Dodoma. Serikali imeahidi kumaliza vikwazo vyote kwa wafanyabiashara wa mazao ya samaki, ikiwemo wanaosafirisha nje ya nchi ili biashara hiyo ilete tija kwa uchumi wa nchi.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uvuvi nchini, Dk Baraka Sekadende jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na washiriki wa kongamano la tathimini baada ya utafiti kuhusu mazao ya samaki.
Warsha hiyo iliitishwa na Shirika la Maendeleo la Kilimo la Afrika Mashariki (Kilimo Trust) ambapo wataalamu, wafanyabiashara na maofisa wanaoshughulikiwa samaki walishiriki kwenye warsha hiyo.
Baraka amesema biashara ya samaki ndani na nje ya nchi ni lazima itazamwe na kusimamiwa kwa umakini mkubwa kutokana na ukweli kuwa imekuwa na manufaa na tija, hivyo isipoangaliwa haiwezi kuwasaidia watu kujikwamua.
“Lazima tutafute namna bora ya kuondoa vikwazo kwenye biashara hii, haiwezekani eneo linalozalisha ajira nyingi kiasi hiki likaachwa kama lilivyo ambapo manung’uniko yanazidi kila wakati.”
Kwa mujibu wa Dk Sekadende, katika kipindi cha 2024 zaidi ya Sh4.68 trilioni zilipatikana kutokana na mazao ya samaki ambapo tani 566,738 zilivunwa.

Rachel Ajambo Msimamizi wa Shirika la Kilimo la Afrika Mashariki (Kilimo Trust)
Mfanyabiashara wa samaki, Kulimushi Bertin kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC), amesema kikwazo kikubwa wanachokutana nacho katika kusafirisha samaki sangara ni vikubwa hasa akitaja eneo la boda ya Mwanza, ambako kila uchao lazima wanakaguliwa si chini ya saa tatu tofauti na maeneo mengine.
“Serikali hatuilaumu, imefanya kazi na kutimiza wajibu wake, lakini kinatuumiza hili la kukaa muda mwingi boda hata kama utakuwa umekamilika kwa kila kitu hivyo Serikali itusaidie,” amesema Bertin.
Msimamizi wa mradi wa Kilimo Trust, Rachel Ajambo amesema mpango mkakati waliojiwekea ni kuwajengea uwezo vijana na kina mama ili waweza kujiajiri, lakini kufanya biashara zao bila vikwazo.