Kocha Azam FC aishtukia Yanga

KOCHA wa zamani wa Azam FC, Bruno Ferry ameula huko Angola baada ya kupewa mkataba wa miaka miwili kuinoa Wiliete Benguela itakayovaana na Yanga katika mechi za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akisema anajua kibarua alichonacho mbele ya wababe hao wa Bara.

Bruno, ambaye pia ni kocha wa makipa aliwahi kuinoa Azam kwa kushirikiana na kocha Youssouph Dabo kabla msimu wa 2024–2025 kujiunga na AS Vita ya DR Congo, ambako Bruno alianza kama kocha msaidizi na kisha kupandishwa kuwa kocha mkuu.

Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya kutambulishwa rasmi na Wiliete, Bruno alisema nafasi hiyo mpya ni changamoto kwake na timu yake.

“Najisikia fahari kujiunga na Wiliete. Ni klabu yenye malengo makubwa, na nimekuja hapa kuhakikisha tunasonga mbele na kuandika historia mpya,” alisema Bruno

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 58 aliongeza maandalizi kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika yataanza mapema ili kuhakikisha kikosi chake kinakuwa katika hali bora kwani mechi dhidi ya Yanga haiwezi kuwa rahisi kwa vile ameshawahi kukutana nayo na kujua inavyocheza kwa juhudi.

“Tumeanza maandalizi kwa nguvu kubwa. Tunajua tuna mechi ngumu dhidi ya Yanga, ambayo ni timu kubwa barani Afrika. Lazima tuwe tayari kiakili na kimwili,” alisema Bruno, aliyekiri kuwa anatambua ubora wa Yanga na rekodi yao katika michuano ya CAF, japo alidai hana hofu nao.

“Yanga ni timu yenye uzoefu mkubwa, lakini sisi hatutakuwa na hofu. Tutashindana na kuonyesha uwezo wetu,” alisema Mfaransa huyo.

Kuhusu uzoefu wake barani Afrika, Bruno alisema umemjenga na kumpa uwezo wa kushindana kwenye michuano mikubwa.

Miongoni mwa washambuliaji hatari wa chama hilo jipya kwa Ferry ni pamoja na Joao Chingando Manha ‘Kaporal’ ambaye alipachika mabao mawili katika mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) akiwa na timu ya taifa la Angola.

Lakini pia timu hiyo ina nyota wa zamani wa Yanga, Mahlatsi Makudubela maarufu kama Skudu.

Wiliete SC na Yanga SC zinatarajiwa kukutana katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi ujao, mechi ya mkondo wa kwanza itacheza Septemba 20 huku marudiano yakiwa Septemba 27 jijini Dar es Salaam.