CAF yailainishia KMKM kombe la shirikisho

UNAWEZA kusema KMKM imelegezewa kamba katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika 2025-2026 baada ya wapinzani watakaokutana nao katika raundi ya kwanza, AS Port ya Djibouti kuchukua uamuzi wa mechi zote kupigwa visiwani Zanzibar.

Meneja wa KMKM, Khamis Haji Khamis amesema wamepewa taarifa kwamba AS Port imepeleka barua Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuomba mechi mbili za raundi ya awali zichezwe kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Khamis amefafanua, timu hiyo imeeleza sababu mbili kuu kutaka mechi hizo zichezwe kisiwani hapa ikiwamo kutokuwa na uwanja uliokidhi kucheza mechi hizo na suala la usalama halipo vizuri nchini kwao.

Alisema timu hiyo imetoa masharti kwa KMKM kupatiwa hoteli kwa ajili ya kukaa na usafiri kitendo ambacho klabu hiyo imekubali.

“Wapinzani wetu wameomba mechi zote mbili zichezwe Zanzibar na masharti waliyoyatoa tumeyakubali ikiwamo kutafuta hoteli na usafiri, vyote vipo isipokuwa masuala mengine yatabaki katika majukumu yao,” alisema Khamis.

Alisema katika mchezo wa pili ambao wao watakuwa wenyeji, watahakikisha kila kitu kimekamilika mapema ili kusitokee usumbufu.

Kwa mujibu wa CAF, KMKM na AS Port zitakutana kati ya Septemba 19-21 ikiwa ni mechi ya kwanza na marudiano ni kati Septemba 26-28 mwaka huu.

Mshindi wa jumla, atacheza hatua inayofuata kuwania kufuzu makundi dhidi ya mshindi kati ya Azam na Al Merreikh Bentiu Juba ya Sudan Kusini.

Wakati KMKM wakipata zali hilo, msimu uliopita timu mbili za Zanzibar zilizoshiriki mashindano ya CAF, JKU na Uhamiaji ziliamua mechi zao zote za hatua ya awali zichezwe nyumbani kwa wapinzani wao.

JKU iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, ilipambana na Pyramids ya Misri na kupoteza mechi zote ikianza kufungwa 3-1, kisha 6-0. Jumla iliondoshwa kwa mabao 9-1. Uhamiaji iliyokuwa Kombe la Shirikisho, ilifungwa 3-1 na 2-0, na Al Ahly Tripoli ya Libya (jumla 5-1).