Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, Grey Chilaza na mwenzake, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kulisababishia hasara ya Sh1.5 bilioni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL ).
Mbali na Chilaza, mshtakiwa mwingine ni Alex Ngonyani ambaye ni mkazi wa Mbinga mkoani Ruvuma.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi Agosti 28, 2025 na kusomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali, Tumain Mafuru mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Hassan Makube.
Akiwasomea mashtaka hayo, wakili Mafuru amedai kati ya Machi 2023 hadi Oktoba, 2024, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washitakiwa wote kwa pamoja kwa nia ovu, waliongoza genge la uhalifu na kuiba Sh1.5 bilioni, mali ya TTCL.
Inadaiwa pia, katika tarehe hizo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washtakiwa hao waliingilia mfumo wa kompyuta wa T-pesa na kuiba kiasi hicho cha fedha.
Pia washtakiwa hao, katika tarehe hizo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walitakatisha Sh1.5 bilioni kwa kuidhinisha kutoka mfumo wa T-Pesa kwenda katika akaunti ya simu huku wakijua fedha hizo zilitokana na kosa tangulizi la wizi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na kesi ya uhujumu uchumi na shitaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi haujakamilika na kuomba mahakama iwapangie tarehe nyingine ya kutajwa
Hakimu Makube amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirishwa kesi hiyo hadi Septemba 8, 2025 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamepelekwa mahabusu.