Mao ajiandaa kuitema KMC | Mwanaspoti

KIUNGO mshambuliaji wa KMC, raia wa Somalia, Ibrahim Elias ‘Mao’, huenda akaachana na timu hiyo baada ya mazungumzo ya kusaini mkataba mpya kuingia dosari, huku ikielezwa makubaliano imeshindikana kufikiwa baina ya pande hizo zote mbili.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Mao hatokuwa sehemu ya timu hiyo kutokana na kutokubaliana kwa baadhi ya vifungu vya kuboreshewa maslahi mapya, jambo linalochochea kufunguliwa mlango wa kutokea ili akatafute changamoto mpya.

Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo kimeliambia Mwanaspoti Mao ana uwezekano wa kutoongeza mkataba mpya, huku sababu kubwa ambayo inadaiwa ni kutokana na majeraha ya mara kwa mara, ambayo kwa msimu uliopita wa 2024-2025, yalichangia kukaa nje.

“Suala sio maslahi kwa sababu hatujashindwa kumlipa, ishu kubwa hapa inayochangia ni rekodi yake ya majeraha ya mara kwa mara aliyokuwa nayo, ni mchezaji mzuri tunayemuheshimu sana, japo ni vigumu kuendelea naye pia,” kilisema chanzo hicho.

Nyota huyo kwa mara ya kwanza alijiunga na KMC msimu wa 2023-24, akitokea Kibra United ya Kenya, ambapo msimu wake wa kwanza alifunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara, ambayo ni idadi sawa ya mabao pia aliyoyafunga kwa msimu wa 2024-2025.

Kiungo huyo kwa msimu wa 2024-2025, alikuwa nje kwa muda mrefu na kushindwa kuitumikia timu hiyo kutokana na majeraha ya mara kwa mara, ambapo bao la mwisho la Ligi Kuu alifunga KMC ilipochapwa kwa mabao 2-1 dhidi ya Namungo, mechi iliyopigwa Aprili 6, 2025.