Kyiv. Shambulio limefanywa na Jeshi la Russia nchini Ukraine, limeuwa watu wanne wakiwemo watoto wawili na kujeruhi wengine 30.
Shambulio kubwa la pamoja likihusisha ndege zisizo na rubani (drone) na makombora limetokea leo, Alhamisi ya Agosti 28, 2025, katika jiji la Kyiv.
Shambulio hilo linatajwa kuwa la kwanza kubwa la aina hiyo tangu Rais wa Marekani, Donald Trump, alipokutana na Rais wa Russia, Vladimir Putin, huko Alaska nchini Marekani mapema mwezi huu kwa mazungumzo ya kutafuta suluhisho la kumaliza vita vya miaka mitatu nchini Ukraine.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press (AP), taarifa ya awali iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine, Ihor Klymenko, imeeleza kuwa miongoni mwa waliopoteza maisha katika shambulio hilo ni watoto wawili.
Huku akitahadharisha kuwa huenda idadi ya vifo ikaongezeka, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine, Ihor Klymenko, amesema bado kuna watu waliokwama chini ya vifusi vya majengo yaliyoharibiwa na mashambulizi hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Utawala wa Jiji la Kyiv, Tymur Tkachenko amesema kwamba Russia ilirusha ndege zisizo na rubani pamoja na makombora ya balestiki yaliyolenga jiji hilo, na kuathiri maeneo 20 katika wilaya saba za Kyiv.
Ameeleza kuwa mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu mkubwa kwa zaidi ya majengo 100, yakiwemo makazi ya watu na jengo kubwa la biashara lililoko katikati mwa jiji, ambapo idadi kubwa ya madirisha yake yalivunjika kutokana na mshituko wa milipuko hiyo.
“Shambulio limehusisha ndege zisizo na rubani, makombora ya kusafiri, makombora ya balestiki, katika mwa jiji,” amesema Tkachenko.
Ameongeza kuwa shambulio hilo limesababisha moto kwenye jengo la makazi ya watu lililo na urefu wa ghorofa tano katika wilaya ya Darnytskyi.
Shambulio hili pia limeharibu miundombinu ikiwemo reli, na kupelekea ucheleweshaji na matumizi ya njia mbadala kama ilivyoelezwa na Shirika la Reli ya kitaifa la Ukraine, Ukrzaliznytsia.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa mataifa ya magharibi wamemshutumu Putin kwa kulegalega katika juhudi za kutafuta amani huku wanajeshi wa Taifa lake wakizidi kuingia nchini Ukraine.
Imeandikwa na Elidaima Mangela (UDOM) kwa msaada wa mashirika ya habari ya nje.