Dar es Salaam. Walalamikaji katika kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameibua shauri dogo jipya, wakiiomba Mahakama iwaamuru walalamikiwa wawapatie nyaraka za chama hicho ili wazitumie kama ushahidi kuthibitisha madai yao.
Kwa upande wao, walalamikiwa kupitia jopo la mawakili wameiomba Mahakama iwape muda wa siku saba kuwasilisha kiapo kianzani kujibu maombi hayo, huku wakibainisha kuwa katika kiapo hicho watayapinga maombi hayo.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini ya chama hicho kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema waliosajiliwa, pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa na katiba ya chama hicho.
Vilevile, wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na utoaji wa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kesi hiyo ilipangwa leo, Agosti 28, 2025, kwa ajili ya kuandaa hoja zinazobishaniwa kutokana na madai yaliyoainishwa kwenye shauri hilo, ambazo zitaiongoza Mahakama kufikia uamuzi kulingana na ushahidi utakaotolewa na pande zote, idadi ya mashahidi wa pande zote na muda wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Hata hivyo, wakili wa walalamikaji, Shaban Marijani, akishirikiana na mawakili Gido Simfukwe na Alvan Fidelis, aliieleza Mahakama kuwa wamefungua shauri jipya la maombi ya nyaraka muhimu kutoka kwa walalamikiwa, ambazo wanakusudia kuzitumia katika kesi hiyo kuthibitisha madai yao.
Kwa mujibu wa hati ya maombi ya shauri hilo, walalamikaji wanaomba wapewe na chama hicho nyaraka saba tofauti, zikiwamo zinazoonesha mali zinazomilikiwa na chama, za kifedha na za vikao kwa kipindi cha miaka sita kuanzia 2019 hadi 2024.
Nyaraka zinazoombwa ni Tamko la Mwaka la Mali zinazomilikiwa na chama hicho, taarifa za fedha zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mihutasari ya vikao vya Bodi ya Wadhamini wa Chadema.
Nyingine ni mihutasari ya ajenda za vikao vya Kamati Kuu, mihutasari yote ya ajenda za vikao vya Kamati Maalumu ya Zanzibar, mihutasari yote ya ajenda za vikao vya Sekretarieti ya Ofisi ya Makao Makuu ya Chadema – Zanzibar.
Taarifa nyingine ni za kibenki za akaunti namba 011103010075 yenye jina Chama cha Demokrasia na Maendeleo iliyoko Benki ya NBC.
Wakili Marijani amesema wameshawapatia walalamikiwa nyaraka za shauri hilo. Wakili wa walalamikiwa, Hekima Mwasipu, amesema walipatiwa nyaraka hizo Agosti 26, 2025.
Marijani ameomba kesi ya msingi isimame kwanza kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa shauri hilo la maombi ya nyaraka kwa kuwa zina athari katika mwenendo wa kesi ya msingi, hoja ambayo imeungwa mkono na wakili Mwasipu.
Jaji Mwanga anayesikiliza kesi hiyo amewapa siku saba walalamikiwa (wajibu maombi) kuwasilisha kiapo kinzani, akielekeza wakiwasilishe mahakamani hapo Septemba 4, 2025.
Pia amewapa walalamikaji (waombaji) siku tano kuwasilisha majibu ya ziada kama yatakuwapo dhidi ya kiapo kinzani, yaani Septemba 9, 2025, huku akipanga kusikiliza shauri hilo Septemba 10, 2025.
Jaji Mwanga ameelekeza kesi ya msingi itajwe Septemba 10, kwa ajili ya amri muhimu kuhusu usikilizwaji wake.
Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanaomba Mahakama itoe hukumu na kutamka kuwa walalamikiwa wamekiuka kifungu cha 6A (1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258, Marejeo ya mwaka 2019, na iwaelekeze wakizingatie kifungu hicho.
Vilevile, wanaiomba Mahakama itamke kuwa ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Amri nyingine wanayoomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwa na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.
Mahakama pia inaombwa itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hicho hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika, na iwaamuru wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo.
Wakati kesi hiyo ikisubiri kusikilizwa na kuamuliwa, Chadema kimezuiwa kufanya shughuli za siasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo itakapoamuliwa.
Zuio hilo linawafunga viongozi wa chama hicho ngazi zote kuanzia Taifa mpaka chini, wanachama na watumishi wa kawaida, mawakala wake na mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba au kwa maelekezo ya walalamikiwa.
Amri hizo za zuio zilitolewa na Jaji Mwanga Juni 10, 2025, kufuatia shauri la maombi madogo ya zuio lililofunguliwa na walalamikaji, wakiomba Mahakama itoe amri za zuio hilo la muda kusubiri kumalizika kwa kesi yao.
Shauri hilo lilisikilizwa na kuamuliwa upande mmoja baada ya mmoja wa mawakili wa Chadema aliyefika mahakamani hapo siku hiyo, Jebra Kambole, kujitoa muda mfupi baada ya Mahakama kutupilia mbali kiapo kinzani cha wadaiwa, kilichopinga maombi hayo kutokana na kasoro za kisheria.
Walalamikiwa waliandika barua kumkataa Jaji Mwanga wakimtaka ajitoe katika kesi hiyo, lakini baada ya kusikiliza hoja zao alikataa kujitoa, akisema sababu zao hazikuwa na mashiko kwani hazikuwa miongoni mwa zilizobainishwa kisheria kumfanya jaji au hakimu kujitoa kwenye kesi.
Walalamikiwa pia walifungua shauri la marejeo, wakiiomba Mahakama iondoe amri zake za zuio wakidai zilitolewa isivyo halali.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, pamoja na mambo mengine walalamikaji walieleza hawakupewa haki ya kusikilizwa baada ya wakili wao kujiondoa.
Hoja zao zilipingwa na jopo la mawakili wa walalamikaji, wakidai hazina mashiko na kwamba walipewa nafasi ya kusikilizwa lakini hawakuitumia.
Jaji Mwanga, katika uamuzi alioutoa Agosti 18, 2025, alitupilia mbali shauri hilo baada ya kukataa hoja za chama hicho, akieleza hazikuwa na mashiko kisheria.
Alisema walipewa fursa ya kusikilizwa lakini hawakutaka kuitumia. Alifafanua kuwa, wakati Mahakama inapanga tarehe ya usikilizwaji wa maombi ya zuio, walalamikiwa na mawakili wao walikuwapo mahakamani, lakini siku ya usikilizwaji hawakufika.
Hivyo, alisema halikuwa jukumu la Mahakama kuwatafuta walalamikiwa mahali walikokuwa baada ya wakili wao kujitoa.