Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakuwa na muda wa wiki moja tu kujiandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zitaakzofanyika Morocco kutokana na uwepo wa mechi ya Dabi ya Kariakoo baina ya Yanga na Simba ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Desemba 13, 2025.
Mchezo wa marudiano baina ya timu hizo mbili umapengwa kufanyika Aprili4, 2026 ambao Simba itakuwa mwenyeji.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Ibrahim Mwayela amesema upangaji wa ratiba hiyo umezingatia mashindano yote ya ndani na nje.
“Tunatambua tuna ratiba ngumu kutokana na uwepo wa michuano mingi hivi karibuni lakini katika kuhakikisha tunakuwa na ratiba imara tumezingatia mashindano yote.
“Tunatarajia kumaliza ligi Mei 23 kama ratiba ilivyopangwa hakutakuwa na sababu ya mchezo wowote kuhairishwa hii ni kutokana na namna ambavyo ratiba imepangwa kwa kuzingatia mashindano yote,’ amesema Mwayela.
Alisema wanatambua ratiba itakuwa inabana lakini katika kuhakikisha ligi inaisha mapema wamezingatia muda wa kikanuni kupanga ratiba kwa kuzingatia mechi zote kuanzia wawakilishi wa kimataifa Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars.
“Ukiondoa wawakilishi hao pia tumezingatia timu kutoka kituo kimoja kwenda kingine kwa kuangalia kanuni na muda wa shirikisho la soka duniani hatutarajii malalamiko kutoka kwa klabu,” amesisitiza Mwayela.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Ligi Kuu msimu wa 2025/2026 itaanza Septemba 17, siku moja baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya Yanga na Simba.