Dar es Salaam. Katika jitihada za nchi kuachana na matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa, mjadala unaibuka mitaani kuhusu matumizi ya gesi ya kupikia na athari zake kwenye ladha ya vyakula.
Wapo wanaodai kuwa vyakula vinavyopikwa kwa kutumia gesi ukiwamo wali, havina ladha ikilinganishwa na unaopikwa kwa kutumia kuni au mkaa.
Lakini je, madai haya yana ukweli kwa kiwango gani? Mwandishi wa makala haya amezungumza na baadhi ya wananchi na wataalamu kuhusu suala hili.
Stumai Seif, anayefanya biashara ya kupika vyakula na mkazi wa Chanika mkoani Dar es Salaam, anasema amejaribu kutumia gesi kupikia lakini haridhishwi na matokeo ya ladha, hasa wali.
“Ukiniambia nipike wali kwa kuni au mkaa, utasikia kabisa harufu nzuri na ladha tamu. Lakini gesi… ni kama chakula hakijaiva vizuri au kimekosa ladha ya asili,” anasema.
Kauli kama hii si ya kwake peke yake, Juma Salum, fundi seremala anayefanya shughuli zake Ilala jijini Dar es Salaam naye ana maoni sawa na ya Stumai.
Anasema, “wali unaopikwa kwa gesi unakosa ule utamu tuliouzoea kwa mapishi ya jadi. Labda ni moto wake, maana gesi huwa ya haraka sana, huwezi kudhibiti moto kama kwenye mkaa.”
Mwingine anayeungana nao ni Sada Amir, mkazi wa jijini Mwanza anasema, “ladha ya wali unaopikwa kwenye mkaa au kuni ina tofauti. Kwenye mkaa kwanza wali unanukia sana, unakuwa na ladha nzuri hasa ukibanikwa kwa juu.
“Lakini kwenye gesi wali unakuwa kawaida. Na wakati mwingine kuiva vizuri inakuwa changamoto au unaungua kwa sababu kwenye gesi kuna shida ya kupata kiwango cha moto sahihi kwa kupika wali hasa maji yakikauka, hivyo ni rahisi kuungua na kufanya harufu na ladha kuwa mbaya.”
Hata hivyo, wataalamu wa lishe na wapishi wa kitaalamu wanapinga dhana hiyo.
Mtaalamu wa lishe Esther Bundala anasema tatizo si aina ya nishati, bali namna ya kupika.
“Gesi ni safi na haina harufu, lakini kwa wapishi wengi wa nyumbani, hawajazoea kuitumia kwa ufanisi. Moto wa gesi unahitaji uangalifu zaidi kudhibiti kiwango chake kwa ufasaha,” anaeleza.
Naye mpishi katika hoteli moja jijini Zanzibar, Asumini Jumanne anasema, “katika hoteli zetu, tunapika kwa gesi na chakula kinakuwa na ladha ya juu. Kinachotakiwa ni uelewa wa kutumia gesi vizuri, kama vile kutumia sufuria zenye mfuniko mzuri, kupika kwa muda unaofaa, na kutumia viungo ipasavyo.”
Mdau wa nishati, Sifuni Mbaga anasema elimu kwa jamii inapaswa kutolewa kuhusu matumizi ya nishati safi kuwa, hayaharibu chochote katika upishi.
“Tunahitaji kuwaelimisha wananchi kuwa gesi ni salama na inaweza kupika chakula chenye ladha bora kama tu itatumiwa kwa njia sahihi,” anaeleza Mbaga.
Mwananchi imebaini changamoto ya baadhi ya watumiaji wa nishati ya gesi wanaosema, nishati hiyo licha ya uzuri wake, ina gharama katika kutumia hasa upishi wa baadhi ya vyakula.
Amina Ally, mkazi wa jijini Dar es Salaam amekuwa akitumia gesi kwa miaka mingi, hata hivyo anasema hawezi kutumia nishati hiyo kupikia vyakula kama maharagwe.
‘’ Unawezaje kupika mfano maharagwe kwa nusu saa nzima, hiyo gesi si itabidi ununue utumie wiki mbili imeisha? ‘’ anahoji na kuongeza kuwa yeye amekuwa akitumia gesi kwa kuungia mboga au kupasha moto vyakula.
Shaka ya Amina, ndiyo kilio cha walio wengi nchini, wanaoamini kuwa nishati hiyo pamoja na uzuri wake bado imekuwa gharama kwa watumaji wengi.
Pengine kama ingekuwa ni nishati nafuu, Amina na wengineo wasingeona gharama kutumia gesi kupikia vyakula vinavyoiva kwa muda mrefu.
Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, inalenga kuhakikisha kaya zote nchini zinatumia nishati safi kufikia mwaka 2034.
Mkakati huo umeweka bayana kuwa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya nishati safi ni muhimu.
Aidha, mkakati unahimiza upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kupikia kama majiko yenye uwezo wa kudhibiti joto ili kusaidia upishi uwe bora na wa ladha.
Ingawa baadhi ya wananchi bado wanaona gesi kama chanzo cha kupotea kwa ladha ya chakula, ukweli ni kuwa matumizi sahihi ya gesi yanaweza kuboresha ubora wa chakula, huku pia yakilinda afya na mazingira.
Ni wakati wa jamii kuachana na nishati chafu kwa kupewa elimu sahihi na kuwezeshwa kupata vifaa bora vya kupikia.
Kwa mujibu wa mkakati huo, mkazo hauwekwi pekee kwa wananchi kutumia nishati ya gesi, bali kuna aina mbalimbali zinazoweza kutumika ikiwamo mkaa mbadala ambao pengine unaweza kuwa kimbilio kwa wale wanaoamini kuwa ladha ya vyakula hainogi pasipo mkaa.
Aina nyingine za nishati safi zinazotajwa na mkakati ni pamoja na umeme, bayogesi, gesi asilia, LPG, bayoethano, nishati ya jua na majiko banifu.
‘’Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya upatikanaji wa nishati nchini ikiwamo miradi ya kuzalisha na kusambaza umeme, miradi ya utafutaji, uzalishaji na usambazaji wa gesi asilia, bayogesi, bayoethano pamoja na LPG, ‘’ inaeleza sehemu ya mkakati huo.
Hali ya matumizi ya gesi asilia nchini
Gesi asilia inatambulika kuwa safi ikilinganishwa na nishati nyingine zitokanazo na mafuta ya petroli kwa sababu inatoa kiasi kidogo cha hewaukaa. Gesi asilia inayopatikana nchini Tanzania ina kiwango cha methani takribani asilimia 97.
Hadi sasa, kiasi cha gesi asilia kilichogundulika nchini ni takribani futi za ujazo trilioni 57.54. Gesi asilia ilianza kutumika nchini, Mwaka 2004 kwa ajili ya kuzalisha umeme, matumizi ya viwandani na majumbani.
Gesi kutoka katika mikoa ya Mtwara na Lindi inasafirishwa kupitia mifumo miwili ya miundombinu ya mabomba, mfumo mmoja wa kilomita 551 una mabomba kutoka Songo Songo Lindi na Mnazi Bay Mtwara na kuungana Somangafungu Lindi hadi Dar es Salaam.
Mfumo mwingine wa kilomita 232 unatokea Songo Songo Lindi kupitia Somangafungu hadi Dar es Salaam.
Katika kipindi cha mwaka 2021/22, Tanzania ilizalisha futi za ujazo milioni (MMscf) 72,533.56 za gesi asilia ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na MMscf 60,691.12 zilizozalishwa 2020/21.
Aina nyingine ya gesi ni LPG. Hii ni gesi ya kupikia inayohifadhiwa katika mitungi ambayo uzalishaji wake unatokana na uchakataji wa mafuta ghafi na gesi asilia yenye kiwango cha propani na buteni kinachozidi asilimia 15.
Tanzania imekuwa ikiagiza LPG kutoka nje ya nchi kwa kuwa utafutaji unaoendelea nchini bado haujagundua mafuta na hakuna kiwanda cha kuchakata mafuta ghafi.
Vilevile, gesi asilia iliyogunduliwa nchini ina kiwango kidogo cha propani (asilimia 0.3) na buteni (asilimia 0.06) ambacho hakitoshi kuzalisha LPG. LPG iliyoingizwa nchini kwa mwaka 2022 ni metriki tani 250,200 kati ya hizo, metriki tani 160,610 zilitumika nchini na metriki tani 89,590 zilipita kuelekea nchi jirani.
Aidha, matumizi ya LPG yameongezeka nchini kutoka metriki tani 20,000 mwaka 2010 hadi metriki tani 160,610 mwaka 2022.