Dar es Salaam. Hatua ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kutoa magari kwa wagombea wa nafasi ya urais 2025, wataalamu wa sheria wameibuka wakihoji ni sheria gani imetumika, tume yenyewe ikijibu hoja hiyo
Japo wengine wamedokeza kwa kuwa magari hayo hayatampunguzia jambo lolote mgombea hakuna tatizo.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele amesema walichofanya ni kukuza demokrasia.

“Sisi tulichofanya ni kukuza demokrasia tunataka uwanja uwe sawasawa kwa sababu kumekuwa na malalamiko kwamba wagombea hawapo kwenye usawa, wengine wanasema Rais aliyepo madarakani ana faida ya kuwa na magari sasa magari haya tumeyatoa kuweka uwanja kuwa sawa,” amesema.
Agosti 28, 2025 jijini Dodoma kulingana na ratiba ya INEC, wagombea waliokidhi vigezo waliteuliwa na tume hiyo na kila mgombea aliyekidhi vigezo alikabidhiwa gari jipya lenye mafuta yaliyojaa tanki (kwa mujibu wa madereva).
Wagombea hao wamepewa madereva wa Serikali na ulinzi katika kipindi chote cha kampeni hadi siku ya kutangazwa matokeo.
“Gari hili unapewa kwa ajili ya kampeni, kumbuka ni mali ya Serikali, ila unaruhusiwa kubadilisha stika kwa gharama zako, na utazitoa kwa gharama zako,” alisema kwa kurudia, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima wakati akiwakabidhi magari hayo kwa nyakati tofauti.
Hata hivyo, Kailima hakutoa ufafanuzi wa nani anahudumia magari hayo kwenye mafuta huko mikoani na kama gari litaharibika.

Kailima akizungumza jana wakati akikabidhi gari na masharti kwa mgombea wa CUF, amesema uamuzi wa kutoa magari kwa wagombea ni baada ya kuona baadhi ya vyama vilikuwa na nguvu ndogo ya kufika katika maeneo yote.
“Tunakupa gari hili jipya, tunakupa na dereva na mlinzi, gari hili ni mali ya Serikali. Litakusaidia katika kipindi chote cha kampeni, na hii inaondoa lawama kwamba baadhi ya wagombea wasingeweza kufika maeneo mengine kwa changamoto za usafiri,” amesema Kailima.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya jambo hilo, Kailima alisema baada ya shughuli zote kukamilika si muda wa kuzungumza, kwani kazi imekwisha.

Akizungumzia hatua hiyo, Wakili Ibrahim Bendera amesema hakuna sehemu tume hiyo ina mamlaka ya kutoa vifaa kuwezesha wagombea.
“Jambo lililofanyika halipo kisheria, lakini kama jambo hilo halimpunguzii mgombea kitu wakati wa kugombea hakuna shida, tunaangalia dhumuni kama aliyepewa karidhika ni sawa,”amesema.
Hoja hiyo ni tofauti na alichosema Wakili Edson Kilatu akisistiza INEC inapaswa kusimamia fursa sawa wakati wa kampeni, kuwapatia wagombea wote ulinzi na ugawaji gari ni jambo jipya.
“Kuwezesha vyama kwa kufuata utaratibu inaweza kuwa ni njia ya kukuza demokrasia na ushindani, shida ni fedha zilizotolewa (gari) ni mali za umma na mali ya umma haiwezi kutolewa bila kufuata utaratibu kwa sababu ukaguzi utafanyika kwa namna gan,i na hapo uwajibikaji ukoje…? amehoji wakili Kilatu.
Wakili huyo ameongeza kuwa itakuaje kwa wagombea wa nafasi ya ubunge na udiwani au wenye uhitaji maalumu.
Amesema ni lazima fedha za umma zinazotolewa zifuate utaratibu wa kisheria, akihoji kwenye bajeti ya uchaguzi mwaka huu hakukuwa na kipengele cha wagombea kuwezeshwa magari.

Mtazamo huo unaendana na wa Mwanaharakati Martin Masese aliyesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 74(6) imeeleza majukumu ya tume hiyo yameanishwa kisheria na kilichofanyika ni uvunjifu wa sheria
“Kulingana na katiba, majukumu ya tume ni kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Rais na wabunge katika Jamhuri ya Muungano.
Masese amesema kulingana na katiba hiyo, Tume ina wajibu wa kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na wabunge; kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge.
Vilevile kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapigakura na uendeshaji wa uchaguzi wa madiwani; na kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge, hivyo kilichofanyika hakina uhalali kwa mujibu wa sheria.
“Kilichofanyika kwa kuwa hakipo kwa mujibu wa sheria, hizi ni fedha za umma matumizi yake kapanga nani,
Serikali kuingia gharama ya kuwatafutia usafiri wagombea ni matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma,” amesema.
Kwa upande wake Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Dk Paul Loisulie amesema kilichofanywa na INEC kimeleta mkanganyiko kwa wananchi.
“Mkanganyiko uliopo kama chama cha siasa hakijitoshelezi imewezaje kumdhamini mgombea, halafu bado vyama vyenyewe vitapata tafsiri kuwa wagombea sio wapinzani bali wapo tu,” amesema.

Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na 2 ya mwaka 2024 kifungu cha 10(1) (2) inafafanua kuwa kuzingatia matakwa ya Ibara za 74(6), 75 na 78 za Katiba, Tume itakuwa na majukumu yafuatayo:
kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na uchaguzi wa Madiwani kwa Tanzania Bara;
kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na Wabunge na uchaguzi wa Madiwani kwa Tanzania Bara; kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za vijiji, mitaa na vitongoji Tanzania Bara kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika Sheria itakayotungwa na Bunge;
Vilevile, kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge; kuteua na kuwatangaza Wabunge Wanawake wa Viti Maalumu katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani Wanawake wa Viti Maalumu kwa Tanzania Bara;
Kuandaa na kusimamia Kanuni za Maadili ya Na.2 Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi 2024 9 Uchaguzi; kutoa elimu ya mpiga kura nchini; (h) kuratibu na kusimamia taasisi na asasi zinazotoa elimu ya mpiga kura; kualika na kusajili waangalizi wa uchaguzi;
Sura ya 298(j) kuajiri au kuteua watumishi na watendaji wa Tume kwa kadri itakavyohitajika kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Utumishi wa Umma na masharti mengine yatakayowekwa na Tume; na kutekeleza majukumu mengine yoyote kama yalivyoainishwa kwenye Katiba au sheria nyingine yoyote.