo lilikuwa mikononi mwangu nikilisoma wakati ule. Washitakiwa hao wawili nao wakahukumiwa kunyongwa.

Sasa kilichonishitua hapo na kunipa taharuki ni lile jina la mtu ambaye aliuawa, Thomas Christopher. Hilo jina lilikuwa ndilo la muuaji niliyekuwa ninamtafuta ambalo nililipata kwenye usajili wa namba ya simu yake.

Yeye ndiye aliyewasiliana na mtu aliyenyongwa mara ya kwanza na wakanywa pombe chumbani kwake. Namba yake niliipata kwenye simu ya marehemu.

Lakini katika yale mafaili ya polisi, inaonekana yeye ndiye aliyeuawa na watu hao.

Hapo ndipo nilipoanza kuchanganyikiwa. Nikahisi ule uchunguzi ulikuwa unanichanganya. Ulinichanganya kwanza kwa sababu wahusika wote walikuwa ni marehemu.

Pili wahusika wote wanaonekana kama walifufuka baada ya kufa. Aliyeuawa kwanza na kusababisha kuwepo na mashitaka, Thomas Christopher alifufuka na kuwaua kwa kuwanyonga watu waliokuwa wamemuua ambao nao wanaonekana kama walifufuka tena baada ya kunyongwa kutokana na hukumu ya mahakama.

Nilijaribu kuwaza ilikuwaje mtu ambaye aliuawa karibu miaka miwili iliyopita awaue watu ambao walimuua yeye, ambao nao walishanyongwa karibu mwaka mmoja na nusu uliopita? Kwa kweli sikupata jibu. Akilini mwangu nilikuwa nikiona kiza kitupu!

Katika utumishi wangu nikiwa katika jeshi hili la polisi sikuwahi kupambana na kesi ngumu na iliyokuwa inatatiza kama ile.

Nikaona niende kwa ofisa upelelezi wa mkoa nikapate ushauri wake. Nikaenda.

Nilipofika nikamueleza matatizo yaliyokuwa yamejitokeza katika uchunguzi wangu. Yeye naye akapatwa na mshangao.

“Hebu kesho asubuhi nenda tena kwa ofisa wa magereza akueleze kuhusu hawa wafungwa wawili Anthony na Lery. Tunahitaji kujua kama walishanyongwa au waliachiwa kwa rufaa,”

“Kama atakwambia kwamba walikata rufani na kuachiwa huru tutajua walikuwa hai.”

“Na kuhusu Thomas Christopher tutajua nini?”

“Yeye alithibitishwa kuwa aliuawa mpaka mahakama ikatoa adhabu ya kifo kwa kina Unyeke.”

“Sasa kwanini inaonekana kwamba yuko hai na ndiye anayewaua wenzake.”

“Itakuwa ni miujiza!”

“Afande mimi siamini miujiza lakini sasa nitaamini!”

“Kesho nenda gerezani tuanze kulifumbua suala la kina Unyeke kwanza.”

“Sawa afande nitakwenda.”

“Hayo mafaili utayaacha kwangu mpaka hapo utakapoyahitaji?”

“Kwa sasa yabaki tu. Nitakapoyahitaji nitayafuata huku.”

Nilipanga nikitoka kwa ofisa upelelezi wa mkoa niende nyumbani nikapumzike lakini sikurudi nyumbani. Akili yangu ilinituma niende kwa mzee Rajab kule Kisosora.

Nilipofika nikamkuta amekaa barazani mwa nyumba yake kwenye kiti chake cha uvivu akivuta mtemba wake. Niliposhuka kwenye gari nikamuamkia na kumpa mkono.

“Marahaba Inspekta. Habari yako?”

“Habari si nzuri” nikamwambia nikiwa nimesimama karibu yake.

“Kumetokea nini kingine?”

“Sijasikia. Kumetokea nini?”

“Yule mtu ambaye ulinielekeza kwake naye amenyongwa!”

Mshituko ulimfanya mzee Rajab ainuke kwenye kiti.

Nikamueleza mzee Rajab nilivyokwenda nyumbani kwake na kumkuta akining’inia kwenye kitanzi.

Mzee akatikisa kichwa kusikitika.

“John Lazaro amenyongwa… na yeye amenyongwa!”

“Na tumegundua kwamba wote wamenyongwa na mtu mmoja”

“Mtu mwenyewe hatujamgundua bado. Hapo tutakapomtia mikononi ndio tutamtaja.”

“Na kwaninii anawanyonga wenzake namna hii?”

“Haijafahamika bado na ndiyo maana nimerudi tena kwako.”

Nilipomwambia hivyo mzee Rajab akanikazia macho.

“Unamfahamu vipi huyu Frank?” nikamuuliza.

“Mbona watu wengi wanamfahamu. Yule ni mtaalamu wa umeme. Hata hii nyumba ninayoishi ni vijana wake walionisambazia nyaya za umeme. Simfahamu zaidi ya hapo.”

“Unawafahamu ndugu zake?”

“Unamfahamu mtu anayeitwa Thomas Christopher?’

“Ndiyo kwanza nalisikia hilo jina.”

“Unamfahamu mtu anayeitwa Athony Unyeke?”

Nilikuwa nimemzunguka akili mzee Rajab. Lakini hakuingia kwenye mtego wangu.

“Hao watu wote unaonitajia siwafahamu.”

Nikajiambia inaelekea mzee Rajab hakuwa akifahamu kuwa Frank alikuwa ndiye Anthony Unyeke.

 “Uchunguzu wetu umeonyesha kwamba aliyekuwa mpangaji wako John lazaro na huyo Frank ni ndugu. Wewe ulikuwa hufahamu hilo?”

“Walikuwa ndugu?” Mzee akaniuliza.

“Sina uhakika lakini inawezekana kwa sababu Frank ndiye aliyemleta kwangu Lazaro.”

“Alikwambiaje, alikuwa ndugu yake?”

“Tatizo ni kwamba hakunieleza kwa undani kuhusu uhusiano wao. Mimi nilichukulia kuwa walikuwa marafiki tu. Mmegunduaje kuwa walikuwa ndugu?”

“Kuna kitu kimoja ambacho sijakwambia. Majina ya hawa watu yanayofahamika huenda si majina yao halisi. Katika kumbukumbu zetu za kipolisi tumeona kwamba John Lazaro anaitwa Ramadhani Unyeke na Frank anaitwa Athony Unyeke.”

Mzee Rajab alikuwa amenyamaza akinisikiliza kwa makini. Nikaendelea kumueleza.

“Kuna mtu mwingine ambaye anaitwa Lerry Unyeke ambaye tunahisi pia ni ndugu yao.”

“Mimi sikuwa nikifahamu kwamba John Lazaro alikuwa na jina jingine. Hao ndugu zake pia sikuwa nikiwafahamu. Na sijui hao watu mmewajuaje.”

“Ngoja nikueleze tulichokigundua. Hao watu wote niliokutajia waliwahi kushitakiwa kwa kosa la mauaji na wote walikuwa wamehukumiwa kunyongwa…”

Mzee Rajab alishituka na kuniuliza.

“Mafaili yao yapo polisi. Tumeyagundua baada ya uchunguzi. Sasa kitu ambacho kimetupa wasiwasi ni kwamba kama hao watu walihukumiwa kunyongwa kwanini walikuwa bado wapo uraiani mpaka wakauawa na mtu asiyefahamika?”

“Inawezekana walikata rufani.”

“Kumbukumbu zetu zinaonyesha hawakukata rufani. Na kwa uapnde wa John Lazaro faili lake linaonyesha kwamba alishanyongwa na hayupo tena duniani.”

“Alinyongwa tangu mwaka jana.”

“Mh! Sasa kama alishanyongwa, yule alikuwa mzuka labda!”

“Mzee uliwahi kusikia kwamba mzuka unaishi na watu?”

“Mzuka ni mfano wa mtu aliyekwishakufa ambao unaonekana na watu.”

“Na unaweza kuuawa tena?”

“Mzuka hauwezi kuuawa kwa sababu ni mtu ambaye tayari ameshakufa.”

“Kwa maana hiyo John Lazaro hatakuwa mzuka.”

“Nataka nikwambie mzee wangu kwamba hili suala linaumiza akili yangu.”

“Linastahili kukuumiza. Ni suala zito na lina utata!”

Pakapita ukimya mfupi kabla ya kuamua kumuaga mzee Rajab na kuondoka.

Asubuhi ya siku iliyofuata nikaenda gereza la Maweni. Nilifanikiwa kumkuta mkuu wa gereza hilo ambaye aliponiona alishangaa kidogo.

“Karibu,” akaniambia huku akinitazama kwa macho ya shauku.

“Asante. Nimekuja tena kwako” nikamwambia huku nikiketi.

“Kuna tatizo gani jingine?”

“Tatizo ni kama lile la kwanza. Kuna watu wawili ambao wanafahamika kwa majina ya Athony Unyeke na Lerry Unyeke ambao walihukumiwa kunyongwa mwaka jana. Nilitaka kujua kama walishanyongwa.”

“Kesi yao ilikuwa namba ngapi na ya mwaka gani?”

Nilikuwa nimekwenda na kumbukumbu zangu. Nikamtajia namba ya kesi hiyo na mwaka wake.

Zilimchukua afande huyo wa magereza dakika zisizopungua thelathini kulipata faili la kina Unyeke.

Alipolitupia macho aliniambia.

“Anthony Unyeke na Lerry Unyeke walishanyongwa. Hatuko nao”

Nikashituka na kumuuliza.

“Walinyongwa lini?”
Inaendelea…