Maswa. Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemuhukumu kifungo cha miaka mitano gerezani, mkazi wa Kijiji cha Malampaka, Zackaria Shija (38), kwa kosa la kuishi kinyumba na kumpa ujauzito mwanafunzi mwenye umri wa miaka 20.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 27, 2025 na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Aziz Khamis, ambaye amesema mtuhumiwa atahukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kila kosa, lakini adhabu hizo zitakwenda pamoja, hivyo atatumikia kifungo jumla cha miaka mitano gerezani.
Pia, mshtakiwa ameagizwa kulipa fidia ya Sh300,000 kwa mwanafunzi huyo.
Hakimu Khamis amesema Shija amehukumiwa adhabu hizo kutokana na makosa aliyoyatenda kwa nyakati tofauti katika kipindi cha Aprili, 2025, kijiji cha Malampaka, wilayani Maswa.
Mbele ya Mahakama hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mkaguzi wa Polisi, Vedastus Wajanga, ameeleza kuwa mshtakiwa alikamatwa na Jeshi la Polisi Aprili 25, 2025, akiwa anaishi na mwanafunzi huyo kama mke wake.
Wajanga amesema kwa mara ya kwanza alifikishwa katika Kituo Kidogo cha Polisi Malampaka, kabla ya kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Maswa, na baadaye kufikishwa mahakamani ambapo alisomewa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha jumla ya mashahidi saba pamoja na vielelezo vinne, ambapo miongoni mwa mashahidi hao alikuwa ni mwanafunzi mwenyewe.
Mahakama ilijiridhisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo.
Hata hivyo, katika utetezi wake, Shija alikana kuhusika na makosa hayo, akidai kuwa alikuwa anamlea mwanafunzi huyo kwa moyo wa huruma kama msamaria mwema.
“Mheshimiwa Hakimu mimi nasingiziwa kwani nilimchukua binti huyu kwa nia njema tu nikiwa msamaria mwema kwa ajili ya kumlea tu,” amesema.
Baada ya kusikiliza utetezi huo, Mahakama ilitupilia mbali madai yake kwa kutokuwa na mashiko na kumuhukumu kifungo cha miaka mitano jela kwa kila kosa.
Hakimu alielekeza kuwa adhabu hizo zitakwenda kwa pamoja, hivyo atatumikia kifungo cha jumla ya miaka mitano.
