Dar es Salaam. Mkazi wa Pangani mkoani Tanga, Hamisi Bali amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka moja ya kughushi wosia.
Bali amesomewa shtaka hilo leo Agosti 28, 2025 na wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube
Akimsomewa shtaka, wakili Mafuru amesema Bali anadaiwa kutenda kosa hilo Februari 5, 2010 eneo la Temeke.
Amedai kuwa siku hiyo ya tukio, kwa nia ovu mshtakiwa alighushi wosia wa Februari 5, 2010 na kuusaini kwa jina la Seleman Iddi Seleman kwa lengo la kuonyesha kwamba mtu huyo aliacha wosia, huku akijua si kweli.
Bali baada ya kusomewa shtaka hilo, alikana kulitenda na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Pia, mshtakiwa ameomba apatiwe dhamana kwa kuwa shtaka linalomkabili lina dhamana.
Hakimu Makube ametoa masharti matatu ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo ambayo ni awe na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria.
Wadhamini hao wanatakiwa wawe na vitambulisho vinavyowatambulisha makazi yao na kusaini bondi ya maneno ya Sh10 milioni kila mmoja. Pia, wadhamini hao wawe ni wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam na sio vinginevyo.
Mshtakiwa amefanikiwa kukamilisha masharti ya dhamana na kuachiwa kwa dhamana. Na kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 17, 2025 kwa ajili ya kutajwa.