Yanga, Simba zagawana viwanja Dar

MUDA mfupi baada ya Bodi ya Ligi kutangaza ratiba ya Ligi Kuu Bara, imethibitisha kuwa Yanga imebadili uwanja wa nyumbani na sasa itatumia ule wa Mkapa, huku Simba ikibaki KMC Complex, Mwenge vyote jijini Dar es Salaam.

Msimu ulioisha Simba na Yanga zote zilikuwa zinatumia Uwanja wa KMC kama uwanja wa nyumbani,lakini sasa Mnyama ndio kabaki hapo kama ilivyokuwa mwanzo kabla ya Yanga kuukimbia Uwanja wa Chamazi na kumfuata mtani wake wa jadi.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo ya ligi ambayo inatarajia kuanza kutumika Septemba 17 kwa mechi mbili za ufunguzi ambazo zitapigwa viwanja viwili tofauti – KMC itakuwa mwenyeji wa Dodoma Jiji mchezo utakaopigwa Uwanja wa KMC na mchezo mwingine utakuwa kati ya Coastal Union dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Mkwakwani – Tanga.

Kwa mujibu wa ratiba, Yanga itaanza kwenye uwanja wa nyumbani ikiikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkapa  wakati Simba itaanzia ugenini dhidi ya Tabora United.

Mechi hizo za kwanza kwa watani zitapigwa Septemba 18 ambapo pia kutakuwa na mechi kati ya Fountain Gate dhidi ya Mbeya City mchezo utakaopigwa saa nane mchana, Mashujaa itakuwa mwenyeji wa JKT Tanzania na Uwanja wa Majaliwa kitapigwa kati ya Mashujaa dhidi ya Pamba Jiji.

Ukiondoa hilo kwenye ratiba hiyo inaonyesha mchezo wa kwanza wa Coastal Union na Tanzania Prisons utacheza saa moja usiku katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Wakati huohuo Uwanja wa JKT Tanzania sasa utapangiwa mechi za usiku huku ikionyesha mchezo wa kwanza muda huo utachezwa katika mzunguko wa tatu ukikutanisha wenyeji JKT Tanzania dhidi ya Azam FC kuanzia saa moja.