Kocha AS Port aichimba mkwara KMKM

KOCHA wa AS Port ya Djibouti, Seninga Innocent ameichimba mkwara KMKM ambayo watakutana nayo kati ya Septemba 19 hadi 21, mwaka huu kwenye mechi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika mjini Unguja.

Seninga ambaye hivi karibuni aliondoka Etincelles ya Rwanda amesema timu yake ipo katika maandalizi ya mechi hiyo, huku akiamini ushindi utaongeza matumaini ya kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

“Tuna wachezaji wenye uzoefu na vijana wenye motisha, hivyo tunatarajia kuonyesha nguvu yetu visiwani Zanzibar,” amesema.

KMKM ambayo ni miongoni mwa wawakilishi wa Zanzibar kwenye mashindano ya CAF ilionyesha ubora katika Ligi Kuu  msimu uliopita, jambo ambalo linatoa changamoto kwa Seninga na kikosi chake.

Kocha huyo ameeleza kuwa uzoefu wa kimataifa ikiwa ni pamoja na kuinoa Gendermerie ya Djibouti na timu kadhaa za Rwanda, utasaidia kukabiliana na maafande hao na kupata matokeo chanya.

“Nina mambo ambayo nafahamu kuhusu wapinzani wangu na kwa bahati nzuri nimekuwa mfuatiliaji mzuri wa soka la Tanzania hata Zanzibar hivyo sidhani kama kutakuwa na tatizo hata kama mechi zote zitacheza Zanzibar,” amesema.

Kwa mujibu wa ratiba, AS Port itatua nchini wiki moja kabla ya mechi hiyo na kuweka kambi ya siku chache kabla ya kukabiliana na KMKM kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar ambako zitacheza mechi zote mbili.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa Julai 8, 2019 katika mashindano ya Cecafa na AS Port iliinyuka KMKM kwa mabao 2-0.