Sh12 bilioni kutumika uchaguzi mkuu Zanzibar, vyama 17 kushiriki

Unguja. Licha ya ratiba ya uchukuaji wa fomu za uteuzi wa nafasi za urais, uwakilishi na madiwani kuanza leo, lakini kwa nafasi ya urais vyama vya siasa vimeandika barua za kuomba kuchukua fomu kuanzia Agosti 30, 2025.

Wakati mchakato huo ukiendelea, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), inatarajia kutumia Sh12 bilioni katika shughuli zote za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. 

Akizungumza leo Agosti 28, 2025 Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Thabit Idarous Faina amesema dimba la uchukuaji fomu litafunguliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho mtiania wake wa urais atachukua fomu Agosti 30, saa 4: 00 asubuhi katika ofisi za Tume hiyo.

Siku hiyohiyo pia Chama cha National League for Democracy (NLD) kitachukua fomu saa 5:00 asubuhi, Chama cha  Alliance for African Farmers Party (AAFP) kitachukua fomu saa 6:00 mchana na Chama cha Wananchi (CUF) kitachukua fomu saa 7:00 mchana na saa 8:00 mchana kitachukua Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) huku saa 9:00 alasiri watafunga siku hiyo kwa kutoa fomu kwa chama cha NRA. 

Kwa mujibu wa Faina, Agosti 31, 2025 wataanza na chama cha NCCR Mageuzi saa 3:00 asubuhi, saa 4:00 asubuhi itakuwa ni Chama cha ACT Wazalendo huku saa 5:00 asubuhi watakuwa na chama cha Kijamii CCK, kikifuatiwa na Chama cha DP ambacho kitachukua fomu saa 6:00 mchana.

Amesema katika uchukuaji wa fomu lazima mwombaji apate namba maalumu ya malipo (control number) kwa ajili ya kulipia na tayari vyama vyote 17 vimeshachukua namba ya malipo kwa ajili ya fomu hizo.

Hivyo, mtiania anapokwenda kuchukua fomu lazima aoneshe malipo hayo ambapo kwa mgombea urais analipa Sh100,000 kwa upande wa wanaume na mwanamke analipia Sh50,000, huku upande wa wawakilishi wanalipia Sh50,000.

“Sambamba na hilo, mtiania huyo atakwenda na barua ambayo amepewa na chama chake kuonesha kwamba ameteuliwa ili kupewa fomu na mambo mengine yaendelee,” amesema.

Akizungumzia pingamizi kwa watiania, Faina amesema ni suala la kisheria lakini Tume imejipanga kuwa makini ili kuhakikisha kunakuwa na pingamizi zenye mashiko vinginevyo haitakuwa tayari kupokea ambazo hazina tija.

“Kwa upande wa ujazaji wa fomu tumehakikisha mgombea anajiridhisha mwenyewe kutoka kifungu cha kwanza hadi cha 89 kama amevijaza kwa usahihi au vinginevyo, ikimaliza kama mgombea amedanganya basi mgombea mwingine anaweza kumwekea pingamizi,” amesema. 

Amesema kuna mambo matatu katika kuwekeana pingamizi ikiwa ni pamoja na kutokueleweka kwa taarifa zilizojazwa na muhusika, kama kuna udanganyifu wa kwenye fomu na iwapo wakijaza ukweli mtupu basi hakutakuwa na pingamizi litakalopenya.

“Ni vyema wagombea tukawasisitiza wakawa wakweli wakajaza na kuhakikisha wanahakiki ili kama kuna kitu amekisahau akijaze tena,” amesema.

Kwa upande wa watiania wa uwakilishi na madiwani, watachukua fomu katika ofisi za wilaya utaratibu ni uleule wa kuandika barua kuomba siku na muda wa kwenda kuchukua fomu.

Amesema wanaweka muda makusudi ili wakienda wakute watendaji wa tume wamejiandaa kuwahudumia kwa wakati na usahihi.

Amesema Tume inatarajia kutumia Sh12.260 bilioni kwa ajili ya kuendesha shughuli za uchaguzi ambapo fedha hizo zinatoka Mfuko Mkuu wa Serikali, ambapo tayari asilimia 71 imeshapewa Tume kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.

Amesema kwa mujibu wa mtiririko wa uingizaji wa fedha, wanategemea kupokea kiwango kingine kilichobaki Septemba mwaka huu ambacho ndicho kitatumika Oktoba.

Amesema wanatarajia kuendesha uchaguzi huru, haki na uwazi ambapo katika uwazi ni kuwashirikisha waandishi wa habari na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa.

Amefafanua kuwa wamepokea maombi ya waangalizi wa ndani na nje 34 kati ya hao 32 ni wa ndani na wawili ni wa kimataifa.
“Tumejipanga kila mwangalizi anapewa na sare kutoka ZEC ili wasihangaike na kupata vifaa vyao, na tunatarajia kuhakikisha tunafanya kwa viwango vya hali ya juu,” amesema.
Amesema wamejifunza kutokana na changamoto za chaguzi zilizopita ili kuweka mazingira mazuri.

Katika mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika jana Agosti 27, 2025, wadau hao licha ya kuonesha kuridhishwa mpaka sasa na hatua za uchaguzi, lakini walitoa uangalizi kuhakikisha haki na usawa unatendeka ili kufanyika uchaguzi wenye tija.

Mohamed Ali kutoka Chama cha Ada Tadea, amesema iwapo kutakuwa na usawa katika uchaguzi huo huenda ukawa bora kuwahi kutokea tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa uwepo.