Dar es Salaam. Maelfu ya wapenzi, wafuasi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza kushiriki uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025.
Hadi kufikia saa 8:30 mchana katika viwanja vya Tanganyika Packers, unapofanyika mkutano huo wa ufunguzi ulikuwa umefurika maelfu ya wananchi.
Walinzi wanaosimamia usalama, ilipofika saa 7:16 mchana walizuia watu kuendelea kuingia kwa kutumia geti namba moja, wakieleza eneo hilo limejaa, wakitaka wananchi kutumia geti la pili, ambako nako mamia ya wananchi walikuwa wamefurika na wakati wowote palitarajiwa kujaa kutokana na idadi ya watu waliopo nje.
Pembeni mwa viwanja hivyo, maelfu ya wananchi pia wanaendelea na pilikapilika, wengine wakifanya biashara na wengine wakiendelea na shamrashamra za ufunguzi wa kampeni hizo.
Inaelezwa tangu saa 12 asubuhi wananchi walianza kuwasili katika viwanja hivyo.
Misafara ya viongozi imeanza kuwasili viwanjani hapo saa 7:41 mchana, ikipishana kwa dakika chache.
Shamrashamra hizo zimegeuka kero kwa watumiaji wa usafiri wa umma kutoka Kawe kwenda kwenye maeneo mengine ya jiji.
Katika eneo la Kawe, kuanzia round about ya Kawe kama unatokea Mbezi Beach, kwenda hadi Ukwamani, kuanzia saa 6 mchana hadi sasa hakuna daladala inayoruhusiwa kuingia, isipokuwa zile zilizokodiwa kubeba watu wanaokwenda kwenye mkutano ambazo zikishashusha abiria zinapaki.
Mamia ya wananchi wanaotokea Kawe wanalazimika kutembea kwa miguu ili kusogea eneo ambako watafanikiwa kupata usafiri wa umma.
Katika mkutano huo, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi wanatambulishwa rasmi kwa Watanzania kabla ya kuendelea na kampeni katika mikoa mbalimbali nchini.
Samia ni miongoni mwa wagombea 17 walioteuliwa na INEC jana Jumatano Agosti 27, 2025 kwa ajili ya kugombea urais katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
