Morogoro. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kuboresha huduma za afya, barabara na kilimo kwa wananchi wa Morogoro vijijini endapo atachaguliwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Katika eneo hilo, ameahidi ujenzi wa Barabara ya Bigwa – Kisaki kwa kiwango cha lami, ujenzi wa kituo kikubwa cha afya na ujenzi wa ghala la mazao.
Mgombea huyo ametoa ahadi hizo leo Agosti 29, 2025 katika eneo la Ngerengere, kilipo kituo cha treni ya SGR.
Amewasili Morogoro saa 4:20 asubuhi kwa kutumia usafiri wa reli ya kisasa (SGR) akitokea Dar es Salaam na kituo cha kwanza cha kampeni baada ya uzinduzi, kimekuwa ni Ngerengere.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais Samia amesema kituo cha Ngerengere ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa Morogoro vijijini ambao wengi ni wakulima, hivyo ameziagiza Wizara ya Kilimo na ile ya Uchukuzi kujenga ghala Morogoro.
“Kituo hiki kiwe na ghala la kuhifadhia mazao na urahisi wa kuyapeleka sokoni. Kwa hiyo naziagiza wizara za Kilimo na Uchukuzi kujenga ghala, Wizara ya Uchukuzi itoe ardhi na Wizara ya Kilimo ijenge,” amesema mgombea huyo.
Amesisitiza kwamba eneo hilo litakuwa ni ushoroba wa viwanda utakaochagizwa na uwepo wa reli ya kisasa.
Kwa upande wa barabara, Rais Samia amesema Serikali inajenga barabara ya Ubena Zomozi yenye urefu wa kilomita 24 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh20 bilioni.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo, mgombea ubunge katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ amemuomba Rais Samia kujenga barabara ya Bigwa – Kisaki kwa kiwango cha lami kwani kimekuwa ni kilio cha wananchi wa maeneo hayo.
“Barabara ya Ubena Zomozi, mkandarasi yuko kazini, barabara ya Bigwa – Kisaki, tunaomba tupate lami, najua umefanya mengi kwa wananchi wa Morogoro Vijijini, tunaomba na hii barabara tupate lami,” amesema.
Akijibu ombi hilo la mgombea ubunge, Rais Samia ameahidi kuijenga barabara hiyo kwa kuwa ni muhimu kwa wananchi wa Morogoro na pia kwake kwani ana mashamba yake huko.
“Barabara hii ni muhimu kwetu, tunakwenda kuijenga. Kwa hiyo, ahadi yetu kwenu, tunakwenda kuijenga barabara ya Bigwa – Kisaki kwa kiwango cha lami,” ameahidi mgombea huyo.
Kwa upande wa sekta ya afya, mgombea udiwani katika kata ya Ngerengere, Kibena Nassoro amemuomba mgombea urais akishinda awasaidie wapate kituo cha afya kikubwa kitakachokidhi mahitaji ya eneo hilo.
“Kituo cha afya tulichonacho ni kidogo, kinazidiwa kwa sababu kinategemewa na wananchi wa hapa pamoja na kambi za jeshi zilizopo hapa jirani. Tunaomba utupatie fedha kwa ajili ya kuboresha kituo hiki,” amesema mgombea huyo wa udiwani.
Akijibu hoja hiyo, Rais Samia ameahidi kujenga kituo cha afya kikubwa cha Ngerengere. Ameongeza kuwa katika miaka mitano iliyopita, Serikali imejenga vituo vya afya 67 katika eneo hilo.

Awali, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Morogoro, Joseph Masunga amesema mkoa huo utaweka viwango kwa mikoa mingine kufuata kutokana na hamasa waliyonayo wananchi wake kwa chama hicho.
Amesema mwaka 2020, mkoa huo ulishika nafasi ya kwanza kwa kutoa kura nyingi kwa mgombea urais, rekodi ambayo wanaitaka tena kwenye uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
“Morogoro ina rekodi ya kutoa kura nyingi za urais, mwaka 2020 tulishika nafasi ya kwanza, mwaka huu tunaitaka tena nafasi hiyo,” amesema mwenyekiti huyo.