MAHAKAMA KUU imebariki hukumu inayolitaka Shirika la Ndege la Turkish Airlines, kumlipa Hassan Othman Hassan ‘Hassano’, aliyewahi kuwa kiongozi wa klabu ya soka ya Simba, fidia ya Sh36 milioni kutokana na mzigo wake kupotea aliposafiri na ndege ya shirika hilo.
Mizigo hiyo ni begi la nguo na vitu vingine, vilevile ndoo iliyokuwa na lita 10 za asali.
Shirika la Ndege la Turkish Airlines Inc. Ltd lina makao makuu katika Jiji la Istanbul, Uturuki na hufanya safari maeneo 340 katika nchi 129 duniani, Tanzania ikiwamo na lina ndege zaidi ya 400 na lina safari za ndani maeneo 53.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Aprili 26, 2023 Hassan alisafiri kwa ndege ya shirika hilo kutoka Dar es Salaam kwenda Casablanca, Morocco kushuhudia mechi ya kimataifa kati ya Simba na Wydad ya Morocco.
Awali, Hassan alifungua kesi ya madai namba 194 ya mwaka 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akiomba kulipwa fidia ya jumla ya Sh200 milioni kutokana na maumivu ya kisaikolojia aliyoyapata.
Pia, aliomba mahakama itoe amri kwa shirika hilo kumlipa fidia ya Sh50 milioni kutokana na uzembe, kulipa riba ya asilimia 21 ya fedha hizo tangu kesi ilipofunguliwa hadi mahakama itakapotoa hukumu.
Pia aliiomba mahakama itoe amri kuwa kwa namna shirika hilo lilivyoshindwa kushughulikia mzigo wake na kutotoa ushirikiano kwa mteja katika kuutafuta, ulikuwa uzembe na haikutimiza wajibu wao wa kuutunza.
Katika hukumu aliyoitoa Desemba 13, 2024, Hakimu Mkuu Mkazi, Benard Nyaki aliliamuru shirika hilo kumlipa Hassan fidia ya Sh36 milioni kutokana na mzigo kupotea.
Shirika hilo halikuridhishwa na hukumu likakata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania, kupinga hukumu hiyo. Jaji Awamu Mbagwa katika hukumu aliyoitoa Agosti 28, 2025 ameitupa akisema haina mashiko.
Katika hati ya madai, Hassan alieleza Aprili 26, 2023 akiwa ofisa wa Simba alisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Casablanca, Morocco kwa ndege namba TK0604 kwa ajili ya kuangalia mechi kati ya timu ya Simba na Wydad Casablanca.
Alidai katika safari aliingiza mzigo aliokuwa akisafiri nao Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jullius Nyerere (JNIA) akitarajia kuuchukua atakapofika Uwanja wa Ndege wa Casablanca.
Nadai aliunganisha ndege alipofika Istanbul, Uturuki, lakini alipofika kituo cha mwisho cha safari, alibaini mzigo hauonekani.
Hassan alidai mzigo ulikuwa na vitu mbalimbali zikiwamo nguo, jozi tatu za viatu zilizotengenezwa nchini Italia, dawa za shinikizo la damu na vidonda vya tumbo na zawadi kwa rafiki zake aliokuwa anakutana nao kwa miadi ya kibiashara.
Alidai licha ya kutoa taarifa Uwanja wa Ndege wa Casablanca, mzigo haukupatikana na hata aliporudi Dar es Salaam aliendelea kufuatilia, lakini juhudi zake hazikuzaaa matunda.
Shirika hilo lilipinga madai hayo na kudai hasara inayodaiwa na mteja wao ni kujichanganya, ilikuwa haijatokea na haina msingi wowote, kwani mlalamikaji alishindwa kuzingatia taratibu za lazima za madai ya mizigo.
Pia lilidai madai yake hayakuwa na msingi wowote wa kisheria kwani tatizo lilisababishwa na mteja mwenyewe kwa uzembe wake.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliona madai ya abiria yana msingi na yamethibitishwa, hivyo iliamuru shirika hilo kulipa fidia inayofikia Sh36 milioni kutokana na uzembe wa kushughulikia mzigo huo.
Shirika hilo halikuridhishwa na hukumu likakata rufaa likiegemea sababu sita, ikiwamo kwamba Hakimu alikosea kwa kushindwa kuchambua na kutathmini ushahidi uliotolewa na mlalamikaji, hivyo kufikia uamuzi usio sahihi.
Sababu nyingine, lilidai mahakama ilikosea kisheria kwa kutoa tuzo kwa Hassan ya Sh36 milioni na riba bila kuwapo kwa ushahidi wa kutosha, uthibitisho na uhalali unaohalalisha kulipwa fidia hiyo.
Shirika hilo lilidai mahakama ilikosea kisheria iliposhindwa kuchambua na kutathmini ushahidi uliokuwa umeletwa mbele yake na pia ilikosea kisheria kutamka ilizembea bila kuzingatia uasili wa mgogoro wenyewe.
Kupitia kwa wakili, Nathalia Michael shirika hilo lilijenga hoja kuwa mahakama ilikosea kisheria kutokana na ushahidi uliopo kwenye jalada la mahakama, hauungi mkono hitimisho ambalo hakimu alilifikia.
Wakili Michael alifafanua kuwa barua pepe iliyotumwa kwa mteja wao inathibitisha kuwa alijulishwa juu ya kufika kwa mzigo wake ofisi za Swissport Dar es Salaam Mei 8, 2023 ikiwa ni siku 15 tangu mzigo huo uwe hauonekani.
Alidai ucheleweshaji ulikuwa ni siku 15, hivyo fidia ambayo mahakama imeitoa haina uhalali, kwani sheria za kimataifa zinasema mzigo ukichelewa kwa siku 21 au zaidi, abiria ndipo anastahili kupewa fidia.
Hoja hizo zilipingwa na wakili Nehemia Mkoko aliyemwakilisha Hassan, akidai shirika hilo halikuwasilisha utetezi wowote wenye mashiko.
Jaji amesema baada ya kupitia mwenendo na hukumu ya shauri hilo, ni wazi mawasiliano yalikuwa baina ya Hassan na Swissport na hakuna ushahidi wenye mashiko kuwa shirika hilo liliwasiliana na mteja wake.
Amesema shirika hilo lilikuwa linawajibika kumjulisha mteja wake juu ya kupotea kwa mzigo wake lakini hata hivyo shahidi wao alipokuwa akitoa ushahidi, alikiri hakuna barua pepe aliyotumiwa Hassan, ikimjulisha kuwasili kwa mzigo.
Baada ya kupima ushahidi huo, amesema anakubaliana na hakimu aliyetoa hukumu hiyo kuwa mrufani (Turkish Airline) alishindwa kutimiza majukumu yake kwa uangalifu katika kushughulikia mzigo wa abiria kulingana na mikataba.
“Badala yake, mjibu rufaa katika shauri hilo alithibitisha kuhusu kuchanganywa au kupotea kwa mzigo wake, hadi wakati anatoa ushahidi wake mahakamani alikuwa hajakabidhiwa mzigo wake,” amesema.
Kuhusu madai ya shirika hilo kuwa kiwango cha fidia kilichotolewa kilikuwa kikubwa na hakina uhalali, jaji amesema mrufani anadai kiwango alichostahili hakikupaswa kuzidi Dola 1,311 za Marekani, lakini hilo haliifungi mahakama.
Amesema ibara ya 22(6) ya mkataba wa Montreal unaipa mahakama mamlaka ya kupima na kuamua shauri linaloletwa mbele yake na imesisitiza kuwa ibara hiyo ya 21 haizizuii mahakama za ndani ya nchi kutoa tuzo inaporidhika na madai.
Kutokana na uchambuzi jaji amesema hoja hizo za rufaa hazina mashiko na haoni sababu ya kubatilisha uamuzi wa hakimu aliyesikiliza na kutoa tuzo hiyo na kwamba, shirika hilo la ndege litawajibika kulipa pia gharama za kesi hiyo.