Njano na kijani zatawala Dar ,CCM kikizindua kampeni

Dar es Salaam. Ni kijani na njano! ndiyo hali halisi ilivyo katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, wanachama, wapenzi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliovalia sare za chama hicho wakiendelea na hekaheka za uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Katika jiji la Dar es Salaam hususani kwenye maeneo ya Mbezi Louis hadi Ubungo, kwenda mpaka Mwenge ni rangi za njano na kijani ndizo zimeshamiri, makada hao wakielekea viwanja vya Tanganyika Packers,  Kawe kwenye shamrashamra za uzinduzi wa kampeni za chama hicho zinazofanyika leo Alhamisi Agosti 28, 2025.

Mwananchi iliyokuwa kwenye mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, imeshuhudia funga kazi kwenye njia panda ya kwenda Kawe, ambako mamia ya wanachama wakiwa wameongozana kuelekea viwanja vya Tanganyika Packers, huku Polisi wa kutuliza ghasia (FFU), Polisi wa Usalama Barabarani na askari wa Jeshi la Wananchi baadhi wakiwa makini kuimarisha ulinzi na usalama huku wakiyaongoza magari na raia.

Katika eneo yalipojengwa maduka Lugalo Jeshini, daladala zinazopita njia hiyo kuelekea Kawe, zinaelekezwa kugeuzia  hapo na hakuna inayoruhusiwa kufika Kawe mwisho ambako ndipo ulipo uwanja wa Tanganyika Packers. 

Katika eneo zilipo flemu za maduka Lugalo ambako ndipo kituo cha daladala kuna wanajeshi wametawanyika sehemu tofauti tofauti, wengine wakiongoza magari yanayogeuzia hapo, wengine wakiongoza mamia ya wananchi wanaoshuka kwenye daladala hizo.

Mbali na wanajeshi hao, pia askari wa kutuliza ghasia ambao hawana silaha, wanaendelea kusimamia na kuhakikisha usalama wa mamia ya wafuasi na wapenzi wa chama hicho wanakuwa salama.

Askari wa usalama barabarani nao hawajabaki nyuma, wanaendelea na jukumu lao la kuhakikisha hakuna foleni ya magari ambayo mengi ni ya binafsi na ya umma yakiegeshwa  mbali kidogo na vilipo viwanja vya Tanganyika Packers.

Hata hivyo, utaratibu huo unaonekana kuibua fursa kwa waendesha bodaboda ambao wanabeba abiria kwa Sh1,000 mpaka Sh2,000 kutoka Kawe Mwisho hadi eneo zilipo flemu za maduka kwenye fensi ya Lugalo ambako daladala zinaishia, kwa wale ambao wako Kawe kwa ratiba zingine na si kampeni za CCM.

Katika mitaa ya Kawe, kuanzia kituo cha Kanisani kuelekea hadi Tanganyika Packers katika nguzo za umeme, kumepambwa kwa bendera za CCM ambazo zinapepea kila upande.

Mamia ya wananchi wenye sare za chama hicho wanapishana wengine wakiingia na wengine wakitoka, wote wakiwa na shauku ya shamrashamra hizo za ufunguzi wa kampeni.

Katika mkutano huo, mgombea urais wa chama hicho,  Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi watatambulishwa kwa Watanzania kabla ya kuendelea na kampeni katika mikoa mbalimbali nchini kuanzia kesho kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM.