KUANZIA sasa na kuendelea, hapa kijiweni tumekubaliana kutoendelea na mjadala kumhusu mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize na suala lake la kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Uamuzi wa Mzize kuongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia timu hiyo tunadhani ameamua kutupa majibu tufanye yanayotuhusu na suala la yeye wapi acheze linabakia katika uamuzi wake.
Tunapaswa kufahamu tunachokijadili kuhusu Mzize kutumia fursa ya kwenda nje au kutokwenda ni maoni tu au ushauri ambao siyo lazima aufanyie kazi au asiufanyie.
Hadi ameamua kubaki Yanga basi kuna mambo ambayo yeye mwenyewe ameyaona yana faida kwake kuliko hata huko ambako wengi wanamshawishi aende wakiamini atapata malisho ya kijani zaidi.
Nimeona hoja pia ya watu kuilaumu Yanga imembania Mzize kwa kutomuuza na wanaamini inapaswa kuwaiga watani zao Simba ambao mara kwa mara huwa ni wepesi kuwauza wachezaji wanapohitajika nje ya nchi.
Hata hivyo, tunapaswa kuelewa hizi ni klabu mbili ambazo zina maisha na tamaduni tofauti na hakuna ulazima wa kinachofanywa na upande mmoja kifanywe na upande mwingine.
Mwisho kabisa jamani hapa Bongo ni patamu sana. Inawezekana hizi raha ambazo zipo hapa nchini mwetu ndio zimemfanya kijana aamue kubakia pale katika mitaa ya Twiga na Jangwani kwa mwaka mmoja zaidi.
Tukumbushane, kiasili sisi binadamu wengi tunapenda raha na hasa katika nchi kama yetu ambayo ukishakuwa na jina kubwa kwenye hizi timu zetu mbili kubwa unaishi maisha ya kifalme.
Si mnajua, huko kwa wenzetu hakuna hela ambayo unaweza kuipata kiandamizi kwa kupigiwa simu ukaifuate kwa tajiri au hata kupewa na shabiki wa kawaida pale unapotoa adhabu kwa mtani kwenye mechi ya dabi.