Ada-Tadea yaja na ujenzi wa daraja Bagamoyo – Zanzibar

Dar es Salaam. Miundombinu ndiyo injini ya maendeleo na ukuaji wa uchumi wa taifa lolote. Nchi yenye barabara za kisasa, bandari bora, reli za kisasa na viwanja vya ndege vyenye viwango vya kimataifa pamoja na madaraja imara hujipatia fursa kubwa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Tanzania ikiwa na jiografia ya kipekee, utajiri wa maliasili na ardhi yenye rutuba katika nchi za Afrika Mashariki, bado imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya miundombinu isiyokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Kwa miaka mingi, mipango ya miundombinu imekuwa ikitekelezwa kwa matumizi ya muda mfupi, jambo linalosababisha barabara kubomolewa kila mara na kujengwa upya.

Wataalamu wanasema tatizo la kulazimika kurudia miradi kila mara hutokana na kutokuwa na mpango wa muda mrefu unaozingatia ongezeko la watu, ukuaji wa teknolojia na mabadiliko ya kiuchumi.

Chama cha African Democratic Alliance (Ada-Tadea) kupitia ilani yake kimeliangalia tatizo hilo na kuweka bayana mkakati wa kufanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya miundombinu.

Chama hicho kinapendekeza mipango ya maendeleo iandaliwe kwa mtazamo wa miaka 100 ijayo, badala ya kuishia kwenye miradi ya muda mfupi inayokumbwa na changamoto za miji kukua haraka.

Miongoni mwa miradi mikubwa iliyotajwa katika ilani ya Ada-Tadea, ni ujenzi wa daraja la kipekee litakalounganisha Bagamoyo na Zanzibar, hatua ambayo itakuwa historia katika Afrika Mashariki na itaongeza zaidi mshikamano wa Muungano.

Daraja hilo linatarajiwa kubadilisha kabisa mfumo wa usafiri kati ya bara na visiwani, huku likihusiana moja kwa moja na mabadiliko makubwa kwenye barabara, bandari, reli na viwanja vya ndege.

Ada-Tadea inasema endapo itapewa dhamana itahakikisha ujenzi wa daraja la Bagamoyo hadi Zanzibar unafanyika kwa viwango vya juu vya kiufundi na kiteknolojia. Lengo ni kurahisisha safari kati ya pande hizo bila kutegemea vivuko au ndege pekee.

Ilani hiyo inabainisha kwamba kwa kutumia daraka hilo wananchi watasafiri muda wowote bila vizuizi, hali ambayo itakuza biashara, utalii na mshikamano wa kijamii.

Pia, daraja hilo litaongeza kasi ya usafirishaji wa bidhaa na watu, huku likiimarisha uwekezaji kati ya Bara na Visiwani.

Kufuatia ahadi hiyo, wataalamu wa uchumi wanasema mradi huu utakuwa chachu ya ongezeko la pato la Taifa, kwani utarahisisha uwekezaji mkubwa katika viwanda, utalii na kilimo kinachopelekwa masokoni kupitia Zanzibar.

Mtaalamu wa miundombinu, Zacharia Singano amesema wazo la Ada-Tadea ni zuri lakini kuna changamoto za kiufundi zimeelezwa kuwa kubwa kutokana na jiografia na tabia za Bahari ya Hindi.

“Umbali wa bahari kati ya Bagamoyo na Zanzibar ni zaidi ya kilomita 30 na sehemu nyingi zina kina kirefu chenye zaidi ya mita 50 hadi 100,” amesema Singano.

Amesema eneo hilo pia linakumbwa na mawimbi makubwa pamoja na mikondo yenye nguvu. “Kwa hali hiyo, ujenzi wa daraja hautakuwa wa kawaida kama wa barabara ya kawaida au madaraja ya kwenye mito. Unahitaji teknolojia ya hali ya juu inayotumika kwenye miradi mikubwa ya kimataifa, kama madaraja marefu yaliyojengwa China, Japan au Korea Kusini,” amesema Singano.

Amesema changamoto hizo zinahusisha pia masuala ya msingi wa nguzo, ambazo zinapaswa kuchimbwa chini kabisa ya bahari kwa usalama wa daraja.

Aidha, zana za chuma na zege zitakazotumika zitalazimika kuwa za kustahimili chumvi ya bahari, kutu, upepo mkali na matetemeko madogo ya ardhi yanayoweza kutokea kwenye eneo la mwambao.

“Hii inamaanisha maandalizi ya usanifu na upembuzi yakinifu pekee yanaweza kuchukua miaka kadhaa, na gharama za awali zitakuwa kubwa sana, kabla hata ya hatua ya ujenzi kuanza,” amesema

Barabara za njia nne hadi nane

Ilani ya Ada-Tadea imeweka mkakati wa kubadilisha kabisa mfumo wa ujenzi wa barabara. Katika mpango huo, inasema barabara zote za kimkakati zitajengwa kwa kiwango cha kisasa, huku barabara zinazoingia kwenye majiji zikiwa na njia nane, zile za manispaa njia sita na za miji njia nne.

Vilevile, inasema ikipewa ridhaa itajenga njia maalumu za watembea kwa miguu na vivuko vya chini au juu kutegemea jiografia ya eneo, ili kuepusha ajali na kupunguza gharama za ubomoaji wa nyumba za wananchi.

Hatua hii inalenga kuwalinda wananchi dhidi ya umasikini unaotokana na fidia zisizo na tija na kuondoa msongo wa mawazo unaowapata wanapobomolewa nyumba zao.

Sekta ya bandari nayo imepewa kipaumbele kwenye ilani ya Ada-Tadea. Imeahidi kuziboresha bandari zote nchini kwa kuzifanya za kisasa na zenye vifaa bora vya kushughulikia mizigo na abiria.

Bandari za Kigoma, Mwanza, Musoma, Bukoba, Mbamba Bay na Itungi zitafanyiwa ukarabati mkubwa ili ziwiane na kasi ya biashara.

Aidha, bandari kavu katika maeneo ya Pwani, Kigoma, Fela, Mtwara, Mbamba Bay na Isaka zitajengewa miundombinu rafiki ili kuongeza ufanisi wa upitishaji bidhaa mbalimbali. Hatua hii inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kuubadilisha usafiri wa anga

Katika sekta ya anga, Ada-Tadea imekusudia kuboresha viwanja vya ndege vya Mtwara, Kigoma, Mwanza na Mbeya kwa viwango vya kimataifa ili viweze kuhudumia ndege kubwa na kuunganisha Tanzania moja kwa moja na nchi jirani.

Vilevile, viwanja vya Singida, Songea, Shinyanga, Iringa, Bariadi, Bukoba na Musoma vitaongezewa hadhi ili kuendana na kasi ya ukuaji wa miji hiyo.

Hatua hii inalenga kupunguza msongamano wa safari kwenye viwanja vikuu na kurahisisha huduma kwa wananchi walioko mikoani.

Ilani hiyo imeweka mkakati wa kukamilisha reli ya kati kuelekea Kigoma na Mwanza, kuanza ujenzi wa reli mpya kwenda Burundi na Mpanda na kufufua reli zilizopendekezwa tangu miaka ya 1970.

Hizi ni pamoja na reli ya Mtwara–Mbamba Bay, reli ya Tanga–Musoma na reli ya Itigi–Ziwa Eyasi kupitia Singida hadi Songea.

Mradi huu unalenga kuunganisha rasilimali za taifa, hasa chuma, makaa ya mawe, soda na masoko ya kikanda na kimataifa, hivyo kuchochea mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

Ada-Tadea imetaja mkakati wa kuimarisha usafiri wa mijini kwa kujenga njia za mwendokasi katika miji mipya kama Dodoma na reli za juu (metro trains) katika miji yenye jiografia tata kama Mwanza.

Pia, inasema kutakuwa na uwekezaji kwenye usafiri wa waya (cable cars) katika maeneo ya milima ili kurahisisha usafiri wa wakazi.

Jijini Dar es Salaam, mfumo wa mabasi ya mwendokasi utaimarishwa kupitia ubia wa PPP kati ya Serikali na kampuni binafsi za wazawa, huku magari ya daladala yakiwekewa mazingira bora ya ushindani. Hatua hii inalenga kupunguza msongamano na kuboresha uzoefu wa usafiri wa wananchi mijini.